*Waziri Majaliwa aenda kumwakilisha
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
RAIS Dk. John Magufuli ameendelea na uamuzi wake wa kutosafiri nje ya
nchi huku akilazimika kutuma ujumbe wa kumwakilisha katika mikutano ya
kimataifa.
Hatua hiyo inatokana na agizo lake alilolitoa Novemba 7, mwaka jana,
ambapo alipiga marufuku safari za nje ya nchi kwa maofisa wa Serikali
ila tu itakapokuwa lazima na kwa ruhusa ya Ikulu.
Kutokana na hali hiyo, safari hii amelazimika kumtuma Waziri Mkuu,
Kassim Majaliwa ili akamwakilishe katika mkutano wa wakuu wa nchi za
Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC), unaofanyika mjini
Gaborone nchini Botswana.
MAJALIWA BOTSWANA
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliwasili nchini Botswana juzi na
kupokewa na Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi wa nchi hiyo, Tshenolo
Mabeo baada ya kuwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Sir
Seretse Khama uliopo Gaborone.
Pamoja na hilo, pia alikutana na Katibu Mtendaji wa SADC, Dk.
Stergomena Tax na kufanya mazunguzo ya muda mfupi kabla ya kuanza kwa
vikao hivyo.
Dk. Stergomena alikuwa Katibu Mkuu wa iliyokuwa Wizara ya Afrika
Mashariki katika uongozi wa awamu ya nne chini ya Rais mstaafu Jakaya
Kikwete.
MSIMAMO WA MAGUFULI
Mara baada ya kuingia madarakani, Rais Magufuli alitangaza kufuta
safari holela za nje alizodai zimekuwa zikiligharimu taifa mabilioni ya
fedha.
Hatua hiyo aliitolea uamuzi Novemba 6, mwaka jana kwa kuagiza safari
zote muhimu ughaibuni ni lazima zipate ruhusa yake au ya Katibu Mkuu
Kiongozi Ikulu, lengo ikiwa ni kuokoa fedha zinazoweza kutumiwa kwa
shughuli nyingine za maendeleo kwa Taifa.
Akitolea mfano, alisema katika mwaka wa fedha wa 2013/2014 na
2014/2015, Taifa lilitumia zaidi ya Sh bilioni 356 kugharimia safari za
nje; jambo ambalo alisema hayuko tayari kulishuhudia.
Hadi sasa, Dk. Magufuli ameshaonyesha mfano kwa kuamuru watu wanne tu
kusafiri wakitokea ofisi ya ubalozi wa Tanzania nchini Uingereza kwenda
kumwakilisha katika mkutano wa wakuu wa nchi za Jumuiya ya Madola
uliofanyika visiwa vya Malta, badala ya watu zaidi ya 50 waliozoea
kusafiri katika safari kama hii ya rais.
Mbali na kudhibiti safari za nje, Rais Magufuli na Serikali yake pia
amedhibiti safari za ndani baada ya kuagiza kuwa vikao vyote vya kikazi
baina ya viongozi wa mikoa vifanywe kupitia teknolojia ya video (video
conference) na si kusafiri kutoka mkoa mmoja hadi mwingine au kukodi
ukumbi wa mikutano.
Desemba 17, mwaka jana Rais Magufuli aliagiza kusimamishwa kazi mara
moja kwa watumishi waandamizi wanne wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na
Rushwa (Takukuru), ambao walisafiri nje ya nchi licha ya kupiga
marufuku safari za nje kwa watumishi wa umma.
Watumishi hao ni Mary Mosha, Ekwabi Mujungu, Doreen Kapwani na Rukia Nikitas.
Agizo hilo la Rais Magufuli lilitolewa na Katibu Mkuu Kiongozi,
Balozi Ombeni Sefue wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.
Kutokana na uamuzi huo, Balozi Sefue aliwataka watumishi wengine wa
umma kutii agizo la Rais Magufuli na kuonya kuwa atakayekiuka
atachukuliwa hatua kali.
Tangu alipoapishwa kushika madaraka ya urais, Dk. Magufuli amesafiri
mara mbili, zote zikiwa ni safari za ndani ambapo ya kwanza alikwenda
mkoani Dodoma kuhutubia Bunge na ya pili ni ya Januari 12, mwaka huu
alipokwenda visiwani Zanzibar kwenye sherehe za miaka 52 ya Mapinduzi.
Chanzo Mtanzania
Monday, 18 January 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment