MBUNGE
wa Bariadi, Andrew Chenge na wabunge wawili wa Viti Maalumu, Dk Mary
Mwanjelwa na Najma Giga, wamechaguliwa kuwa Wenyeviti wa Bunge kwa
kipindi cha miaka miwili na nusu.
Uchaguzi
huo ulifanyika jana baada ya majina yao kupendekezwa na Kamati ya
Uongozi na kuyawasilisha bungeni kwa ajili ya uchaguzi.
Katika
uchaguzi huo, uliotanguliwa na wabunge hao kujieleza mbele ya wenzao na
kuulizwa maswali, sakata la Tegeta Escrow liliibuka baada ya Chenge
kujieleza.
“Katika
Bunge lililopita, chama chako na wabunge walikuwajibisha kwa kashfa ya
Escrow, je, siku ukiliongoza Bunge na hoja ikarudi ndani uko tayari
kuisimamia,” Mbunge wa Ndanda, Cecil Mwambe (Chadema) alimuuliza Chenge.
Akijibu
swali hilo, Chenge alisema Bunge linaongozwa na Kanuni na itakapokuja
mbele ya Bunge au kwenye Kamati, ikaonekana kuna maslahi ama inamhusu
mbunge, ni busara kuzingatia kanuni nafasi hiyo ikaachwa mwingine
aifanye shughuli za Bunge zisiwe na makandokando ya aina yoyote.
“Naona niishie hapo, ningeweza kusema zaidi ya hapo,”
alisema Chenge ambaye alikuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa zaidi ya
miaka 10 na pia Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti ya Bunge la 10 kabla ya
kujiuzulu kutokana na sakata la Tegeta Escrow.
Awali akijieleza Chenge ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo, alisema “napenda niliahidi Bunge na Watanzania kwa ujumla, kwamba hii ni dhamana nzito ya kumsaidia Spika na Naibu.
“Lakini
niwahakikishie nitatekeleza jukumu hilo kwa uadilifu, na kwa uaminifu
ili nitende haki inayoonekana na bila chuki, wala upendeleo wowote kwa
faida ya kujenga misingi bora ya Bunge hili lakini pia kwa kuwatumikia
Watanzania wote,” alisema.
Kuhusu
swali la Mbunge wa Nsimbo, Richard Mbogo (CCM) aliyetaka kufahamu ni
namna gani Chenge atadhibiti matumizi ya lugha ya kuudhi au kudhalilisha
wengine, Chenge alisema Kanuni za Bunge kama zilivyo sheria za nchi,
zinakata pande zote kama ilivyo msumeno.
Alisema ikithibitika kwamba mbunge amekiuka kanuni, kiti kitazingatia baada ya kupima kauli na maelezo aliyotoa bungeni.
“Baada ya kupima, tuhakikishe kwamba tunayosema humu bungeni yawe ya kweli, kweli tupu yasiwe ya uongo,” alisisitiza.
Mwanjelwa
ambaye ni Mbunge wa Viti Maalumu mkoani Mbeya, katika kujieleza mbele
ya wabunge, aliomba wamwamini na kuahidi kuwatumikia bila kujali itikadi
kwa faida ya wananchi wote.
Mwanjelwa alikiri kwamba Bunge hili lina changamoto nyingi, lakini atakachozingatia ni utaifa kwanza.
Najma,
ambaye kitaaluma ni Mwanasheria, aliahidi kuwa msaada mkubwa kwa Spika.
Aliahidi kuwa atahakikisha anaweka maslahi ya taifa mbele kwa kutoa
haki sawa kwa wabunge wote bila kujali vyama vyao.
Spika
wa Bunge, Job Ndugai alihoji kwa pamoja wanaoafiki mapendekezo ya
Kamati ya Uongozi, ndipo wabunge walio wengi wakaridhia Chenge,
Mwanjelwa na Najma wawe wenyeviti. Wenyeviti wa Bunge hufanya kazi
wakati ambao Spika au Naibu Spika wakiwa hawapo bungeni.
Katika
Bunge la 10, wenyeviti walikuwa Mussa Azzan Zungu, Kidawa Himid Saleh,
Lediana Mng’ong’o, Muhammed Seif Khatib, Sylvester Masele na Jenista
Mhagama.
Kwa
mujibu wa Ndugai, Kamati yau Uongozi imejiwekea utaratibu wa
kupendekeza majina na ilipokutana chini ya uenyekiti wa spika, iliamua
kuwapendekeza wabunge hao watatu ambao wote ni kutoka CCM.
Credit; Mpekuzi blog
0 comments:
Post a Comment