Saturday, 16 January 2016

Tagged Under:

UKAWA washinda umeya Ilala, Kinondoni

By: Unknown On: 22:10
  • Share The Gag

  • Meya mpya wa Manispaa ya KinondoniBoniface Jacob akiwa mbele ya bara hilo jipya la Manispaa hiyo mapema leo mara baada ya kushinda kwa nafasi ya Umeya Kinondoni.

    HATIMAYE uchaguzi wa Meya katika Manispaa ya Ilala na Kinondoni jijini Dar es Salaam umefanyika na wagombea kutoka vyama vya upinzani kuibuka washindi wa nafasi ya Umeya na Unaibu Meya.
    Aliyeibuka mshindi wa kiti cha Umeya Ilala ni Charles Kuyeko (Chadema) na Omary Kimbilamoto (CUF), alitangazwa kuwa Naibu Meya, wakati Umeya Kinondoni aliyeibuka mshindi wa kiti hicho ni Boniface Jacob, Diwani wa Kata ya Ubungo (Chadema) na Naibu Meya alishinda Diwani wa Kata ya Tandale Jumanne Amir (CUF).
    Katika uchaguzi huo Umeya Ilala, uchaguzi ulifanyika bila kuwepo wajumbe wa CCM baada ya kuususia na kuondoka ukumbini, hata hivyo akidi ya wajumbe ilikuwa 54, waliopiga kura walikuwa 31. Uchaguzi ulifanyika katika ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam na ulianza saa saba mchana.
    Katika uchaguzi wa Umeya Kinondoni mgombea wa Chadema Jacob alipata kura zote za upinzani 38 ambazo zilimpa ushindi dhidi ya mgombea mwenzake wa CCM, Benjamin Sitta aliyeibuka na kura 20.
    Baada ya ushindi huo, Jacob aliweka kaulimbiu ya kuunganisha “mabadiliko na kazi” na hii alisema ni kwa sababu Serikali Kuu inaongozwa na CCM na Halmashauri yake inaongozwa na upinzani.
    Katika uchaguzi huo, wajumbe hao walimchagua pia Diwani wa Kata ya Tandale kwa tiketi ya Chama cha Wananchi (CUF), Jumanne Amir aliyepata kura 38 na kumshinda mpinzani wake ambaye ni wa CCM, John Manyama aliyepata kura 19.
    Kukamilika kwa uchaguzi huo kunafanya halmashauri zote za Dar es Salaam kuwa na mameya wake. Abdallah Chaurembo, Diwani wa Charambe kupitia CCM ndiye Meya wa Temeke baada ya kuibuka na kura 32 dhidi ya Jummane Kambangwa mgombea kupitia CUF aliyepata kura 16.
    Wakati katika nafasi ya Unaibu Meya, Feisal Hassan aliibuka na ushindi kwa kura 31 dhidi ya Prosper Malufi wa Chadema aliyepata kura 18 .

    Chanzo HabariLeo.

    0 comments:

    Post a Comment