NA SHABANI MATUTU, DAR ES SALAAM
MBUNGE wa Ubungo, Saed Kubenea (Chadema) amesema anatarajia kufufua
hoja ya kujadiliwa upya kwa ripoti ya fedha zilizokwapuliwa za Tegeta
Escrow zaidi ya Sh bilioni 200.
Akizungumza na MTANZANIA jana jijini Dar es Salaam, alisema sababu za
kutaka mjadala huo kurejeshwa ni kutaka kujua iwapo fedha hizo ni za
umma au ni mali ya Kampuni ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL).
Sababu nyingine aliyoitaja Kubenea ni kutaka kuchukuliwa hatua kwa wahusika wa sakata hilo, ili iwe fundisho kwa watu wengine.
Mapendekezo ya Taarifa ya PAC
Iliyokuwa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) katika Bunge la
10, iliwasilisha bungeni mapendezo zaidi ya 10 likiwemo azimio namba
moja la kuitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na
Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI), kumkamata Mkurugenzi Mkuu wa
Kampuni ya Pan Africa Power Ltd (PAP) Harbinder Singh Sethi na
kumfikisha mahakamani kwa makosa ya utakatishaji wa fedha na ukwepaji
kodi.
Kamati inaelekeza Serikali kutumia sheria za nchi, ikiwamo sheria ya
Proceeds of Crime Act, kuhakikisha kuwa Singh Sethi anarejesha fedha
zote alizochota kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Kwa mujibu wa Taarifa ya CAG iliyothibitishwa na TAKUKURU, fedha hizo pia ziligawiwa kwa watu binafsi.
Aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya PAC, Zitto Kabwe, alisema kamati
yake ilijiridhisha kuwa fedha iliyotumika kulipia manunuzi hayo ni fedha
ambayo sehemu yake ni ya umma iliyochotwa bila huruma wala aibu, kutoka
Benki Kuu (BoT).
Historia ya Escrow
Akaunti hiyo ilifunguliwa na Serikali kwa pamoja kati ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Kampuni ya IPTL.
Fedha hizo zilizua mjadala mkubwa bungeni, ambapo Rais mstaafu Jakaya
Kikwete aliweka msimamo wa Serikali kupitia mkutano wa wazee wa Mkoa wa
Dar es Salaam, akisema kuwa fedha hizo hazikuwa za umma na hivyo
kuzidisha mjadala.
Chanzo Mtanzania
Sunday, 17 January 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment