Makamu Mwangalizi Mkuu wa Makanisa ya Baptist Tanzania, Mchungaji Michael Nhonya KANISA la Babtist Tanzania limeshauri Serikali kuchunguza utitiri wa madhehebu ya dini na wahubiri nchini, kama wana usajili na vibali halali. Makamu Mwangalizi Mkuu wa Makanisa ya Baptist Tanzania, Mchungaji Michael Nhonya, ameomba ichunguze ikiwa wote wanatenda shughuli zao kwa mujibu wa katiba na taratibu za nchi, ikiwemo kubaini wasio raia kama wana vibali vya kufanya utumishi nchini. Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini hapa, kiongozi huyo wa kanisa hilo lenye zaidi ya waumini milioni 1.5 nchini likiwa na makanisa zaidi ya 1,200, taasisi za elimu kikiwamo Chuo Kikuu cha Mount Meru Arusha, alikemea vitendo vya wageni kuingia nchini bila vibali. Alisema baadhi ya wahubiri, hawafuati utaratibu na sheria za nchi zinazowataka kuzingatia maadili ya utumishi wao bali wana malengo binafsi. Alisema wengi wa wahubiri nchini na duniani, wamejitokeza kuanzisha makanisa na huduma, si kwa lengo la kutangaza dini, bali kujipatia mkate wa kila siku kwa njia isiyo halali na kuchafua dini. Alisema wapo wengine huwatapeli watu mali zao na kutokomea kusikojulikana. “Ni vema serikali ikafanya ukaguzi, tena wa kina kwa kushirikiana na vyama ama muungano wa majukwaa ya dini nchini kama vile CCT (Jumuiya ya Kikristo Tanzania), TEC (Baraza la Maaskofu), PCT (Kanisa la Kipentekoste Tanzania),” alisisitiza mchungaji huyo. Aidha alisema iko haja pia kwa Idara ya Uhamiaji kufanya uchunguzi na kufuatilia watumishi hao ambao baadhi ni wahamiaji haramu wanaotumia mgongo wa kuhubiri dini, kuingia nchini kinyemela. Aliwataka Watanzania kutii sheria bila shuruti na kufichua watu wanaowafahamu kuwa ni wahamiaji haramu, sheria ichukue mkondo wake. Aliwataka waumini wa makanisa na Watanzania, kutorubuniwa na watu wanaotumia mwavuli wa dini kujipatia fedha, badala ya kuhubiri neno la Mungu. Created by Gazeti la Habarileo. |
Monday, 18 January 2016
Tagged Under:
‘Utitiri wa madhehebu uchunguzwe’
By:
Unknown
On: 22:50
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment