Mahakama Kuu ya Tanzania Kitengo cha Ardhi imeweka zuio la kubomoa nyumba zilizopo katika wilaya ya Kinondoni hasa zile ambazo wamiliki wake wameleta ombi lao mahakamani kuzuia kubomolea.
Akitoa
hukumu hiyo jana mbele ya walalamikaji, wakili wa Serikali, mawakili
wa walalamikaji na wananchi, Jaji wa Mahakama hiyo kuu ya Ardhi
Mhe.Panterine Kente alisema kuwa mahakama imezingatia maelezo toka pande
zote mbili kwa kuangalia madhara watakayopata wananchi kwa kutekelezwa
kwa zoezi hilo.
Jaji Panterine Kente aliongeza kuwa mahakama ya Ardhi haijaweka zuio la bomoa bomoa kwa Tanzania nzima
bali kwa wale tu walioleta maombi ya shauri la zuio la kubomolewa
nyumba zao na kusisitiza kuwa Serikali itaendelea na uwekaji wa alama
za x na ubomoaji wa nyumba zilizopo sehemu hatarishi na sehemu
zisizostahili.
“
Nakuagiza Wakili Abubakari Salim uniletee majina yote leo hii na sio
kesho ya waliofungua shauri la zuio la kutobomolewa nyumba zao ili
tuweze kuendelea na zoezi la ubomoaji” Alisema Jaji Kente
Akizungumza
baada ya kutolewa hukumu hiyo Wakili wa Serikali Manchare Henche
alisema wamepokea hukumu hiyo na wao wataendelea na majukumu yao ya
ubomoaji wa maeneo hatarishi kama Mahakama ilivyoeleza kuwa haijatoa
zuio la bomo bomoa kwa Tanzania nzima ila kwa wale tu walioleta shauri
la zuio.
“Tunaomba
walio maeneo ya mabondeni wahame kwani zoezi hili linaendelea na zoezi
la uwekaji wa alama za x litaendelea kama kawaida kwa maeneo mengine nje
ya haya yaliyowekewa zuio” Alisema Henche.
Aidha
akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutolewa hukumu hiyo Mbunge
wa Jimbo la Kinondoni Maulid Mtulia alisema kuwa uamuzi umeridhisha na
pia mahakama imetenda haki kwa wananchi wa kinondoni na wanashukuru kwa
kupata nafasi ya kusikilizwa kwa hoja zao.
Kesi hiyo namba 822 ilifunguliwa na wawakilishi nane wanaowawakilisha wananchi 674 ambao nyumba zao zilikuwa katika mpango wa kubomolewa chini ya sheria za mipango miji.
Baada
ya Mahakama kuu ya Tanzania kitengo cha Ardhi kutoa zuio la bomoa bomoa
kwa wakazi hao kesi ya msingi itatajwa tena Januari 11.
Mkuu wa Mkoa Wa Dar Atoa Tamko
Mkuu wa Mkoa Wa Dar Atoa Tamko
Wakati mahakama kuu ikisimamisha zoezi la bomoa bomoa, Mkuu wa Mkoa Dar es
Salaam, Said Meck Sadick amekanusha taarifa za upotoshaji
ambazo zimekuwa zikitolewa na viongozi wa kisiasa hususani wenyekiti wa
mitaa na baadhi ya wakazi wanaoishi maeneo hatarishi ya mabondeni juu
ya serikali kuvunja nyumba, ikizingatia kutotoa maeneo mbadala ya
kujenga makazi mapya ya kudumu.
Meck
sadick amesema mwaka 2011 yalipotokea mafuriko serikali iliwapatia
viwanja wakazi waliokuwa na nyumba katika maeneo hatarishi ya
mabondeni kwa Wilaya zote tatu za Mkoa Dar es Salaam katika eneo la
Mabwepande wilaya Kinondoni.
Kwa
mujibu mkuu wa mkoa jumla ya viwanja 1007 viligawiwa kwa wakazi hao wa
mabondeni na viwanja vitatu havikugawiwa kwa sababu viliangukia maeneo
yasiyofaa kwa makazi.
Aidha
sambamba na kupatiwa viwanja wakazi hao walipatiwa misaada ya
kibinadamu pamoja na vifaa vya kiujenzi ikiwemo mifuko ya saruji 100
mabati na mbao kila kaya na kuwawekea huduma muhimu za kijamii.
Amesema
wakazi hao wamediriki kuuza viwanja vyao kwa bei ya chini na kurudi
maeneo waliyokuwa wakiishi awali na wengine kuuza na kupangisha nyumba
zao walizojenga mabondeni licha ya Serikali kuwataka waondoke katika
maeneo hayo hatarishi.
Vile
vile amesema Serikali kwa kushirikiana na halmashauri zote nchini
imeanza na inaendelea na zoezi la bomoa bomoa kwa ajili ya kuwaondoa
wakazi wote wanaoishi maeneo hatarishi na wale waliovamia maeneo
yasiyostahili kujengwa.
Pia
amesema zoezi hili la bomoa bomoa litafanyika nchi nzima ambapo kwa
sasa limeanzia Mkoa Dar es Salaam na wakazi waliojenga katika maeneo
hatarishi wabomoe wenyewe na kuondosha baadhi ya vifaa vya ujenzi
ambavyo vitawasaidia kwenda kuendeleza makazi mapya katika viwanja
walivyopewa na serikali.
Amewataka
wananchi kuacha kuendelea kulalamika wakati wanafahamu kuwa wamevunja
sheria licha ya serikali kuwataka kuondoka kabla hawajapata madhara
ikiwemo kuvunjiwa nyumba zao.
Credit; Mpekuzi blog
0 comments:
Post a Comment