Saturday, 16 January 2016

Tagged Under:

Agizo la Serikali la Kukamatwa Waliomuozesha Binti wa Miaka 13

By: Unknown On: 00:24
  • Share The Gag

  • (PRESS RELEASE).
    WIZARA YAAGIZA KUKAMATAWA KWA WALIOMWOZESHA MTOTO WA MIAKA 13 WILAYA YA KISHAPU, MKOA WA SHINYANGA
    WIZARA ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imepokea kwa masikitiko makubwa na inataka hatua kali zichukuliwe dhidi ya wazazi wawili tofauti wanaotuhumiwa kuwaozesha watoto wao wa umri wa miaka 13 na kuwakatisha masomo katika mkoa wa Shinyanga na Dodoma.
    Imeelezwa kuwa, wakati mtoto mmoja mwanafunzi wa shule ya msingi Wishiteleja wilayani Kishapu mkoa wa Shinyanga ameozeshwa kwa nguvu kwa mahari ya ngombe 13 na kumkatisha masomo yake akiwa darasa la sita, mtoto mwingine wa mtaa wa Chikole, Kata ya Msalato Manispaa ya Dodoma anasemekana kuozeshwa kwa mahali ya shilingi 600,000. Kufuatia kuwepo kwa matukio haya mawili Wizara inataka vyombo vya dola kwa kushirikiana na Kamati za Ulinzi wa Mtoto katika mikoa yote kuhakikisha kuwa watuhumiwa wanachukuliwa hatua kali.
    Tukio la kuwaoza watoto katika umri mdogo siyo tu linakinzana na haki za msingi za mtoto bali pia linamkosesha mtoto haki ya kuendelezwa ikiwa ni pamoja na kuhatarisha uhai wake kwa kupatiwa majukumu ya mtu mzima katika umri mdogo.
    Wizara inawataka wazazi na walezi kubadilika na kuachana na tabia ya kuwaoza watoto wao katika umri mdogo maana vitendo hivyo ni vya kikatili. Jamii inatakiwa kutambua kuwa, vitendo vya kikatili kama hivyo vinapofanywa katika familia vinarudisha nyuma juhudi za Serikali za kupambana na ukatili maana kwa kiasi kikubwa familia inatakiwa kuwa mahala salama panapofaa watoto kuishi na kulindwa.
    Aidha, Wizara inakumbusha wazazi, walezi na wadau wengine kuwa, ndoa za utotoni ni kinyume na Sheria ya Mtoto (2009) na Mikataba ya Kimataifa kuhusu Haki na Ustawi wa Mtoto. NIwajibu wa kila mtu kuhakikisha kuwa watoto wanaishi katika usalama na kuhakikishiwa haki zao zote za msingi ikiwemo kulindwa, kuendelezwa, kuishi na kushirikishwa katika maisha ya kila siku ili kujenga Taifa linaloheshimu maslahi ya watoto.
    Erasto T. Ching’oro
    Kny: KATIBU MKUU
    MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZAZI NA WATOTO.
    Credit; Mpekuzi blog

    0 comments:

    Post a Comment