Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tamisemi, George Simbachawene
WAKURUGENZI watendaji wawili wa manispaa ya Mpanda mkoani Katavi na
ya Kigoma, wamesimamishwa kazi kwa tuhuma za kuridhia na kutekeleza
uamuzi ulioisababishia serikali hasara na upotevu wa fedha.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
(Tamisemi), George Simbachawene alitoa taarifa ya kusimamishwa kwao
kwenye mkutano na waandishi wa habari, jana. Taarifa ya kusimamishwa kwa
watendaji hao, ilitolewa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Ofisi ya Rais (Tamisemi), Rebecca Kwandu.
Alitaja waliosimamishwa ni Boniface Nyambele wa manispaa ya Kigoma
anayekabiliwa na tuhuma za uuzaji wa nyumba za halmashauri bila kufuata
sheria, kanuni na taratibu zilizopo, zinazomtaka awe na kibali cha
waziri mwenye dhamana.
Mwingine ni Mkurugenzi wa Manispaa ya Mpanda, Suleiman Mkanga
anayekabiliwa na tuhuma za ununuzi hewa wa gari la kusomba taka kwa Sh
milioni 92.75 na ubadhirifu wa fedha za ujenzi wa skimu ya umwagiliaji
ya Kakese, Sh milioni 294.
“Waziri ameagiza nafasi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigoma ikaimiwe
na Sultan Ndilowa ambaye ni Mkuu wa Idara ya Maji Manispaa ya Kigoma na
nafasi ya Mkurugenzi wa manispaa ya Mpanda ikaimiwe na Lauteri Kanoni
ambaye ni Katibu Tawala Msaidizi kutoka ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa
Katavi,” alisema Kwandu.
Pia Waziri Simbachawene aliwataka wakurugenzi watendaji wa mamlaka za
serikali za mitaa nchini kuwa makini katika kutekeleza majukumu yao kwa
kufuata sheria, kanuni na taratibu zilizopo.
Alisema serikali haitasita kuchukua hatua za kinidhamu kwa watumishi
wote, ambao watakiuka matakwa ya sheria, kanuni na taratibu na kutoweka
mbele maslahi ya umma.
Created by Gazeti la HabariLeo.
Monday, 18 January 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment