Azimio
La Baraza Kuu La Uongozi La Taifa Kuhusu Tangazo La Mwenyekiti Wa Tume
Ya Uchaguzi Ya Zanzibar La Kuitisha Uchaguzi Wa Marudio Zanzibar
Baraza
Kuu la Uongozi la Taifa la THE CIVIC UNITED FRONT (CUF – Chama Cha
Wananchi), likiwa ndiyo chombo cha juu cha maamuzi katika Chama baada ya
Mkutano Mkuu wa Taifa, limefanya kikao cha dharura leo, tarehe 28
Januari, 2016, katika Ofisi Kuu ya CUF, mjini Dar es Salaam.
Kikao
hicho kilikuwa na ajenda moja tu, ambayo ni kufanya maamuzi kuhusiana
na tangazo la Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar la kuitisha
uchaguzi wa marudio.
Baada
ya kujadili kwa kina tamko hilo la Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya
Zanzibar, Jecha Salum Jecha, la kuitisha uchaguzi wa marudio tarehe 20
Machi, 2016 na mwenendo mzima wa hali ya kisiasa Zanzibar tokea alipotoa
tamko lake batili la tarehe 28 Oktoba, 2015 kudai kwamba amefuta
uchaguzi mkuu wa Zanzibar wa tarehe 25 Oktoba, 2015 na matokeo yake, Baraza Kuu la Uongozi la Taifa limefikia maazimio yafuatayo:
1.
KWAMBA Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar umeshafanyika tarehe 25 Oktoba, 2015,
ambapo kwa upande wa uchaguzi wa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na
Madiwani ulikwisha kamilika na washindi wote kupewa shahada za
kuwathibitisha na kuwatambua kama washindi halali.
Kwa
upande wa uchaguzi wa Rais wa Zanzibar, matokeo yalikwisha bandikwa nje
ya vituo vya majumuisho vya majimbo yote 54. Kilichokuwa kinaendelea
baada ya hapo ni kuhakiki matokeo hayo kutoka majimboni na kazi hiyo
ilikwishakamilika kwa majimbo 40 na katika hayo, matokeo ya uchaguzi wa
Rais kwa majimbo 31 yalikwishatangazwa kabla ya Mwenyekiti wa Tume ya
Uchaguzi, Jecha Salum Jecha, kutangaza isivyo halali kwamba ameufuta
uchaguzi huo.
2. KWAMBA Chama Cha Wananchi (CUF) hakitoshiriki katika uchaguzi wa marudio uliopangwa kufanyika tarehe 20 Machi, 2016 kwa sababu uchaguzi huo si halali kwani uchaguzi halali ulishafanyika.
3.
KWAMBA linatoa wito kwa Wazanzibari wote wanaoipenda nchi yao na ambao
wanaamini katika utawala wa sheria, demokrasia na kuheshimu Katiba na
Sheria za nchi yetu kutoshiriki katika uchaguzi huo usio halali wa marudio.
4.
KWAMBA sababu kuu ya Baraza Kuu kufikia maamuzi haya ni kutokana na
matamko yote mawili ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, Jecha
Salum Jecha, kutokuwa halali na kwenda kinyume na Katiba ya Zanzibar na
Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar Nam. 11 ya 1984.
Hakuna
kifungu chochote cha Katiba ya Zanzibar au Sheria ya Uchaguzi ya
Zanzibar kinachotoa uwezo kwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar
na hata kwa Tume yenyewe kufuta uchaguzi au kuitisha uchaguzi wa
marudio.
5.
KWAMBA linazipongeza na limetiwa moyo sana na taasisi na jumuiya zote
za kimataifa na kikanda zikiwa ni pamoja na Jumuiya ya Madola (The
Commonwealth), Umoja wa Ulaya (European Union), Umoja wa Afrika (African
Union), Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) na
Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) pamoja na nchi za Marekani na
Uingereza kwa msimamo wao wa kuungana na Wazanzibari na kutetea haki yao
ya kidemokrasia na maamuzi halali waliyoyafanya katika uchaguzi mkuu wa
tarehe 25 Oktoba, 2015 na kutaka mchakato wa uchaguzi huo ukamilishwe
na matokeo yake kutangazwa.
6.
KWAMBA linazipongeza na kutiwa moyo pia na taasisi za hapa nchini
zikiwemo taasisi na jumuiya za kidini, taasisi za haki za binadamu,
vyombo huru vya habari, vyama vyengine vya siasa na Wazanzibari na
Watanzania wote wanaopenda amani na demokrasia kwa msimamo wao wa
kutetea maamuzi ya Wazanzibari waliyoyafanya katika uchaguzi mkuu wa
tarehe 25 Oktoba, 2015 na kuendelea kusisitiza haja ya kuheshimu na
kufuata Katiba na Sheria za nchi yetu na pia haja na umuhimu wa kutunza
amani ya nchi yetu kwa kutaka haki itendeke.
Baraza
Kuu linazihakikishia taasisi na jumuiya hizo zote na pia kuwahakikishia
Wazanzibari na Watanzania wote kwamba CUF itaendelea kusimama kidete
katika kulinda na kutetea Katiba na Sheria za nchi yetu na pia kutetea
maamuzi ya Wazanzibari waliyoyafanya tarehe 25 Oktoba, 2015.
7.
KWAMBA limesikitishwa na kushangazwa na kitendo cha Msajili wa Vyama
vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, kuandika barua na kutoa taarifa kwa
vyombo vya habari kutaka vyama vya siasa vishiriki uchaguzi wa marudio
uliopangwa kufanyika tarehe 20 Machi, 2016 bila ya kujali kwamba
uchaguzi huo ni haramu na unakiuka matakwa ya Katiba ya Zanzibar na
Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar Nam. 11 ya 1984.
Baraza
Kuu halikutarajia mtu mwenye hadhi ya Ujaji kufanya kazi ya kutumikia
maslahi ya watawala ambao wameamua kuvunja Katiba na Sheria za nchi yetu
na kukanyanga misingi ya haki na demokrasia huku akishindwa kukemea
uhuni mkubwa uliofanywa wa kubaka demokrasia na haki za watu.
8.
KWAMBA limesikitishwa na kitendo cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mheshimiwa Dk. John Pombe Magufuli, kukwepa dhamana na wajibu
wake kama Mkuu wa Nchi na Amiri Jeshi Mkuu kwa kuiacha njiani kazi
aliyoianza ya kutafuta ufumbuzi wa mkwamo wa uchaguzi Zanzibar.
Baraza
Kuu linamtaka Rais Magufuli kujitathmini na kujiuliza anajiweka vipi na
kutoa taswira gani mbele ya macho ya Watanzania na jumuiya ya kimataifa
kutokana na kutosimamia ahadi yake aliyoitoa mbele ya Watanzania wakati
akilizindua Bunge jipya kwamba atafanya kazi na vyama vya CUF na CCM
ili kuupatia ufumbuzi mkwamo huu.
9.
KWAMBA linalaani matumizi ya nguvu kubwa ya vyombo vya ulinzi na
usalama vya Jamhuri ya Muungano na Vikosi vya SMZ dhidi ya wananchi
wasio na hatia na ambao wamekuwa watulivu licha ya vitendo vingi vya
uchokozi wa makusudi na hata mashambulizi ya hujuma dhidi yao
yanayofanywa na makundi ya vijana wa CCM waliowekwa katika makambi
kadhaa kisiwani Unguja.
10.
KWAMBA linaitaka jumuiya ya kimataifa na hasa taasisi zinazosimamia
haki za binadamu na zinazopambana na makosa ya jinai kimataifa ikiwemo
Mwendesha Mashtaka wa Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai
(International Criminal Court – ICC) kufanya uchunguzi wa kauli na
matendo ya uhalifu, uvunjwaji mkubwa wa haki za binadamu na ubaguzi
ambao umekuwa ukifanywa dhidi ya wananchi wa Zanzibar na kuchukua hatua
dhidi ya watu walio nyuma ya maamuzi na utekelezaji wa matukio hayo.
11.
KWAMBA linawapongeza wananchi wa Zanzibar kwa kuonesha ukomavu wa hali
ya juu na kuwa watulivu licha ya machungu makubwa waliyoyapitia na
wanayoendelea kuyapitia tokea pale maamuzi yao yalipopinduliwa na CCM
kwa kumtumia Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, Jecha Salum
Jecha.
Baraza
Kuu linatoa wito kwa Wazanzibari wote kuungana pamoja chini ya chama
chao cha CUF walichokipa ridhaa halali kupitia uchaguzi mkuu wa tarehe
25 Oktoba, 2015 kutetea maamuzi yao waliyoyafanya kupitia sanduku la
kura kwa njia za amani.
Baraza
Kuu linawasisitiza tena Wazanzibari kwamba waendelee kutunza amani ya
nchi yetu na kutambua kwamba kutunza amani si udhaifu bali ni jambo
linaloipa nguvu jumuiya ya kimataifa kufuatilia haki za kidemokrasia za
wananchi wa Zanzibar.
12.
Baraza Kuu la Uongozi la Taifa linawatahadharisha CCM na watawala
wasiowajali na kuwaheshimu wananchi kwamba zama za utawala wa mabavu
usioheshimu Katiba na Sheria za nchi hazina nafasi tena katika dunia ya
leo. Baraza Kuu lina imani kwamba HAKI ITASHINDA.
LIMETOLEWA NA:
BARAZA KUU LA UONGOZI LA TAIFA
THE CIVIC UNITED FRONT
(CUF – Chama Cha Wananchi)
DAR ES SALAAM
28 JANUARI, 2016
Credit;Mpekuzi blog
0 comments:
Post a Comment