Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jji Mstaafu, Damian Lubuva akizungumza na wanahabari juu ya mambo yahusuyo tume hiyo.
TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imeamua kuwa viti vitatu vya wabunge
wanawake wa Viti Maalumu vilivyobaki uteuzi wake ufanyike mara baada ya
kukamilika kwa uchaguzi katika Jimbo la Kijitoupele Zanzibar.
Kikao cha NEC kilichokutana Januari 14 na 15, mwaka huu kilifikia
uamuzi huo kwa sababu ya kuahirishwa uchaguzi katika jimbo hilo. Kwa
mujibu wa mgawanyo wa viti maalumu uliofanywa na- Tume, kuna jumla ya
viti 113 ambavyo ni asilimia 40 ya wabunge wote 281 wa Bunge la Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania, ambapo Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilipata viti
64, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), viti 36 na Chama cha
Wananchi (CUF), viti 10.
Katika mgawanyo huo, vimebaki viti vitatu kukamilisha idadi ya viti
113 ambavyo havikugawanywa kutokana na kutokamilika kwa uchaguzi katika
majimbo nane ya Ulanga Mashariki, Arusha Mjini, Handeni Mjini, Ludewa,
Masasi Mjini, Lushoto, Lulindi na Kijitoupele.
Uchaguzi umefanyika katika majimbo hayo saba na Jimbo la Kijitoupele
kubaki, hali iliyosababisha kikao cha Tume kuamua kuwa uteuzi wa viti
hivyo vitatu ufanyike mara baada ya kukamilika kwa uchaguzi katika Jimbo
la Kijitoupele.
Kwa mujibu wa Ibara ya 78 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, 1977, ili chama cha siasa kilichoshiriki katika Uchaguzi Mkuu
kiweze kupata viti maalumu, ni lazima kiwe kimepata angalau asilimia
tano ya kura zote halali za wabunge.
Aidha, ili kuweza kukamilisha zoezi hili ni wazi kuwa, uchaguzi ni
lazima ukamilike katika majimbo yote. Kwa kuwa uchaguzi haujafanyika
katika Jimbo la Kijitoupele, Tume haitaweza kugawa viti vilivyobaki.
Hii inaelewa kuwa ni kutokana na ukweli kwamba endapo uteuzi
utafanyika, kura za Kijitoupele hazitatumika katika kupata viti maalumu
vilivyobaki, jambo ambalo litakuwa ni kinyume na matakwa ya Katiba. Kwa
mantiki hiyo viti hivyo vitatu vitagawanywa mara baada ya uchaguzi
kufanyika katika Jimbo la Kijitoupele.
Created by Gazeti la HabariLeo.
Saturday, 16 January 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment