Mkurugenzi wa upangaji na Utoaji mikopo wa bodi ya mikopo ya wanafunzi wa Elimu ya Juu, Onesimus Laizer akizungumza na waandishi wa
habari Dar es Salaam jana kuhusu utoaji wa mikopo ya elimu ya juu kwa
mwaka 2015/2016. Kushoto ni Meneja Habari, Elimu na mawasiliano wa bodi hiyo Omega Ngole.
BODI ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imetoa jumla ya
Sh bilioni 459 kama mikopo kwa elimu ya juu kwa wanafunzi 122,486,
wanaosoma katika vyuo mbalimbali ndani na nje ya nchi katika mwaka wa
masomo 2015/2016.
Hiyo ni idadi kubwa zaidi ya wanufaika na fedha kuwahi kutolewa tangu
kuanzishwa kwa Bodi hiyo mwaka 2005 na kwa ujumla, katika historia ya
utoaji wa mikopo nchini. Fedha hizo zimetolewa kati ya Novemba 2015 na
Januari 10, mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, Meneja Habari,
Elimu na Mawasiliano HESLB, Omega Ngole alisema katika mwaka uliopita
wa masomo 2014/2015, Serikali kupitia Bodi ilitoa jumla ya Sh bilioni
341 zilizowanufaisha wanafunzi 99,069.
Ngole alisema kati ya fedha zilizotolewa, Sh bilioni 199.7 zinakwenda
kwa wanafunzi 53,537 waliojiunga na masomo kwa mwaka wa kwanza Novemba
2015 katika vyuo mbalimbali na Sh bilioni 259.1 zinalipwa kwa wanafunzi
68,916 wanaoendelea na masomo, yaani mwaka wa pili, wa tatu na kuendelea
katika vyuo vya umma na binafsi.
Aliongeza kuwa kundi kubwa la wanafunzi waliopata mkopo ni wale
wanaosoma programu za kipaumbele, ambazo ni Udaktari wa binadamu,
Udaktari wa Meno, Udaktari wa Wanyama, Ufamasia na Uuguzi na Ualimu wa
masomo ya Sayansi na Hesabu na Uhandisi wa Umwagiliaji, wengine ni
yatima na walemavu.
Aidha, alisema pamoja na mafanikio ya kuwawezesha wanafunzi hao, bado
wanakabiliwa na changamoto kadhaa, ikiwemo kasi ndogo ya urejeshaji wa
mikopo kutoka kwa wanufaika, hali inayoathiri uwezo wa Bodi kuwakopesha
Watanzania wengi zaidi.
“Licha ya changamoto hizo, uwezo wa Bodi katika kukusanya madeni
umeongezeka kwa mwaka kutoka milioni 53.6 mwaka 2006/2007 wakati Bodi
inaanza kazi hadi kufikia bilioni 21 kwa mwaka 2014/2015 na kwa miezi
sita ya mwaka huu wa fedha Julai hadi Desemba 2015, Bodi imekusanya
jumla ya bilioni 12.1,” alisema Ngole.
Ngole alisema Bodi hiyo inatoa mwito kwa waajiri katika taasisi za
umma na binafsi nchini, kuhakikisha wanazingatia matakwa ya sheria
iliyoanzishwa na Bodi inayowataka kuwatambua waajiriwa wao, ambao ni
wanufaika wa mikopo kukata sehemu ya mishahara yao na kuwasilisha kwa
bodi kama marejesho.
Alisema sheria inawataka waajiri wawatambue waajiriwa walionufaika na
kuijulisha Bodi ndani ya siku 28 tangu wapate ajira na sheria hiyo, pia
inawataka waajiri baada ya Bodi kuthibitisha kuwa mwajiriwa ni
mnufaika, mwajiri anapaswa kuitaarifu Bodi ndani ya siku 30 za ajira
yake na kukata makato kutoka katika mshahara wa mwajiriwa na kuwasilisha
Bodi ndani ya siku 15 baada ya kila mwisho wa mwezi.
“Waajiri wote wanapaswa kutimiza matakwa hayo ya kisheria na kuwa
Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ameanza kukagua
taasisi za umma kama zinazingatia matakwa haya ya sheria na endapo
mwajri atakiuka anaweza kupata adhabu ya faini ya Sh milioni saba au
kifungo cha mwaka mmoja,” anaongeza Ngole.
Pia aliwataka wanafunzi walionufaika na mkopo, kuhakikisha
wanarejesha mikopo hiyo kwa wakati ili iwasaidie na wanafunzi wengine na
kuwataka wanafunzi waliopo vyuoni na walinufaika na mikopo watumie kwa
lengo lililokusudiwa.
Created by Gazeti la Habarileo.
Thursday, 14 January 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment