Wanasheria
nchini wamemtaka Rais John Magufuli ingilie kati sakata la Zanzibar kwa
sababu sintofahamu inayoendelea kutokea visiwani humo ni aibu ya
Tanzania mbele ya Jumuiya ya Kimataifa.
Wakizungumza
jana katika mdahalo ulioandaliwa na Chama cha Wanasheria cha Tanganyika
(TLS) kujadili changamoto za kisheria zilizojitokeza katika Uchaguzi
Mkuu uliofanyika nchini Oktoba 25 mwaka 2015, wanasheria hao walisema
Rais Magufuli anaweza kutumia nafasi yake kumaliza sintofahamu hiyo.
Aliyekuwa
Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Othman Masoud Othman alisema kufutwa kwa
uchaguzi wa Zanzibar kumekiuka Katiba na sheria mbalimbali za uchaguzi
zinazosimamia uchaguzi.
“Ingawa
haya yanatokea Zanzibar, lakini ni suala la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania. Tunamtaka Rais Magufuli katika kutumbua majipu alione na hili
la Zanzibar tunataka alipasue kabisa.”
Aliongeza kuwa, “kuendelea kutembea nalo linakuwa mzigo mkubwa, kwa hiyo tunamtaka kulipasua ili kutua hilo zigo.”
Othman alisema hakuna sheria yoyote inayompa mamlaka mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar kufuta uchaguzi.
Alisema
hata vifungu alivyovitumia Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salim Jecha wakati
anatangaza kufuta uchaguzi, vinazungumzia mambo mengine kabisa.
“Ni
vema Rais Shein (Ali Mohamed) akajiuzulu kwa sababu yeye ni sehemu ya
tatizo la Zanzibar. Hawezi kuendelea kugombea wakati yeye ndiye
aliyesababisha mkwamo huo wa kisiasa,” alisema mwanasheria huyo.
Wakili
Fatma Karume ambaye pia ni mtoto wa rais mstaafu wa Zanzibar, Amani
Abeid Karume alisema kuna haja ya kubadilisha kifungu cha 119 (10)
kinachotaja sifa za mwenyekiti wa Tume ya uchaguzi kwamba anatakiwa kuwa
jaji wa Mahakama Kuu au mtu yoyote mwenye kuheshimika.
“Ni
jambo la kushangaza kabisa, yaani Jecha anapewa uenyekiti wa Tume
wakati hajui mambo ya kisheria halafu makamu wake ndiyo jaji. Hapa kuna
tatizo na amewekwa hapo kwa ajili ya kulinda maslahi ya watu,” alidai wakili huyo.
Fatma
alisema hakushangazwa na kitendo cha wanasheria kushindwa kwenda
mahakamani kufungua kesi ya kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi kwa sababu
anajua hawana imani na mahakama. Alisema yule aliyemteua Jecha (Rais
Shein) ndiye aliyewateua pia majaji.
Mwakilishi
wa Chama cha Wananchi (CUF), Ismail Jussa alisema Jecha ni kada wa CCM,
hivyo hafai kuongoza Tume hiyo kwa sababu anaonyesha maslahi yake wazi
wazi kwa chama hicho.
“Katika
uchaguzi wa mwaka 2010, Jecha aligombea katika jimbo la Amani kupitia
CCM akashindwa. Shein akaona amteue kuwa mwenyekiti wa ZEC ili kulinda
maslahi yake.”
Jecha alitangaza kufuta uchaguzi huo wa rais, wawakilishi na madiwani visiwani humo akisema kanuni na taratibu zilikiukwa.
Uchaguzi huo kwa sasa umepangwa kufanyika Machi 20, mwaka huu.
Credit;Mpekuzi blog
0 comments:
Post a Comment