Na Ruth Mnkeni, Dar es Salaam
MBUNGE wa Mkuranga, Abdallah Ulega (CCM), amemwomba Waziri wa Ardhi
Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wiliam Lukuvi, kuhakikisha maeneo
yaliyochukuliwa na wawekezaji bila kuendelezwa yanarudishwa kwa wananchi
kwa mujibu wa sheria.
Hayo aliyasema jana, alipokuwa akizungumza na wananchi wa vijiji vya
Magodani na Lugwadu mkoani Pwani, ambapo alisema maeneo yaliyohodhiwa na
wawekezaji kwa muda mrefu bila kuendelezwa sasa ni muda mwafaka
kuyarejesha katika mikono ya wananchi.
Alisema pamoja na wawekezaji hao kupewa maeneo hayo lakini
wameshindwa kuyaendeleza kwa muda wa miaka 20 na kusema hatua hiyo ni
sawa na jipu linalosubiri kutumbuliwa.
Akizungumzia eneo la vijiji hivyo viwili lenye ekari 750 ambalo
limekaa kwa muda mrefu bila kuendelezwa aliwataka wananchi kuhakikisha
wanasimama imara na kwenda katika Serikali ya kijiji ili waanze
maandalizi ya kupata hati za maeneo yao.
“Fedha zitakazopatikana kuandikiwa hati ni vyema zikatumika kwenye
masuala ya kijamii ikiwemo ujenzi wa shule kwani eneo hili halina shule
iliyokaribu sote tu mashahidi, watoto wetu wanatembea kilomita sita hadi
saba kufuata shule.
“Pia hakuna zahanati katika eneo hili wanakijiji mnaifuata Kongowe tunataka kuondoa unyonge huu,” alisema Ulega.
Alisema sheria ndogondogo za vijiji lazima zifuatwe katika
kuhakikisha kwamba wanaendeleza maeneo hayo kwa maendeleo ya wilaya hiyo
na nchi kwa ujumla.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Taasisi ya kijamii ya TAMADA, Abeli
Mwakabenga, alisema ni viongozi wachache ndio wenye moyo wa kusaidia
kutetea maslahi ya wananchi lakini wengi wao wanatafuta masilahi yao
binafsi.
Chanzo Mtanzania.
Sunday, 17 January 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment