Wanawake wa kimasai wakiimba. Baadhi yao walichumbiwa wakiwa tumboni mwa mama zao, hali ambayo iliwanyima uhuru wa kuchagua mume wanayemtaka na hata kupata elimu. |
KUNA mila na desturi potofu katika jamii mbalimbali zinazosababisha ukatili wa kijinsia kwa wasichana katika wilaya ya Simanjiro. Jamii ya kimasai imekuwa ni miongoni mwa makabila yenye mila kandamizi kwa mtoto wa kike.
Katika kabila hilo, mtoto wa kike hana haki na hathaminiwi kama yule wa kiume ikiwa ni pamoja na suala zima la kupata elimu. Ofisa Elimu Shule za Msingi wilayani Simanjiro, Silvanus Tairo anasema, kitendo cha kutoandikisha watoto wote wa kike wenye umri wa kwenda shule ni ukatili wa kijinsia kwa kuwa kinawanyima fursa ya kujengewa uwezo wa kujitegemea.
Utamaduni wa wanaume kuhitaji kuoa wanawake waliokeketwa ni ukatili mwingine katika kabila la Wamasai. Inadaiwa kwamba, katika kabila hilo, ili msichana aolewe moja ya sifa ni lazima awe amekuzwa kimaumbile kwa maana ya sehemu za siri tangu akiwa mdogo kwa kuwekewa vidole au vijiti na mama au bibi yake. Inasemekana kwamba, maumbile hayo yakikuzwa yanamrahisishia mwanamume asipate shida atakapomwingilia mwanamke huyo.
“Anafanyiwa hivyo na mama au bibi yake ili akipelekwa kwa mume asipate tabu kwa kuwa mama anakuwa amefanya kazi yake,” anasema mmoja wa wakazi wa huko. Kutokana na utamaduni huo, kuna tatizo la utasa kwa Wamasai linalotokana na vitendo hivyo.
Kama wanaume wangesusa kuoa wanawake waliofanyiwa ukatili huo huenda hali ingebadilika. Tairo anasema, ni vigumu kuwafuatilia watoto wanaopata mimba za utotoni kama hawajaandikishwa shuleni. “Mfano mtoto ni mjamzito na walimu wanamripoti, tunataka maofisa, watendaji wa kijiji na kata wafuatilie yule mhalifu.
Mtoto anapofuatwa anasema alienda kuchota maji akakutana na morani kundi la wanaume au dereva wa lori akambaka. Katika hilo unakuta mzazi sio mkali. Je, wewe wa nje utafanya nini?” Anahoji.
Kwa mujibu wa Tairo, chanzo cha tatizo hilo ni mila, hamasa ndogo kwa elimu hasa kwa watoto wa kike na utajiri wanaoutarajia wazazi kwa kuwa na mtoto wa kike. Anasema, utekelezaji dhaifu wa sera na sheria ngazi ya kijiji kunachangia tatizo hilo liendelee.
Dk Ayubu John (jina si rasmi) anasema watoto wa kike wamekuwa wakifanyiwa ukatili mkubwa kwa kuwa bibi na mama zao hutafuta vibuyu vile vyenye mrija mwembamba kama mrija wa boga, na kuwaingizia kwenye sehemu zake siri.
“Kile kimrija anaingiza kwenye sehemu za siri za mtoto anazungusha taratibu kila siku na njia inaongezeka. Huanza kitendo hicho kwa mtoto taratibu tokea akiwa mdogo hivyo mtoto akifikia miaka 12 mpaka 16 anaweza kuolewa,” anasema daktari huyo.
Anasema hata hizo ndoa za utotoni ni tatizo kubwa kwa sababu watoto wengi wanashindwa kujifungua, pia wengi wanashindwa kuhimili majukumu ya familia na kwamba, hata kunyonyesha hufundishwa.
Mratibu Mtendaji wa Mtandao wa Kuelimisha Jamii kuhusu madhara ya ukeketaji pamoja na aina nyingine za unyanyasaji wa kijinsia (NAFGEN), Francis Selasini anasema, vitu vinavyoharibu elimu ya mtoto wa kike ni ule mtazamo wao kwamba tayari ana mchumba hivyo anakosa morali wa kupenda kusoma.
Daktari huyo anasema, kitendo cha kumlazimisha mtoto aolewe ili wazazi wapate ng’ombe wengi ni ukatili. “Utajiri wa baba mwenye boma ni pale mtoto wake anapokuwa amekeketwa na pia hajapata mimba akiwa nyumbani, wakati wa kumwozesha hupata mali nyingi zaidi,” anasema.
Anashauri Serikali kusaidia taasisi zinazopinga ukatili ili ziweze kufanya kazi vizuri. Kaimu Ofisa Elimu Sekondari, Mwalimu Kamota Kimweri anasema ni vigumu kupata takwimu za ndoa za utotoni kiwilaya.
Anasema mwaka 2013 waliwachukulia hatua wazazi 20 ambao watoto wao walikuwa hawana mahudhurio mazuri shuleni, baada ya hapo tatizo lilipungua. Kimweri anasema, chanzo cha ndoa za utotoni ni mila na mazoea ya Wamasai kuchumbia mimba hivyo mtoto akizaliwa wa kiume huwa rafiki wa mchumbiaji na akizaliwa wa kike huwa ni mke mtarajiwa.
Wamasai wanalipa mahari ya ng’ombe taratibu na ikifika muda mwafaka hudai mke wake. Kimweri anasema elimu ni muhimu kwa watu wanaokubalika katika jamii kama viongozi wa siasa, wa kidini na wa kimila ili wasaidie kubadili mila potofu.
Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA), kimefanya utafiti katika mikoa 14 ikiwemo mitano ya Zanzibar na kubaini aina tano za ukatili ukiwemo ubakaji, wanafunzi wa shule kulazimishwa kuolewa, ukeketaji, vipigo kwa wanawake pia watoto na wanawake kutelekezwa. Tamwa imefanya utafiti huo kutokana na kushamiri kwa vitendo hivyo, vingi haviripotiwi ama hayapewi vipaumbele inavyostahili katika vyombo vya habari.
Chanzo Gazeti la HabariLeo.
0 comments:
Post a Comment