Na Veronica Romwald, Dar es Salaam
WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy
Mwalimu, ametoa siku saba kwa viongozi walio chini yake kumwandikia
sababu za kitaalamu zitakazomshawishi asivunje Baraza la Wauguzi
Tanzania kwa kuwa limeshindwa kutimiza wajibu wake.
Waziri Ummy alitoa agizo hilo jana wakati alipokuwa akizungumza na
wauguzi na wakunga wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) ambapo
walifikisha malalamiko yao juu ya baraza hilo.
Wauguzi hao walilalamikia uongozi wa baraza hilo kuwa umeshindwa
kudhibiti utitiri wa vyuo vinavyotoa elimu ya uuguzi hata kwa watu ambao
hawajatimiza vigezo.
“Mmeniambia baraza hili limeshindwa kudhibiti utitiri wa vyuo na
kusimamia mitaala yake itoe elimu ya uuguzi hadi kwa watu ambao wamepata
daraja la sifuri.
“Ndiyo maana siku hizi watu hawana imani na wauguzi, wanaona heri
wakatibiwe na mabibi zetu huko ‘tiba asili’, najua NACTE walipitisha
mwongozo kwamba watoe elimu kwa ngazi ya cheti kwa miaka miwili, yaani
sawa na uhasibu, hili ni jambo ambalo sikubaliani nalo.
“Katika hili ikiwezekana hata Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na
Ufundi aandikiwe barua kwa sababu NACTE walipitisha na ipo chini yake,
mimi sikubaliani nalo… lazima fani ya uuguzi iheshimiwe,” alisema.
Aliwahakikishia wauguzi hao kuwa watasimamia suala la masilahi yao kuongezwa tofauti na ilivyo sasa.
Awali akisoma risala ya wauguzi, muuguzi Agnes Mtawa alisema wauguzi
hao wamekuwa wakifanya kazi ngumu kiasi cha asilimia 70 kuugua migongo.
“Tunahudumia idadi kubwa ya wagonjwa wakati mwingine wanazidi,
tunafanya kwa moyo tu, masilahi yetu bado ni madogo ikilinganishwa na
kada nyingine ikiwamo ya madaktari,” alisema.
Chanzo Mtanzania.
Thursday, 14 January 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment