Katibu Mkuu wa TAMONGSCO, Benjamin Nkonya.
WAMILIKI wa Shule na Vyuo Visivyo vya Serikali wameiomba Serikali
kufuta mfumo wa GPA unaotumiwa na Baraza la Mitihani (Necta) kupanga
madaraja ya mitihani ya sekondari, kwa maelezo kuwa haufai kwa kuwa
unahalalisha watahiniwa waliofeli waonekane wamefaulu.
Akizungumza jana Dar es Salaam kuhusu matokeo ya kidato cha pili
ambayo yametangazwa na Necta hivi karibuni, Katibu Mkuu wa Shirikisho la
Wamiliki wa Shule na Vyuo Binafsi (TAMONGSCO), Benjamin Nkonya alisema
matokeo hayo hayaeleweki kwani yameshuhudia baadhi ya wanafunzi
wanaoonekana kufanya vizuri chini ya mfumo wa GPA wakati katika mfumo wa
madaraja (division) wanaonekana wamefanya vibaya.
Kwa hali hiyo, Nkonya amemwomba Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia
na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako, kufuta mfumo huo hadi pale Necta
itakapokuwa tayari kujibu maswali kadhaa ya wadau wa elimu ambao wanaona
mfumo huo hauna tija katika kuboresha elimu.
Baadhi ya hoja ambazo zilihojiwa na Nkonya ni kwamba kulikuwa na
kasoro gani katika mfumo wa madaraja mpaka ukaja huo wa GPA na akataka
kujua ni nani alilalamikia mfumo wa division mpaka ukaondolewa? Alihoji
kabla ya mfumo huo kuletwa, ni wadau wapi walishirikishwa?
Alisema TAMONGSCO ilipata taarifa za kuwepo kwa mfumo huo wa GPA
kupitia vyombo vya habari na hawakushiriki katika ngazi yoyote ya
mijadala ya kisera kama sheria inavyoelekeza. Katibu Mkuu huyo wa
TAMONGSCO alihoji, “Je, alama za chini za gredi D, C,B na A zilibaki
kama zilivyokuwa wakati wa mfumo wa division au kuongeza gredi E na B+
ilikuwa mbinu ya kushusha alama za ufaulu na matumizi ya GPA
yakaanzishwa kwa lengo la kuficha ukweli kuwa viwango vimeshushwa kwa
kiasi kikubwa?
Nkonya pia alihoji mfumo huo una faida zipi na unasaidiaje katika
kuhakikisha kuwa wanafunzi wanaomaliza wanakuwa na ujuzi stahiki
utakaowawezesha kuhimili changamoto za soko la ajira na utandawazi?
“Kwa hali hii bado tunaishauri Serikali isitishe matumizi ya mfumo wa
GPA hadi pale hoja zetu zitakapopatiwa ufumbuzi,” alisema Nkonya.
Chanzo Gazeti La habariLeo.
Sunday, 17 January 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment