Na Elias Msuya, Dodoma
TANZANIA inakabiliwa na upungufu mkubwa wa watumishi wa afya, hali
inayochangia vifo kwa wagonjwa wengi kutokana na kukosa huduma.
Akiwasilisha mkakati wa kuboresha rasilimali watu katika sekta ya
afya nchini, kwa wabunge wa Kamati ya Huduma za Jamii na Maendeleo ya
Jamii, Meneja wa Mipango na Utetezi wa Sera kutoka Taasisi ya Benjamin
Mkapa, Manka Kway, alisema mwaka 2014-15 kulikuwa na mahitaji ya
madaktari wasaidizi 1,744, lakini waliopatikana ni 149 tu.
Alisema tathmini hiyo imefanyika wilaya 30 za mikoa saba ya Tanzania
ambayo ni Geita (Bukombe na Chato), Iringa (Kilolo, Mafinga, Iringa,
Mufindi), Kilimanjaro (Mwanga, Siha, Rombo, Hai, Moshi na Moshi
Manispaa).
Mikoa mingine ni Mtwara (Tandahimba, Masasi, Mtwara, Manispaa ya
Mtwara), Pwani (Kisarawe, Rufiji, Bagamoyo, Kibaha na Mji wa Kibaha),
Ruvuma (Mbinga, Namtumbo, Songea na Mji wa Songea), Shinyanga (Shinyanga
Manispaa na Halmashauri ya Shinyanga).
“Mahitaji ya madaktari wasaidizi kwa mwaka 2014-15 yalikuwa 1,744,
waliokuwapo ni 149 na waliopungua 1,595 sawa na asilimia 91,” alisema
Kway.
Mbali na madaktari wasaidizi, alisema kuna upungufu wa maofisa
wauguzi kwa asilimia 33, maofisa tabibu wasaidizi kwa asilimia 78,
maofisa tabibu kwa asilimia 26, wauguzi kwa asilimia 72, maofisa wauguzi
kwa asilimia 53 na wataalamu wa maabara kwa asilimia 37.
“Sekta ya afya inakabiliwa na uhaba wa rasilimali watu kwa asilimia
52 kupitia ikama ya mwaka 2014…zaidi ya asilimia 74 ya madaktari waliopo
wanafanya kazi maeneo ya mijini… wakati daktari mmoja anahudumia
wagonjwa 78,880 maeneo ya vijijini, daktari mmoja mijini anahudumia
wagonjwa 9,095. Shirika la Afya Duniani (WHO) linaelekeza uwiano wa
1:10,000,” alisema Kway.
Baadhi ya wabunge wakichangia maoni kuhusu tathmini hiyo, waliitaka
Serikali kurekebisha sera na sheria zake ili kuweka mazingira wezeshi
kwa watumishi wa afya kufanya kazi vijijini.
Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe (CCM), alisema sera ya afya
inayowezesha madaktari wa mijini kulipwa zaidi ya wanaofanya kazi
vijijini ni kikwazo kwao kwenda vijijini.
“Kwanini mhitimu wa shahada ya udaktari akiajiriwa Hospitali ya Taifa
Muhimbili au Mwananyamala analipwa mshahara mkubwa kuliko yule
anayefanya kazi Wilaya ya Nzega?” alihoji Bashe.
Alisema tatizo hata bajeti ya afya inapopitishwa bungeni huwa
haifikishwi yote, hivyo akawataka wabunge kusimamia bajeti hiyo itolewe
kikamilifu.
Naye Mbunge wa Urambo Mashariki, Margaret Sitta, alisema ili
watumishi wa afya waende vijijini ni vema wapewe mafao ya kuwa huko.
Chanzo Mtanzania
Sunday, 31 January 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment