Saturday, 16 January 2016

Tagged Under:

Bandari kwazidi kuwaka moto

By: Unknown On: 00:10
  • Share The Gag

  • Meli ikiwa na shehena katika Bandari ya Dar es Salaaam.

    SERIKALI imeendelea kuisafisha Bandari kwa kuwaondoa watendaji wa ngazi za juu na kuwahamishia wizarani ili kuongeza ufanisi katika utendaji, sambamba na kuongeza ukusanyaji wa mapato.
    Wakati hayo yakitokea Bandari, Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) amesimamishwa kazi huku Mhasibu Mkuu na Meneja Manunuzi wa taasisi hiyo wakihamishwa kwa tuhuma za kushindwa kusimamia ukusanyaji wa mapato katika taasisi hiyo.
    Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam kuhusu mabadiliko Bandarini, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa (pichani) alisema serikali ya awamu ya tano imedhamiria kuhakikisha inasimamia mapato ya serikali na taasisi zinafanya kazi kwa ufanisi mkubwa.
    Aliwataja watumishi walioondolewa Bandari kuwa ni Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu, Peter Gawile, Kaimu Mkurugenzi wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), Killian Challe na Kaimu Mkurugenzi wa Manunuzi, Mashaka Kishanda.
    Alisema watendaji hao wamerudishwa wizarani na itafanyika tathmini ili waangaliwe watapangiwa nafasi gani kwa kuwa inawezekana katika Bandari uwezo wao na ufanisi wao ulikuwa mdogo ila inawezekana maeneo mengine wakafanya vizuri zaidi.
    Aidha alisema imewateua watendaji wengine kushika nafasi hizo akiwemo Anthony Mbilinyi kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ambaye anakwenda Bandari kushika nafasi ya Gawile, Benito Kalinga ambaye alikuwa Ofisa Manunuzi Mkuu wa TCRA anayeenda Bandari kushika nafasi ya Kishanda na Abdulrahaman Bamba ambae alikuwa TEHAMA Uchukuzi anayeenda kushika nafasi ya Challe.
    “Tatizo kubwa lililokuwa linaonekana pale Bandari ni mfumo wa IT hivyo tumeamua hao waondoke… Tunaamini tukiwapa ushirikiano watendaji hawa wanaoingia watafanya vizuri zaidi na kufanikisha azma ya serikali ya kuongeza ukusanyaji wa mapato,” alisema.
    Katika hatua nyingine, Profesa Mbarawa amemsimamisha kazi Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Charles Chacha na kutaka kuhamishwa mara moja kwa Mhasibu Mkuu Alhaji Said Mteule na Meneja manunuzi wa taasisi hiyo, Said Kaswela kwa kushindwa kusimamia ukusanyaji wa mapato katika taasisi hiyo.
    Serikali pia imeona ifanye uchunguzi kuhusu ununuzi wa mtambo wa kufuatilia vyombo angani unaojulikana kama Automatic Data Surveillance-Broadcast (ADS-B) na mtambo wa kukusanya taarifa za usafiri wa anga (AMHS), ambayo imegharimu kiasi cha Euro milioni 1.5.
    Mbarawa alitoa agizo hilo jana akiwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango pamoja na watendaji wa TCAA katika ziara aliyoizungumzia kuwa ni ya kuangalia uendeshaji na ukusanyaji wa mapato unavyofanyika katika taasisi hiyo.
    Waziri huyo alisema kuna mambo yamejitokeza hivyo serikali imeona lazima ifanye uchunguzi kwenye ununuzi wa baadhi ya mitambo na pia imebaini kuna upotevu mkubwa wa ukusanyaji wa mapato ambao umechangiwa na uongozi wa taasisi kwa kutojipanga vizuri.
    “Wizara imeamua Chacha kuanzia leo (jana), hataendelea na nafasi hiyo tena badala yake atatafutwa mwingine. Mhasibu Mkuu wa taasisi hii atahamishwa na ofisa wa manunuzi wa taasisi hii. Iko haja ya kumpeleka sehemu nyingine ili tupate mtu safi na makini,” alisema Waziri huyo.
    Mitambo hiyo ilitakiwa kuanza kufanya kazi tangu Novemba mwaka jana, lakini mpaka sasa haijaanza kufanya kazi. “Bora ubaki na watu wawili kwenye kazi kuliko 10 ambao sio waadilifu,” alisema Mbarawa.
    Kwa upande wake Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mpango alisema kikubwa wanachopigania ni kuhakikisha serikali inakusanya mapato yote ya kodi na yasiyo ya kodi na kuongeza kuwa taasisi hiyo ina vyanzo ambavyo vingeweza kuingizia serikali fedha nyingi.
    “Mkaguzi Mkuu alikuja na kufanya utafiti lakini taarifa aliyoitoa haikufanyiwa kazi. Pia katika kudodosa inajulikana TCAA ina akaunti saba ambazo zinatia shaka,”alisema Waziri Mpango na kuagiza akaunti hizo kutokuguswa mpaka uchunguzi utakapofanyika.
    “Nimeagiza ili fedha za taasisi hii zibaki salama isitoke hata senti, pia ndani ya wiki mbili ufanyike ukaguzi kubaini upotevu wote wa fedha za umma uliofanyika,” alisema na kuitaka Mamlaka ya Usimamizi wa Manunuzi ya Umma (PPRA), ifanye uchunguzi wa mchakato mzima wa ununuzi wa mitambo hiyo miwili ya ADSB na AMHS, pamoja na kusisitiza kuwa watumishi waliosimamishwa watahamishwa mara moja.

    Chanzo HabariLeo.

    0 comments:

    Post a Comment