Rais wa shirikisho la soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi (kushoto) akizungumza na waandishi wa habari Dar es
Salaam jana kuhusu suala la Azam kwenda Zambia. Mwingine ni Mjumbe wa
Kamati ya Utendaji ya shirikisho hilo, Ayoub Nyenzi.
RAIS wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi ameziomba
radhi klabu 15 na wadau wa soka kutokana na sakata la ruhusa ya Azam FC
kwenda kucheza mechi za kirafiki Zambia na kuahirishwa baadhi ya michezo
yao ya ligi.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Malinzi alisema kuondoka kwa Azam FC,
wakati ligi ikiendelea ni jambo ambalo haliwezi kuvumilika endapo
tunahitaji kuwa na ligi bora ambayo ina ushindani.
“Ndugu zangu mtu mzima akivuliwa nguo huchutama na siyo kukimbia
akiwa uchi, hivyo na mimi kwa unyenyekevu naomba radhi timu zote 15 na
wadau wa soka na kuwahakikishia haki itatendeka,” alisema Malinzi.
Pia alisema kuondoka kwa Azam FC, hakutasababisha kupanga matokeo
badala yake watajiumiza wenyewe, kwani watalazimika kucheza mechi mbili
au tatu kwa wiki ili kwenda sambamba na wengine.
“Kuondoka kwa Azam FC kunawaathiri wenyewe, kwani watajikuta hawapati
mapumziko ya kutosha kwa vile watalazimika kucheza michezo miwili au
mitatu kwa wiki ili kuziba pengo na pia watakuwa kwenye maandalizi ya
Kombe la Shirikisho,” alisema Malinzi.
Hatua hii ya Malinzi imekuja baada ya klabu za Ligi Kuu kupinga hatua
ya kuwapa ruhusa Azam FC kwenda kucheza mechi za kirafiki na
kuahirishiwa baadhi ya michezo yao ya ligi.
Yanga ilikuwa ya kwanza kupinga ziara hiyo ya Azam na kutangaza leo ingeenda Afrika Kusini kwa ajili ya mashindano maalumu.
Juzi pia Simba nayo ilitangaza haitaendelea kucheza ligi hiyo kama hadi raundi ya 20 baadhi ya timu zitakuwa na mechi za viporo.
Mkuu wa Idara ya Habari ya Simba, Haji Manara alikaririwa na gazeti
hili akisema kitendo cha TFF kuahirisha mechi za baadhi ya timu ni
kutaka kubebana.
“Simba haitaki ligi iahirishwe na tutacheza, lakini katika kucheza
kwetu tumeiandikia TFF ili kutokuwa na mashaka mashaka itakapofika
raundi ya tano ya mzunguko wa pili au mzunguko wa 20 wa ligi, klabu zote
ziwe zimecheza mechi sawa. “Pia tumeiandikia TFF na Bodi ya Ligi kwamba
ligi iishe katika muda uliopangwa, labda kuwe na dharura za kibinadamu,
lakini sio za kwenda kucheza bonanza, hatutakubali, tutacheza ligi kwa
matarajio kwamba mechi ya 20 itakapofika ya ligi kila timu itakuwa
imecheza,” alisema Manara.
Azam ipo Zambia kwa mwaliko wa mechi mbalimbali, ambapo juzi ilicheza na Zesco ya huko na kufungana bao 1-1.
Chanzo Gazeti la HabariLeo.
Thursday, 28 January 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment