Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako.
WANAZUONI na wadau wa sekta ya elimu wamepongeza hatua ya Waziri wa
Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako kufuta
mfumo wa Wastani wa Alama (GPA), uliokuwa unatumiwa kupanga madaraja ya
mitihani.
Wameeleza kuwa GPA ni mfumo uliokuwa unaficha hali halisi ya ufaulu
wa mitihani katika shule za sekondari. Wamesema kurejeshwa kwa mfumo wa
Divisheni katika kukokotoa madaraja ya mitihani, kutaisaidia nchi
kutambua hali halisi ilivyo kwenye ufaulu wa mitihani na hata kama
kutakuwa na tatizo la ufaulu, Serikali itajipanga namna ya kushughulikia
kiini cha tatizo.
Wamedai mfumo wa GPA, uliletwa kisiasa na ulichangia kuwafanya
wanafunzi wanaohitimu sekondari kwenda vyuo vikuu, kutokuwa na ubora
kwani waliokuwa wamefeli na wale waliofaulu, wote walihesabiwa
wamefaulu.
Juzi Profesa Ndalichako alitangaza kufuta mfumo wa GPA kwa maelezo
kuwa mfumo huo haukupata baraka za Kamishna wa Elimu, kama ilivyokuwa
imeshauriwa na wizara. Pia alisema mfumo huo umeonesha watahiniwa
waliofaulu, kuonesha kiwango kidogo cha maarifa kuliko kiwango chao cha
ufaulu.
Mtaalamu wa Elimu, Profesa Justinian Galabawa alisema mfumo wa GPA,
ulikuwa unakiuka taratibu za upimaji na tathmini katika elimu, kwani
ulikuwa hautofautishi mtahiniwa aliyefaulu na aliyefeli, bali wote
walionekana wamefaulu.
Alisema jambo hilo halikuwa haki kwa sekta ya elimu, kwani sheria za
mtihani lazima zipime alichofundishwa mwanafunzi na watahiniwa hao
watofautishwe kwa ufaulu.
“Hebu angalia kuna ufaulu bora sana, ufaulu mzuri sana na vizuri,
hawa utawatofautishaje. Hata mwanafunzi ambaye amepata GPA ya 0.3 naye
anahesabiwa amefulu, kwa kweli haya yalikuwa ni maneno ya kisiasa na
hayakulenga kusaidia kuboresha elimu,” alisema.
Aliwashutumu wanasiasa kuwa hawakuitendea haki sekta ya elimu, kwani
waliwanyang’anya mamlaka Kamishna wa Elimu na Baraza la Mitihani na
kuagiza kuanza kutumika kwa mfumo wa GPA, bila hata kushirikisha wadau.
Mkurugenzi wa Hakielimu, John Kalaghe alisema mfumo wa GPA
ulianzishwa kisiasa na ndio maana Necta wameshindwa kuutetea. Alisema
nchi inapoamua kubadilisha mfumo wowote wa elimu hasa wa kukokotoa alama
za ufaulu wa mitihani, lazima kuwe na sababu za kisayansi.
Alisema wanasiasa walileta GPA kwa kuwa walibanwa katika kufikia
malengo kwenye mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) ambao ulitaka ufaulu
katika mwaka wa kwanza uwe asilimia 60, mwaka wa pili asilimia 70 na
mwaka wa tatu uwe asilimia 80. Alimpongeza Profesa Ndalichako kwa
kurudisha mfumo wa madaraja.
“Kama watoto wanafeli, acha tujionee, ni aibu yetu kama taifa, ili
tukae pamoja tutafute dawa na sio kuficha ukweli wa mambo,” alieleza.
Rais wa Chama cha Walimu (CWT), Gratian Mkoba alisema licha ya sekta
ya elimu kuwa na changamoto nyingi na kufanya ufaulu kushuka, sio vizuri
kuingiza siasa kuficha ukweli wa mambo kama ilivyofanyika kupitisha
GPA.
Katibu wa Katibu Mkuu wa Wamiliki na Mameneja wa Shule na Vyuo
binafsi Tanzania (Tamongsco), Benjamin Nkonya alisema Profesa Ndalichako
ameitendea haki nchi yake kwa kufuta mfumo wa GPA na aliomba waziri
huyo alindwe, kwa kile alichodai kuwa uamuzi wake unaweza kumfarakanisha
na wakubwa wengine.
Mwenyekiti wa Taifa wa Tamongsco, Mrinde Mnzava alisema maamuzi
aliyoyafanya Waziri ni bora na yatawasaidia wanafunzi na wazazi, ambao
wengi wao walikuwa hawaielewi na kusababisha kuwepo kwa maswali mengi
kutoka kwa wazazi na wanafunzi juu ya mfumo huo.
Chanzo Gazeti la HabariLeo.
Friday, 22 January 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment