Monday, 11 January 2016

Tagged Under:

TOLEO MAALUMU LA MAPINDUZI YA ZANZIBAR: Wanasiasa wameilaumu CUF kwa kususa sherehe

By: Unknown On: 23:02
  • Share The Gag

  • Baraza la mawaziri la kwanza baada ya Mapinduzi lililoweka dira na maana ya mapinduzi matukufu. Kususa kwa CUF ni kutothamini maana yake.

    LEO wananchi wa Zanzibar wanaadhimisha miaka 52 ya kumbukumbu ya Mapinduzi matukufu Zanzibar yaliyotokea mwaka 1964.
    Sherehe za Mapinduzi huadhimisha Januari 12 kila mwaka kwa lengo la kutunza historia 1964 na hasa kuwafahamisha vijana tulikotoka, tulipo na tunakokwenda. Kabla ya Mapinduzi Matukufu, Wazanzibar walitawaliwa na mataifa mbalimbali wakiwamo Waarabu, Wajerumani na Waingereza. Watu weusi waliwekwa katika daraja la chini ambapo walidharauliwa, kunyanyaswa na kukandamizwa wakiwa ndani ya nchi yao wenyewe. Baada ya kugombania uhuru kwa muda mrefu, Waingereza waliamua kutoa uhuru kwa Sultani.
    Kitendo hicho kilisababisha Zanzibar kukosa uhuru kamili kwa kuwa uongozi wa Kisultani uliendelea kuwaweka Waafrika katika daraja la chini. Mpango wa Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ulifanikiwa tarehe 12 Januari 1964 na kuung’oa utawala wa Kisutani kisha wananchi walio wengi wazalendo kushika hatamu ya kuongoza dola chini ya Uongozi wa Rais Abeid Amaan Karume.
    Mapinduzi ya Zanzibar ni tukio muhimu ambalo wananchi wanapaswa kulikumbuka na kujivunia kwani kuanzia mwaka 1964 Wazanzibari walikuwa huru katika nchi yao na kutambuliwa utu wao rasmi. Haki zote ambazo wananchi wazalendo walistahiki kuzipata ikiwemo elimu, matibabu na matumizi ya ardhi kwa kilimo na makaazi walinyimwa na utawala dhalimu wa Kisultani.
    Vyama vya siasa Zanzibar hivi karibuni vimelaani vikali uamuzi wa chama cha wananchi (CUF) kususia sherehe za miaka 52 ya Mapinduzi ya Zanzibar na kusema kimedhihirisha chama hicho kilivyo na kigugumizi kutambua Mapinduzi ya mwaka 1964. Akizungumza na waandishi wa habari Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi Zanzibar, Vuai Ali Vuai, anasema kwa muda mrefu chama cha wananchi na viongozi wake walisusia sherehe za Mapinduzi kabla ya kuja kwa mfumo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
    Kwa mfano alisema kwa muda mrefu viongozi wa chama cha (CUF) walikuwa wakipinga na kutaka neno SMZ likimaanisha Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar lisitumike kwa sababu tu ya kuchukizwa na Mapinduzi. “Mimi chama cha CUF kususia sherehe za miaka 52 ya Mapinduzi ya Zanzibar sio kitu kigeni hata kidogo kwa sababu viongozi wa chama hicho kwa muda mrefu walikuwa wakipata kigugumizi kuyatambua Mapinduzi hayo ambayo baadhi yao walidiriki kusema kwamba ni umwagaji wa damu,” alisema Vuai.
    Aliwataka wananchi kuchukua tahadhari na kufahamu dhamira ya chama hicho ambapo kama kitachukua dola basi upo uwezekano mkubwa wa kufuta sherehe hizo moja kwa moja. Aliyekuwa Mgombea wa nafasi ya urais wa Zanzibar kwa chama cha AFP katika uchaguzi uliofutwa Said Soud anasema sherehe za Mapinduzi kwa sasa ni za kitaifa na kamwe zisihusishwe na itikadi ya vyama vya siasa.
    Soud anasema sherehe hizo ni utambulisho wa wananchi wa Zanzibar walivyojikomboa na utawala wa Kisultani kwa hivyo zinatakiwa kuenziwa na kutunzwa na sio kubezwa kama walivyofanya viongozi wa (CUF). “Hawa viongozi wa (CUF) wanatakiwa kurudi darasani kupewa Elimu ya uraia ile iliyokuwa ikitolewa na Taasisi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam maarufu kwa jina la Redet kuhusu wajibu wa mwananchi na taifa lake na sio kubeza mafanikio ya uhuru,” anasema Soud.
    Aidha Soud anasema inasikitisha sana kuona chama cha (CUF) kinasusia sherehe za miaka 52 katika kipindi hiki ambapo viongozi wa chama hicho ni sehemu ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa,” anasema Soud. Juma Khatib aliyekuwa Mgombea wa nafasi ya urais kwa tiketi ya chama cha TADEA katika uchaguzi wa mwaka 2015 ,anasema kitendo kilichofanywa na CUF kususia sherehe za Mapinduzi kimeleta picha mbaya na inajaribu kupandikiza mbegu za chuki kwa kizazi kijacho.
    Anasema Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964 ndiyo ufahari wa wananchi wa Zanzibar kama wanavyofanya nchi nyingine ambapo hutumia fedha nyingi kusherehekea huku zikiwakumbusha vijana kufahamu wapo wapi na wanatoka wapi. “Mapinduzi ndiyo ufahari wa wananchi wa Zanzibar sasa kinapojitokeza chama cha siasa kikawashawishi wafuasi wake kususia kamwe haipendezi na ni kitendo cha usaliti mkubwa,” anasema Khatib.
    Khatib anasema kitendo cha kususia sherehe za miaka 52 ya Mapinduzi ya Zanzibar zinaweza kuzorotesha mazungumzo yanayoendelea ya kuleta suluhu ya kisiasa ambayo yanavishirikisha vyama vya siasa vya CCM na CUF. Kada wa Chama Cha Mapinduzi, Baraka Shamte anasema nchi zote duniani zinaweka na kutunza kumbukumbu siku ya uhuru wake kwa ajili ya faida ya vizazi vijavyo ili ziweze kujua hatua na juhudi zilizochukuliwa na waasisi wa Taifa.
    Kwa mfano anasema wapo viongozi wengi wa CUF hawayatambuwi Mapinduzi ya Zanzibar isipokuwa wanautambua Uhuru wa Desemba 1963 uliotolewa na Uingereza ambao haukuwa na lengo la kuwanufaisha wananchi wa Zanzibar isipokuwa walikuwa wakitaka kuendelea kudumu kwa utawala wa Kisultani. “Kauli ya viongozi wa CUF kususia sherehe za miaka 52 ya Mapinduzi ya Zanzibar sasa zinadhihirisha wazi wazi kwamba wenzetu wengine wanataka kuona Sultani anarudi kwa mlango wa nyuma,” alisema Shamte.
    Chama cha Wananchi (CUF) kimetangaza uamuzi wa kususia sherehe za miaka 52 ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa madai kwamba misingi na dhamira ya Mapinduzi hayo yamekiukwa kwa maoni na maamuzi ya wananchi kupuuzwa. Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi, anasema licha ya viongozi wa chama CUF kususia sherehe hizo, ufunguzi wa miradi ya maendeleo utaendelea kama ulivyopangwa.
    Kwa mfano Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Iddi ameshiriki katika kuweka jiwe la msingi katika ujenzi wa kituo cha kisasa cha tiba kwa vijana walioathirika na matumizi ya dawa za kulevya kiliopo Kidimni wilaya ya Kati Unguja. Balozi Seif anasema kituo hicho ambacho ni cha kwanza katika Afrika ya Mashariki kina lengo la kutoa tiba na kurekebisha tabia kwa vijana wanaotumia dawa za kulevya kwa kuwa athari zake ni kubwa kwa taifa.
    Aidha Balozi Iddi anasema kitendo cha viongozi wa chama cha wananchi CUF kususia sherehe za miaka 52 ya Mapinduzi kinatia wasiwasi kuhusu dhamira ya kweli ya chama hicho kuyatambua mapinduzi hayo ambayo ndiyo yaliyoleta utu wa binaadamu kuwa bora kwa wazalendo weusi. “Wazee wetu na waasisi walifanya Mapinduzi ya mwaka 1964 kwa lengo la kuondoa utawala dhalimu wa wachache na ili kuwapa uhuru wazalendo walio wengi waweze kunufaika na nchi yao asiyeyatambua Mapinduzi ni msaliti,” anasema Balozi Seif.
    CUF wamesusia sherehe za miaka 52 ya Mapinduzi ya Zanzibar huku kisingizio chao kikubwa ni kwamba malengo na dhamira ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964 yamekiukwa na kudharauliwa ikiwemo haki na maamuzi ya wananchi ya kuchagua.
    Kisingizio hicho kimekuja baada ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), kufuta matokeo ya uchaguzi mkuu iliofanyika Oktoba 25 mwaka jana ambapo mgombea wake Maalim Seif Sharif Hamad alijitangazia ushindi. Kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar ndiyo yenye uwezo wa kutoa na kutangaza matokeo ya uchaguzi mkuu ikiwemo wa kura za urais. Hata hivyo mgombea wa CUF alijitangazia ushindi kinyume na sheria.

    Created by Gazeti la HabariLeo.

    0 comments:

    Post a Comment