Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera, Nassoro Mnambila.
MKUU wa Shule ya Sekondari ya Bilele ya Mjini Bukoba, mkoani Kagera,
Siasa Phocus amevuliwa madaraka kwa madai ya kuendelea na msimamo wa
kutaka wazazi wenye watoto shuleni hapo, waendelee kutoa michango
kinyume na agizo la serikali.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera, Nassoro Mnambila aliliambia gazeti
hili jana mjini hapa kwamba mwalimu huyo alishapewa utaratibu wa
kuzingatia sera ya utoaji elimu msingi bure, lakini alikaidi.
“Kwa mamlaka niliyonayo, nachukua hatua hii kwa kumvua mamlaka mkuu
wa shule Bilele kutokana na kushindwa kutekeleza maelekezo yaliyotolewa
na serikali…,” alisema Mnambila.
Alisema mwalimu huyo aliendelea na msimamo wa kuwaambia baadhi ya
wazazi waliofika kuuliza utaratibu wa michango, kwamba hana taarifa na
miongozo ya serikali, akiwasisitiza kila mzazi kutimiza mahitaji
yaliyopo kwenye fomu ya mwanafunzi.
“Mwalimu huyo aliendelea kutoa fomu kwa kila mwanafunzi iliyoainisha
kila mahitaji kama ilivyokuwa hapo awali (miaka ya nyuma) huku akitaka
michango ya madawati, karatasi za kuchapia mitihani na mlolongo wa
gharama nyingine nyingi,”alisema Katibu Tawala.
Michango mingine ambayo wanafunzi wa sekondari wamekuwa wakitozwa
kila mwaka ni ya fyekeo, ndoo, jembe, uji, chakula cha mchana na uzio.
Katibu tawala alionya walimu wakuu na wakuu wa shule, kuzingatia na
kutekeleza sera ya utoaji wa elimu msingi bure, kama ilivyo kwenye
taratibu za miongozo iliyotolewa kwao katika idara ya elimu.
Fedha zafika mikoani
Wakati huo huo, mikoa mbalimbali imethibitisha kupokea fedha
zilizotolewa na Serikali kwa ajili ya utekelezaji wa mpango wa elimu
bure. Jumla ya Sh bilioni 18.77 zimetolewa na serikali kwa ajili ya
shule zote za umma nchini.
Miongoni mwa mikoa iliyothibitisha kwa waandishi wa habari kupokea
fedha zilizotolewa na serikali kwa ajili ya kutekeleza elimu msingi bila
malipo ni pamoja na Kagera, Morogo, Rukwa na Mwanza.
Ofisa Elimu wa Mkoa wa Kagera, Aloyce Kamamba alisema wamepatiwa
jumla ya Sh 810,157,000 ambazo zimeshaelekezwa kwenye akaunti za shule
zilizoko mkoani humo, ambapo za msingi ni 888 na sekondari 190. Kati ya
hizo, 17 ni sekondari za bweni. Kiasi hicho kimetolewa na serikali kwa
ajili ya kugharimia huduma mbalimbali ikiwemo chakula.
Mkoani Rukwa, Mkuu wa Mkoa, Magalula Said Magalula alisema wamepokea
Sh milioni 336 ambapo Sh 143,859,000 zimepelekwa kwenye shule za msingi
360 na kiasi kilichobaki, kimepelekwa shule 105 za sekondari. Kwa mujibu
wa Magalula, fedha hizo ni kwa ajili ya mwezi huu kwani kila mwezi
serikali itakuwa ikitoa fedha kwa ajili ya mpango huo.
Mkuu wa Shule ya Sekondari Kalangasa Manispaa ya Sumbawanga, Gabriel
Hokororo, alikiri shule yake kupokea Sh milioni 1.4 kwa ajili ya Januari
mwaka huu. Katika Mkoa wa Morogoro, Katibu Tawala Msaidizi wa mkoa huo
anayeshughulikia elimu, Wariambora Nkya, alithibitisha kupokea Sh
milioni 724.7 kwa ajili ya shule 846 za msingi na 179 za sekondari za
bweni na kutwa.
Mkoa mwingine uliothibitisha kupokea fedha hizo ni Mwanza wenye shule
za sekondari 197, ambazo zimepewa Sh 642,648,000 kwa ajili ya fidia ya
ada za kutwa na bweni na chakula kwa shule za bweni. Mkuu wa Mkoa wa
Mwanza, Magesa Mulongo alisema upande wa Shule za Msingi, zipo 850
ambazo zimepokea Sh milioni 356,728,000.
Alisema hadi Desemba 30 mwaka jana, shule zote zilishawekewa fedha kwenye akaunti zake.
Wahadharishwa matumizi
Walimu wakuu, wakuu wa shule, bodi wamesisitizwa juu ya matumizi
sahihi ya fedha hizo na wakati huo huo kuzingatia maelekezo ya serikali
ya kuhakikisha elimu msingi inatolewa bure.
Licha ya wakuu wa mikoa na idara ya elimu kuhadharisha juu ya hilo,
pia Wizara ya Fedha na Mipango hivi karibuni, ilionya wakuu wa shule za
msingi na Sekondari watakaotumia ovyo fedha hizo zilizotolewa na
serikali kutoa elimu bure, ikisema atakayebainika kuzitumia isivyo,
atashughulikiwa.
Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango iliwataka walimu katika
kuhakikisha fedha hizo zinatumika ipasavyo, waweke wazi fedha
walizopokea kutoka serikalini wananchi wafahamu alichopewa na matumizi
yake.
Bodi za shule zimepewa kazi ya kuhakikisha zinasimamia matumizi na
kutoa taarifa. Pia wakuu wa wilaya, mikoa na wakurugenzi wamepewa wajibu
wa kusimamia fedha hizo Sh bilioni 14.7, ambazo kati yake, Sh bilioni
tatu zimepelekwa katika vyombo vya usimamizi wa mitihani.
Chanzo Gazeti la HabariLeo.
Wednesday, 13 January 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment