Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein akihutubia wanachama wa CCM. |
MAKAMU Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein amesema chama
hicho kipo tayari kwa uchaguzi wa marudio Machi 20 kwa lengo la
kuhakikisha kinashika dola na waliochukua uamuzi wa kususa ni maamuzi
yao binafsi. Aidha, amesema Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Shariff Hamad ndiye aliyekiuka makubaliano ya mazungumzo ya mwafaka na kukimbilia katika vyombo vya habari. Akihutubia mamia ya wanachama wa CCM katika viwanja vya Makao Makuu ya CCM Kisiwandui mjini hapa kuzindua maadhimisho ya miaka 39 ya CCM, Dk Shein alisema maamuzi ya kurudiwa kwa Uchaguzi Mkuu yamefanywa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) ambayo ndiyo chombo halali kwa mujibu wa Katiba cha kushughulikia masuala yote ya uchaguzi nchini. Aliwataka wanachama na wafuasi wao kujipanga vizuri na kushiriki uchaguzi huo kikamilifu kwani kwa mujibu wa Katiba ya CCM ni kushinda uchaguzi zote zinazofanyika nchini ili kushika dola na kuwatumikia wananchi. “Hayo ndiyo maamuzi ya chama chetu tuliyokubaliana kushiriki Uchaguzi Mkuu wa marudio baada ya kufutwa kwa ule wa Oktoba 25 mwaka jana kwa hivyo wanachama na wafuasi jitayarisheni kushiriki kikamilifu kwa ajili ya kushika dola,” alisema Dk Shein. Dk Shein ambaye ni Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, alisema amesikitishwa na uamuzi pamoja na kauli za Katibu Mkuu wa CUF ambaye ni Makamu wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif za kujitoa katika mazungumzo yaliyokuwa yakifanyika, ambayo wote kwa jumla walikubaliana kwamba yawe siri kwa muda wote. Huku akishangiliwa na wafuasi na wanachama wa CCM, Dk Shein alisema ni Maalim Seif ndiye aliyemuandikia barua kukutana na kufanya mazungumzo kwa ajili ya mustakabali wa wananchi wa Zanzibar, ombi ambalo yeye alikubaliana nalo na kuliwasilisha kwa wenzake na hapo mazungumzo yalianza. Alifahamisha kwamba moja ya masharti ya mazungumzo yao ni kuheshimu na kutunza siri hadi muafaka utakapopatikana kwa kutoa taarifa ya pamoja kwa wananchi, lakini Dk Shein alisema kwa masikitiko makubwa Maalim alishindwa masharti hayo na kujitoa katika mazungumzo. “Nasikitika sana aliyejitoa katika mazungumzo ni mwenzangu Maalim Seif ambaye alikiuka makubaliano yetu na kuamua kwenda mbele ya vyombo vya habari kuzungumza....... mimi ni muungwana bwana naheshimu makubaliano na ndiyo maana nimekaa kimya,” alisema. Aliwataka wananchi na wafuasi wa CCM kujiandaa na uchaguzi wa Machi 20, akitamba kuwa wembe ni ule ule wa kuhakikisha wanashinda uchaguzi huo na kurudisha na kujenga imani ya wananchi walio wengi ambao anaamini kwamba CCM ndiyo chama kitakacholinda amani na utulivu. Aidha, alisema SMZ haipo tayari kuona kwamba watu wachache wanavuruga amani ya nchi kwa maslahi yao binafsi na uroho wa madaraka na kuwataka wananchi kushiriki kwa wingi katika uchaguzi wa marudio Machi 20. “Nasisitiza tena Zanzibar itabakia kuwa na amani katika kipindi cha uchaguzi wa marudio na atakayejaribu kuleta fujo, vyombo vya sheria vitachukua mkondo wake na hakuna sababu ya wananchi kuogopa kwenda kupiga kura kwani suala la uchaguzi wa marudio ni la kawaida ambalo linatokana na matakwa ya kisheria,” alisema. Mapema, Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana aliwataka wanachama na viongozi kwa ujumla kujipanga kuhakikisha kwamba CCM inashinda, akisema uchaguzi ni kujipanga na kuweka mikakati pamoja na mahesabu. Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinatimiza miaka 39 tangu kilipozaliwa Februari 5, 1977 baada ya kuvunjwa kwa vyama vya ASP na TANU na kuzaliwa kwa chama hicho kwa lengo la kuimarisha umoja na mshikamano na mapenzi ya wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kilele cha sherehe kitakuwa mjini Singida Jumamosi wiki hii. Chanzo Gazeti la habariLeo. |
0 comments:
Post a Comment