RAIS John Magufuli pamoja na mawaziri wake, wamehimizwa kutovunjika
moyo kwa kauli za kubeza kazi wanazofanya, badala yake wahakikishe
wanaendelea na kasi yao kudhihirisha wanachofanya si moto wa kifuu.
Hayo yalielezwa jana bungeni wakati wabunge wakichangia Hotuba ya
Rais Magufuli aliyoitoa Novemba mwaka jana wakati wa ufunguzi wa Bunge
la 11. Katika mjadala huo ambao wabunge wote waliendelea kumpongeza Rais
Magufuli kwa kazi anayofanya, Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe
(CCM) alishauri Serikali kuwasilisha bungeni sheria zote zinazokinzana
na kasi ya Rais, zifanyiwe mabadiliko ya haraka.
Mbunge wa Korogwe Mjini, Mary Chatanda (CCM) alimpongeza Rais
Magufuli kwa hatua ya kubana matumizi na kuchukua hatua kwa watumishi
wasiowajibika. Alisema kazi hiyo inatambuliwa pia na wananchi, kiasi
kwamba ikishafika kipindi cha taarifa ya habari, wamekuwa wakikimbilia
kuangalia televisheni kwa ajili ya kuona ni nini rais na mawaziri wake
wanasema.
Mbunge wa Mufindi Kusini, Mendard Kigola (CCM) alisema hotuba ya Rais
Magufuli, imekuwa mwongozo pia kwa wabunge kwa yale wanayopaswa
kuyasimamia majimboni mwao kutokana na kugusa mambo yote ambayo wananchi
wanahitaji.
Alisema kilichomfurahisha ni namna ambavyo Rais amemudu kutekeleza
ahadi, alizotoa wakati wa kampeni ndani ya kipindi kifupi cha miezi
mitatu. Alitoa mfano wa mpango wa elimu bure na kusema hakuna mtu ambaye
hasikii wala haoni kazi inayofanyika.
“Kufanya utekelezaji ndani ya miezi mitatu…kuna watu wengine wanasema
anatekeleza kidogo kidogo…tusimkatishe Rais tamaa, ameanza kufanya kazi
na anaonekana kwa Watanzania,” alisema Kigola.
Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe alimpongeza Rais kwa hotuba
aliyoitoa wakati wa ufunguzi wa Bunge akisema ndiye Rais ambaye
Watanzania walikuwa wakimhitaji kwa ajili ya mageuzi nchini huku
akisisitiza kwamba taifa liko kwenye dharura likihitaji uongozi wa aina
hii.
Bashe alisema wapo watu ambao wamekuwa wakisema Rais amekuwa akivunja
na kukanyaga sheria katika mambo ambayo amekuwa akifanya sasa. Mbunge
huyo alisema lipo tatizo la uwapo wa sheria ambazo baadhi ya watu
wamekuwa wakizitumia kuiibia nchi.
Alisema sheria za namna hiyo zimekuwa zikiwapa fursa watendaji wengi
kuiibia nchi yetu. Alishauri kwamba jambo linalopaswa kufanywa sasa ni
Ofisi ya Mwanasheria Mkuu na Waziri mwenye dhamana ya sheria kukaa na
kuleta bungeni sheria zote alizoziita za hovyo wazifute.
Bashe alisema utashi wa kisiasa wa Rais Magufuli umeonekana hivyo
wabunge wanapaswa kumsaidia kuhakikisha mambo anayotaka kuyatekeleza
ikiwemo ujenzi wa viwanda, yanafanikiwa. Alihimiza ufanyike uamuzi
sahihi wa uwekezaji katika viwanda kwa kuhakikisha vinavyoanzishwa
vinalenga kuinua wananchi walio wengi hususan wakulima.
Kuhusu ujenzi wa reli ya kisasa, alisema taarifa hizo zimekuwepo kwa
muda mrefu bila utekelezaji jambo aliloomba wabunge katika bajeti ijayo
wahakikishe fedha zinatengwa, vinginevyo wasikubali kuipitisha.
Wakati wabunge wakitoa kauli hizo dhidi ya wanaobeza utendaji wa
Rais, juzi katika mkutano na waandishi wa habari, Kambi ya Upinzani
kupitia kwa Kiongozi wake, Freeman Mbowe, walishutumu hatua ambazo
zimekuwa zikichukuliwa dhidi ya watumishi wazembe na wabadhirifu.
Mbowe alisema watendaji na watumishi serikalini wamekuwa wakifukuzwa
kazi kinyume cha taratibu, bila uchunguzi wala ushahidi. “Mawaziri
wanafukuza hovyo watu, sisi tunang’ang’ana kwamba wanatumbua majipu,”
alisema Mbowe.
Created by Gazeti la HabariLeo.
Thursday, 28 January 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment