Na Veronica Romwald, Dar es Salaam
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (Takukuru)
imetangaza inashughulikia kesi kubwa 36 zinazowahusisha watuhumiwa
wenye ushawishi na hadhi kubwa nchini.
Kutokana na hali hiyo, taasisi hiyo imesema tayari imeomba kibali
cha Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), ili watuhumiwa hao wanaohusisha na
ufisadi mkubwa wafikishwe mahakamani kwa mujibu wa sheria.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Kaimu
Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Valentino Mlowola, alisema tayari kuna
kesi nne ambazo zimekuwa zikizungumzwa na wananchi.
Mlowola alisema katu taasisi yake haipo kwa ajili ya kulinda wabadhirifu wa mali za umma.
Alisema kati ya hizo ipo Kampuni ya Mafuta ya Lake Oil ambayo
inaelezwa kuwa ilifanya udanganyifu na kukwepa kodi kwa kuuza kwenye
soko la ndani lita 17,461,111.58 za petroli
Kampuni hiyo inadaiwa ilidanganya kwamba ilikuwa imesafirisha
petroli hiyo kwenda Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kupitia
Zambia, na kuisababishia Serikali hasara ya takribani Sh bilioni 8.5.
“Takukuru imekamilisha uchunguzi wa shauri hili na mtuhumiwa na
washirika wake wamepewa miezi miwili kuzirejesha mikononi mwa umma fedha
zote Sh bilioni 8.5.
“Serikali ilipata hasara ya fedha hizo kutokana na ukwepaji kodi
huo na tunajiandaa kuwafikisha mahakamni endapo watashindwa kutekeleza,”
alisema Mlowola.
EGMA NA UTAKATISHAJI FEDHA
Kaimu Mkurugenzi huyo wa Takukuru, pia alizungumzia suala la hati
fungani hasa kuhusu suala la malipo ya dola milioni milioni sita (Sh
bilioni 12) zilizolipwa kwa Kampuni ya Enterprise Growth Market Advisors
(EGMA).
Alisema Takukuru imebaini fedha hizo zilitakatishwa na watumishi wa
umma wasio waaminifu kwa kushirikiana na baadhi kutoka sekta binafsi
wakati wakifahamu fedha hizo walizipata kwa njia haramu.
“Tupo kwenye hatua nzuri kukamilisha uchunguzi huu na watuhumiwa wote
bila kujali hadhi au nafasi ya mtu pamoja na taasisi zilizohusika,
tutawafikisha mahakamani kwa mujibu wa sheria,” alisema.
Tamko hilo la Takukuru limetolewa siku chache baada ya Serikali
kupitia Wizara ya Fedha na Mipango, kutangaza Januari 17 mwaka huu
kuichukuliwa hatua Benki ya Stanbic Tanzania na kutakiwa kulipa faini ya
Sh bilioni tatu kwa kuhusika kufanya malipo kwa kampuni ya EGMA kinyume
cha sheria.
Habari zinasema vigogo hao tayari wamekwisha kuhojiwa na vyombo vya
dola Desemba mwaka jana kutokana na tuhuma hizo za ufisadi.
Wakati huo, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, alisema
baada ya uchunguzi iligundulika ulikuwapo upungufu kwa benki ya Stanbic
Tanzania katika kufanya miamala iliyoihusisha EGMA na haikuweka
utaratibu wa madhubuti wa udhibiti kuhusiana wizi wa ndani.
“Sheria inaitaka Benki ya Stanbic kutoa utetezi katika kipindi cha
siku 20 ambacho kitaishia Januari 30 mwaka huu na endapo Benki Kuu
haitaridhika na utetezi, benki ya Stanbic italazimika kulipa faini
hiyo,” alisema Dk. Mpango ambaye kwenye mkutano huo alifuatana na Naibu
Gavana, Lila Mkila.
MWENENDO WA KESI
Mwenendo wa kesi kuhusu suala hilo iliyotolewa hukumu Uingereza,
Novemba 30 mwaka jana, unasema tangu mwaka 2011 Serikali ya Tanzania
ilifanya juhudi za kupata mkopo wa miradi ya miundombinu kupitia soko la
kimataifa la hati fungani bila mafanikio kutokana na kile kilichoelezwa
ni kukosa vigezo.
Mwenendo huo unasema benki za Standard na Stanbic kwa pamoja
zilichukua jukumu la kutafuta mkopo huo kwa Serikali ya Tanzania kupitia
waziri wa fedha wa wakati huo, Mustafa Mkulo.
“Pendekezo lilikuwa Standard na Stanbic ziwasilishe wazo la
kuiwezesha Serikali kupata mkopo, na lilikuwa liwasilishwe kwa waziri wa
fedha kwa sharti kwamba Standard na Stanbic kwa pamoja zipokee ada ya
asilimia 1.4 kwa kuandaa na kuwezesha mkopo huo.
“Standard na Stanbic zilisema kwamba wazo lao hilo lingeuzwa kama
mchakato binafsi kwa mujibu wa sheria na mwongozo wa usalama wa
Marekani,” unaeleza mwenendo huo wa kesi.
Katika barua pepe ya Februari 25, 2012, Kaimu Mkuu wa Masuala ya
Uwekezaji wa Stanbic, Shose Sinare, aliwafahamisha watu fulani ndani ya
Standard na Stanbic, akiwamo Mkuu wa Masuala ya Kimataifa ya Madeni ya
Masoko ya Mitaji wa Standard na Mkurugenzi Mtendaji wa Stanbic, kwamba
wazo lao limekubaliwa na waziri wa fedha.
Kwa herufi kubwa na maandishi manene, Sinare ambaye kwenye mwenendo
wote huo ametajwa kwa nafasi yake bila kugusia jina lake, alibainisha
kwamba benki ingepata asilimia 1.4 kama ada ya kuwezesha mpango huu kwa
Serikali ya Tanzania.
Mwenendo huo unasema kuwa Mei 2012, kabla ya wazo la mpango huo
kusainiwa, Waziri wa Fedha, Mkulo aliondolewa na nafasi yake
kuchukuliwa na waziri mwingine (Dk. William Mgimwa).
“Kuanzia Mei 2012 kuelekea mwishoni mwa mwaka 2012, Standard na
Stanbic zilijaribu kufufua mpango huo kupitia juhudi zilizofanywa na
Sinare na Mkurugenzi Mtendaji wa Stanbic (Bashir Awale), ambao
walikutana na maofisa wa Serikali nchini.
Mkuu wa Kimataifa wa Madeni ya Mitaji ya Masoko alikuwa akifahamishwa
hatua kwa hatua ya maendeleo hayo na Standard, pamoja na timu ya ndani
ya ushauri iliyohusika kuandaa nyaraka za mpango huo.
Juni 2012, Sinare aliwasilisha kwa ofisi ya Waziri wa Fedha nakala
ya mpango huo, ukiendelea kuonyesha Standard na Stanbic kwa pamoja kama
maneneja viongozi wa mpango huo, wakitarajia kupokea ada ya asilimia 1.4
ya sehemu ya mkopo huo.
Julai 2012, Stanbic ilimuajiri mtoto wa kiume wa waziri huyo mpya wa fedha.
Agosti 29, 2012, Sinare alimwandikia barua pepe Mkuu wa Masuala ya
Kimataifa ya Madeni ya Masoko ya Mitaji wa Standard, kwamba yeye na
Bashir wamefikia ‘mahali pazuri’ baada ya mkutano mzuri na Waziri wa
Fedha na timu yake, na kwamba kwa sasa wako katika mwelekeo mzuri wa
kusaini makubaliano ya mpango huo.
Mwenendo wa kesi hiyo unasema Sinare pia alimfahamisha Mkuu wa
Masuala ya Kimataifa ya Madeni ya Masoko ya Mitaji wa Standard kwamba
mkutano na Waziri wa Fedha ulithibitishwa ungefanyika Septemba 18.
KESI RAHCO
Akizungumzia Shirika Hodhi la Reli (RAHCO), Mlowola alisema jana
kuwa shauri hilo linahusu ukiukwaji wa sheria na taratibu za kuwapata
wazabuni kwenye ujenzi wa reli ya kisasa ya kimataifa (Standard Gauge),
mchakato unaosimamiwa na RAHCO.
Alisema baadhi ya watuhumiwa katika kesi hiyo wamekamatwa na
kuhojiwa akiwamo raia wa Kenya aliyekuwa mtu muhimu katika mchakato wa
kumpata mzabuni, Kanji Muhando.
“Mtakumbuka kuwa Rais Magufuli alitengua uteuzi wa aliyekuwa
Mkurugenzi Mkuu wa RAHCO, Benhadard Tito, kutokana na tuhuma mbalimbali
zilizokuwa zinamkabili, tunazo kesi tunazichunguza kuhusiana na TRL.
“…tupo kwenye hatua za mwisho kukamilisha uchunguzi huu na
tutawafikisha mahakamani wote watakaobainika kujihusha na vitendo vya
rushwa bila kujali hadhi zao wala nyadhifa walizonazo,” alisema Mlowola.
MABEHEWA TRL
Mlowola alisema shauri la TRL linahusu ukiukwaji wa Sheria za
Ununuzi wa Umma Namba 21 ya mwaka 2004 pamoja na kanuni zake kwenye
ununuzi wa mabehewa 25 ya kokoto kutoka katika Kampuni ya Hindusthan
Engineering and Industries Limited.
Alisema kutokana na uchunguzi wao walioufanya tayari wamekwisha
kumpelekea Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), ili kibali cha kuwafikisha
mahakamani watuhumiwa wote waliobainhika kujihusisha na vitendo vya
rushwa na ukiukwaji wa sheria, taratibu na kanuni za ununuzi wa umma.
Ujenzi wa reli hiyo mpya yenye urefu wa kilometa 2,561 ambayo itakuwa
na kiwango cha kisasa cha ‘Standard Gauge’ unatarajiwa utakuwa mradi
mkubwa kutekelezwa na Serikali ya Tanzania.
Aliyekuwa Waziri wa Uchukuzi wa Serikali ya awamu ya nne, Samuel
Sitta, aliwahi kusema kuwa reli hiyo mpya itakuwa tofauti na nyingine,
na yenye uwezo wa kimataifa kutokana na kuchukua mabehewa ya ghorofa
ambako itaanzia Dar es Salaam hadi Kigoma.
Treni hiyo itapita katika mikoa ya Tabora, Mwanza, Isaka hadi Rusumo,
Kaliua-Mpanda – Karema na Uvinza hadi Musongati nchini Burundi.
Pamoja na masuala mengine, reli hiyo itasaidia kukidhi mahitaji
makubwa ya ubebaji mizigo kwenda nchi jirani za DRC, Rwanda, Burundi na
Uganda lakini pia itasaidia usafirishaji wa wananchi kwenda mikoani kwa
wingi na kasi zaidi.
Ujenzi wa reli hiyo ya kisasa unatokana na uamuzi wa serikali baada
ya reli iliyopo ya kiwango cha ‘Meter Gauge’ kuwa na uwezo mdogo
ikizingatiwa kuwa ina uwezo wa kusafirisha tani milioni tano tu kwa
mwaka ambazo haziwezi kukabili mahitaji ya mizigo katika kanda hiyo
ambayo yatafikia tani milioni 30 ifikapo 2025.
Reli hiyo mpya ya kisasa itakapokamilika itasafirisha mizigo kutoka
bandari ya Dar es Salaam hadi Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC)
kwa muda wa saa 12 tu.
Uzinduzi wa reli hiyo ulifanyika Juni 30 mwaka jana na Rais mstaafu
wa awamu ya nne Jakaya Kikwete kwa kuweka jiwe la msingi eneo la Mpiji,
Mkoa wa Pwani ambako ndipo ujenzi utakapoanzia.
ONYO
Mlowola alisema jana kuwa Serikali imedhamiria kukabiliana na tatizo la rushwa na ufisadi kwa nia ya dhati.
Alisema wakati wa kampeni za uchaguzi na hata alipokuwa akizindua
Bunge la 11, Rais Dk. John Magufuli alionyesha nia ya dhati kutoka
moyoni mwake kwamba atalishughulikia tatizo la rushwa na ufisadi bila
kumuonea mtu huruma na aliwaomba Watanzania wamwombee kwa Mungu.
“Alisema atatumbua majipu. Majipu kama mnavyojua hayawezi kutumbuliwa
bila ya kuwapo kwa vidole, sasa sisi (Takukuru) ni vidole na
tutahakikisha tunashirikiana na Rais kulishughulikia kila jipu
litakalotumbuliwa.
“Ninajua watu walikuwa wakifanya kazi kwa mazoea, kama Rais
alivyosema kazi yake ni kutumbua majibu na mimi ni dole gumba na
watambue kwamba ‘The game is over’(mchezo umefikia tamati).
“Kwa sababu hatutasita kuchukua hatua kali za sheria kwa yeyote
atakayejiingiza kulihujumu Taifa. Wananchi wana kiu ya kupata maendeleo
na tunatambua kwamba bila kukusanya kodi ni vigumu kuwaletea maendeleo
hayo,” alisema Mlowola.
Mlowola aliwaonya maofisa maduhuli na watekelezaji wa jukumu la
kukusanya kodi kuhakikisha wanajiepusha na vitendo vya rushwa na ufisadi
kwa sababu Takukuru haitasita kuwashughulikia.
Chanzo Mtanzania.
Tuesday, 26 January 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment