Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
HOTUBA ya ufunguzi wa Bunge ya Rais John Magufuli, imeanza kujadiliwa
bungeni huku wachangiaji wengi wakieleza kuridhishwa na kasi yake ya
uongozi.
Wamesisitiza kwamba kama yako mambo ambayo hayaendi vizuri, wabunge wanapaswa kumjulisha, yafanyiwe kazi.
Pamoja na wabunge kuainisha maeneo kadhaa ambayo Serikali inapaswa
kuyafanyia kazi, wachangiaji wengi wamempongeza Magufuli na kuendelea
kusisitiza Watanzania wamwombee atimize malengo yake.
Michango ya wabunge hao, ambao baadhi waliweka bayana kuwa wananchi
wana imani naye kubwa kutokana na kuonesha kuwa analosema analitekeleza,
ilitolewa baada ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuwasilisha hoja
bungeni ya kujadili hotuba ya Rais, aliyoitoa Novemba 20 wakati wa
ufunguzi wa Bunge la 11.
Waziri Mkuu Majaliwa alisema hotuba ya rais imetoa mwelekeo na dira
ya serikali ya kutekeleza ahadi, alizotoa katika mikutano ya kampeni.
Alisema hotuba ya Rais imeeleza vipaumbele mbalimbali, vinavyotakiwa
kutekelezwa katika miaka mitano ijayo na kusisitiza kuwa serikali
imejipanga kikamilifu kuvitekeleza.
Aliomba wabunge wa vyama vyote, kutoa michango itakayosaidia serikali
katika utekelezaji wa mambo mbalimbali yaliyoainishwa, ambayo
utekelezaji wake umeshaanza kwa kasi kubwa.
“Bado serikali inahitaji sana michango na mawazo ya wabunge kwa ajili
ya kuboresha maeneo na yanahitaji usimamizi wa karibu na utekelezaji,”
alisema Waziri Mkuu.
Aliahidi kwamba michango yote ya wabunge itaheshimiwa na kufanyiwa
kazi. Wabunge wasifu Mbunge wa Mvomero, Suleiman Murad (CCM) alimpongeza
Rais Magufuli kwa juhudi zake za kupambana na mafisadi, kuimarisha
uchumi na kukusanya mapato.
Alisisitiza kuwa yako mambo mengine ambayo hayajui hivyo wabunge
ndiyo wanaopaswa kumjulisha yafanyiwe kazi. Murad alizungumzia tatizo la
ardhi kwa wakulima na wafugaji na kusema eneo hilo, linahitaji kazi ya
ziada.
Alishauri wizara zote zenye dhamana ya ardhi, mambo ya ndani ya nchi,
kilimo, mifugo na maliasili, zishirikiane kwa pamoja kukabili tatizo
hilo. Akizungumzia mikakati ya kuimarisha uchumi, alisema lipo suala la
baadhi ya wafanyabiashara kutokuwa waaminifu.
Aliomba wanaohusika na masuala ya bajeti na uchumi, kuwa macho na
watu wa namna hiyo, aliowataja kuwa wanacheza na Kamati ya Bajeti,
kuingiza mambo yao kwenye bajeti.
Akizungumzia vocha za pembejeo za kilimo, alisema lipo tatizo kubwa
vijijini kutokana na kuwapo watendaji serikalini wasio waaminifu ambao
ndiyo wamekuwa wakinufaika nazo.
Mvutano Zanzibar
Wakati suala la mvutano wa kisiasa lilikuwa miongoni mwa mambo ambayo
baadhi ya wabunge walilijadili kwa mtazamo tofauti wakiwemo waliotaka
Rais Magufuli aingilie kati aamuru mshindi wa urais atangazwe, mbunge
huyo wa Mvomero aliwakosoa, akisema suala hilo ni la kisheria.
Murad alisema, “Suala ni la kisheria, tuwatakie kila la heri wafanye
uchaguzi wao (Zanzibar) kwa amani. Rais hawezi kuingilia tena. Tume
(ZEC) imetangaza Machi 20 ni uchaguzi…Mizengwe ndiyo imesababisha hali
hii.” Aliendelea,
“Tumtake rais afanye makubwa, tusimchanganye, tumepata rais
asiyeogopa, mkweli, mwaminifu kwa taifa na ana ndoto nyingi. Tumpe
ushirikiano tuache maneno maneno, tumuache asonge mbele.”
Mbunge wa Temeke, Abdallah Mtolea (CUF) katika kuchangia kuhusu suala
la Zanzibar, alionesha imani kwa Rais Magufuli, akisema wananchi wana
imani naye kubwa kutokana na kuonesha kuwa analosema analitekeleza.
Mbunge huyo wa Temeke pia alizungumzia matatizo katika sekta ya afya
jijini Dar es Salaam na kusema licha ya hospitali za Temeke,
Mwananyamala na Amana, kupandishwa hadhi na kuwa za mkoa, zimeendelea
kuachwa zikihudumiwa na halmashauri huku zikikabiliwa na ukosefu wa
vitanda, dawa na maslahi ya watumishi.
Mbunge wa Mbinga Mjini, Sixtus Mapunda (CCM), alimpongeza Rais
Magufuli kwa hotuba aliyosema ni nzuri iliyosheheni weledi na
iliyoangalia kila sekta na maono mapana ya maslahi ya taifa. Aliomba
Watanzania waendelee kumuombea azma yake ya kuleta maendeleo ifanikiwe.
Chanzo Gazeti la HabariLeo.
Tuesday, 26 January 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment