Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa, Itikadi na Uenezi CCM, Nape Nnauye
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) imekitaka Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema), endapo kina nia ya dhati ya kupambana na ufisadi,
kijitangaze hadharani kumuunga mkono Rais John Magufuli katika vita hiyo
na si kuudanganya umma.
Pia imekitaka chama hicho ili kitekeleze vyema na kuibeba ajenda hiyo
ya ufisadi, kiwafukuze wanachama wake, wanaotuhumiwa kwa rushwa.
Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa, Itikadi na Uenezi CCM, Nape
Nnauye aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati akizungumza na waandishi
wa habari, ambapo alijibu hoja ya Mwanasheria wa Chadema, Tundu Lissu
aliyedai kuwa ajenda ya ufisadi inayotekelezwa kwa vitendo na Dk
Magufuli, ni ya chama122,4 hicho na ni ya kudumu.
Nape ambaye pia ni Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo,
alisema Lissu ameudanganya umma wa Watanzania kwa kuwa anafahamu fika
kuwa chama chake kilishajiengua na ajenda tangu kipindi cha Uchaguzi
Mkuu mwaka jana.
“Lissu anadai eti ajenda ya kupiga vita ufisadi ni ya chama chao,
kauli hii inashangaza kwa sababu kipindi cha kampeni Chadema ilijitenga
kabisa na ajenda ya ufisadi tena si tu kuizungumzia, walijitenga nayo
hata kwa vitendo,” alisisitiza Nape ambaye alikuwa mstari wa mbele ndani
ya chama chake kupinga mafisadi.
Alisema kama kweli chama hicho cha upinzani kina nia ya dhati ya
kuitekeleza ajenda hiyo ni vyema wakajitokeza hadharani na kumuunga
mkono Dk Magufuli, ambaye ameonesha si tu kwa kulizungumzia ajenda hiyo
ya kupambana na ufisadi, bali anaitekeleza kwa vitendo.
Dk Magufuli tangu ashike madaraka Novemba 5, mwaka huu, amekuwa kwa
vitendo, akipambana na ufisadi katika kile ambacho mwenyewe alikiita ni
kutumbua majipu, kwa kuwafukuza baada ya watendaji wa serikali na
kuwasimamisha kazi wengine kutokana na ubadhirifu.
Hatua yake hiyo imepongezwa na Watanzania wengi pamoja na jumuiya za
kimataifa kwa jinsi anavyoshughulikia suala la kupambana na ufisadi,
huku akisisitiza kuwa nia ya serikali yake ni kuwajali Watanzania
wanyonge ili wafaidi rasilimali za nchi yao.
Kuhusu kufukuzwa kwa Edward Lowassa kutoka CCM, Katibu wa Itikadi na
Uenezi wa CCM alisema Lissu amekuwa akiwadanganya Watanzania, kwa kuwa
Chadema inafahamu kuwa pindi walipompokea Lowassa, ndipo walipoamua
rasmi kuachana na ajenda ya kupambana na ufisadi.
“Kabla hawajamchukua, sisi tulijaribu kuwaambia kwa nini tulimkataa
Lowassa, hawakutusikiliza, sasa waache kudanganya wananchi. Lowassa
alipoenda kwenye chama chao ndiye aliyeua ajenda ya ufisadi,” alieleza
Nape.
Akijibu swali kwa nini CCM haikumfukuza Lowassa hadi alipoondoka
mwenyewe kama ilitambua kuwa ana kasoro kiutendaji, Nape alisema chama
hicho kilishaanza kuchukua hatua na ndio maana ilianzishwa operesheni ya
kuvua magamba.
“Huyu tulishaanza kushughulika naye, si lazima umfukuze mtu ndio
ujulikane umeshughulikia, tulimshughulikia hadi akaondoka mwenyewe,”
alieleza Nape.
Lowassa alijiuzulu nafasi ya Uwaziri Mkuu Februari 2008, baada ya
kuhusishwa na sakata la zabuni ya kampuni ya kufua umeme ya Richmond, na
mwaka jana alijitosa kuwania urais ndani ya CCM, lakini jina lake
lilikwama katika vikao vya uteuzi Julai.
Mwezi mmoja baadaye alikimbilia Chadema ambako aliteuliwa kuwa mgombea urais, lakini alishindwa na Dk Magufuli.
Hivi karibuni, Lissu alikaririwa na moja ya gazeti la kila siku (si
HabariLeo) akibainisha kuwa upinzani utaendeleza ajenda ya ufisadi kwa
kuwa ajenda za taifa ziko nyingi na Rais Magufuli, hataweza kuzitekeleza
mwenyewe.
Chanzo Gazeti la HabariLeo.
Thursday, 14 January 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment