Thursday, 28 January 2016

Tagged Under:

Wagombea wamkejeli Trump kwenye mdahalo

By: Unknown On: 22:10
  • Share The Gag
  • Image caption Trump hakujiunga na wagombea wenzake kwa mdahalo huo wa Fox News
    Wagombea urais wa chama cha Republican nchini Marekani wamemkejeli Donald Trump baada yake kususia mdahalo wa kupeperushwa runingani katika jimbo la Iowa.
    Aliamua kusususia mdahalo huo wa shirika la Fox News baada ya shirika hilo kukataa kumuondoa msimamizi wa mdahalo Megyn Kelly, ambaye Bw Trump amemtuhumu kwa kuwa na mapendeleo.
    Mfanyabiashara huyo tajiri badala yake aliandaa hafla ya kuchangisha pesa, za kuwasaidia wanajeshi wastaafu.
    Wapiga kura jimbo la Iowa watapiga kura Jumatatu kuchagua mgombea wao katika kila chama.
    Lakini kutokuwepo kwa Trump katika mdahalo huo mjini Des Moines kulijitokeza wazi, na wagombea saba wanaoshindana naye walihisi kutokuwepo kwake.
    Seneta wa Texas Ted Cruz aligusia hilo kwa ucheshi dakika za kwanza za mdahalo na kuwakejeli wapinzani wake.
    "Mimi ni wazimu na kila mtu katika jukwaa hili ni mjinga, mnene na asiyevutia, na Ben [Carson], wewe ni daktari mbaya wa upasuaji,” alisema, huku akijaribu kumuiga Trump, ambaye hakuwepo.
    Gavana wa zamani wa Florida Jeb Bush pia alimchokoza mfanyabiashara huyo tajiri kutoka New York, ambaye amekuwa akimshambulia Bw Bush midahalo ya awali.
    "Kwa kiasi fulani namkosa Donald Trump; alikuwa mwanasesere wa dubu kwangu,” alisema huku akitabasamu.
    Mengine makuu yaliyojitokeza:
    • Seneta wa Florida Marco Rubio alitetea msimamo wake wa awali wa kufunga misikiti ambayo inatumiwa kueneza itikadi kali
    • Pia aliahidi kuvunja mkataba wa nyuklia na Iran siku ya kwanza akiwa rais.
    • Seneta wa Texas Ted Cruz alisema: "Nitawawinda Isis [IS] popote walipo na kuwaangamiza "
    • Gavana wa New Jersey Chris Christie alisema hajui lolote kuhusu misongamano ya magari ambayo inadaiwa kusababishwa makusudi na wasaidizi wake
    • Gavana wa zamani wa Florida Jeb Bush amesema wanajeshi wa Marekani waliowahi kupigana vijani wanafaa kupata heshima zaidi kuliko wanavyopata sasa chini ya utawala wa Obama
    • Seneta wa Kentucky Paul alieleza wasiwasi kuhusu kuongezeka kwa mchango wa Marekani kijeshi nchini Syria
    Kwingineko mjini Des Moines wakati uo huo, Bw Trump ameongoza mkutano mkubwa wa kutoa heshima kwa wanajeshi wa Marekani waliostaafu
    “Unaponyanyaswa, lazima usimame na kutetea haki zako,” amesema, akirejelea mzozo wake na Fox News.
    Trump hakupendezwa na mtangazaji Megyn Kelly “Lazima tusimame kidete kama watu na kutetea taifa letu iwapo tunanyanyaswa.”
    Wengi katika mitandao ya kijamii walionekana kukubali kwamba mdahalo huo wa Fox News ulimkosa sana Trump.
    Lakini wengine walisema kukosekana kwake kulisaidia wagombea wengine, ambao hawajakuwa wakisikika kutokana na ‘ubabe’ wa Trump, kusikika.
    Uchaguzi wa Iowa Jumatatu ijayo utakwua mtihani wa kwanza kamili kwa wagombea, na mwanzo tu wa msururu wa uchaguzi wa kuwachagua wajumbe wa vyama vya Republican na Democrats.
    Kinyume na uchaguzi wa kawaida wa wagombea, ambapo kura za siri hupigwa, uchaguzi wa Iowa huwa ni mkutano wa wagombea wa vyama waliosajiliwa ambao kwanza huwajadili wagombea na kisha kupiga kura zao.


    Chanzo BBC Swahili.

    0 comments:

    Post a Comment