Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema msimamo wa Serikali wa
usitishwaji wa matangazo ya moja kwa moja kutoka bungeni ya Shirika la
Utangazaji la Taifa (TBC) utabaki palepale.
“Msimamo wa TBC ni msimamo wa Serikali,” amesema Majaliwa jana wakati
akijibu swali la papo kwa hapo la Kiongozi wa Upinzani Bungeni ambaye
ni Mbunge wa Hai, Freeman Mbowe (Chadema) aliyetaka kufahamu kauli ya
serikali juu ya TBC kusitisha matangazo kwani ni haki ya wananchi
kikatiba.
Waziri Mkuu alisema suala hilo lilishatolewa ufafanuzi na Waziri wa
Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye na kilichofanywa na TBC
ni kubadilisha ratiba. “Huo ni mpango wa ndani wa taasisi yenyewe
kujiendesha, msimamo wa TBC ni msimamo wa serikali,” alieleza.
Juzi, Nape alitoa kauli ya serikali kuhusu TBC na kubainisha kuwa,
kabla ya kuanza kurusha matangazo ya moja kwa moja TBC wakati huo
Televisheni ya Taifa ilikuwa inarekodi matukio yote ya Bunge na kurusha
usiku katika vipindi maalumu vilivyojulikana kama Bungeni Leo kwa maana
ya yaliyojiri ndani ya Bunge kwa siku husika.
Alisema baada ya kuanza kwa kurushwa kwa matangazo hayo ya Bunge moja
kwa moja mwaka 2005, TBC imekuwa ikilazimika kulipia gharama ya Sh
bilioni 4.2 kwa mwaka ili kuwezesha urushwaji huo. Pia imekuwa
ikigharimia kwa sehemu kubwa matangazo hayo kwa kutumia mapato yake
yanayotokana na matangazo madogo ya biashara.
Akitetea hoja juzi usiku Nape alisema kinachofanyika sasa cha
kurekodi na kisha kurusha baadaye matangazo ya Bunge, si jambo geni
kwani uzoefu unaonesha kutoka mabunge mengine mengi Afrika na baadhi ya
nchi zilizoendelea, hazirushi matangazo yao moja kwa moja.
“Kilichofanyika ni kubadilisha muda,” alisema na kusisitiza matangazo
ya moja kwa moja yataendelea kurushwa tangu saa 3:00 asubuhi mpaka saa 5
isipokuwa kama kutakuwa na jambo kubwa na baada ya hapo, shughuli
zitakazoendelea bungeni zitarekodiwa na kuoneshwa kwenye kipindi cha Leo
katika Bunge.
Nape alisema uzoefu unaonesha mabunge mengine mengi hayafanyi
utaratibu huu wa kurusha matangazo ya moja kwa moja siku nzima kama
ilivyokuwa ikifanyika nchini. Alitoa mfano wa mabunge hayo ni pamoja na
ya nchi za Jumuiya ya Madola.
Kwa mujibu wa Nape, Australia wanarusha matangazo ya bunge kwa muda
wa saa nne kwa wiki; Canada wanarusha kupitia cable. Kwa upande wa
Uingereza, Nape alisema wana kipindi kinaitwa Today in Parliament
ambacho alisema kinaoneshwa kwa saa moja na wakati mwingine wanaonesha
maswali ya moja kwa moja kwa Waziri Mkuu.
Waziri Nape alisema uamuzi uliofikiwa, umetokana na TBC yenyewe ambao
waliiandikia serikali barua wakieleza tatizo la gharama kubwa
wanazoingia katika kurusha matangazo ya moja kwa moja. “Haya ndiyo
mazingira tuliyofikia baada ya kushauriana na TBC. Huu ulikuwa uamuzi wa
ndani,” alisema.
Chanzo Gazeti la HabariLeo.
Thursday, 28 January 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment