Wachezaji wa Simba kutoka kushoto Hamis Kiiza, Peter Mwalyanzi na Ibrahim Ajib wakishangilia bao pekee jana
lililofungwa na Kiiza katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kati ya
timu hiyo na Mtibwa Sugar Uwanja wa Taifa, Dares salaam.
MSHAMBULIAJI Hamis Kiiza jana aliwapa furaha mashabiki wa Simba na
kumpa raha Kaimu Kocha Mkuu wa timu hiyo, Jackson Mayanja baada ya
kufunga bao pekee katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya
Mtibwa Sugar.
Mchezo huo uliofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam umekuja wiki
moja baada ya Simba kufungwa pia bao 1-0 na Mtibwa katika mchezo wa Nusu
Fainali ya Kombe la Mapinduzi Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
Matokeo hayo ya mchezo wa Zanzibar yalileta upepo mbaya Simba ambao
ulisababisha Kocha Mkuu wa timu hiyo Dylan Kerr, kuondolewa na majukumu
kukabidhiwa Mayanja. Kutokana na ushindi huo Simba imefikisha pointi 30
kwa michezo 14 na kuendelea kujinafasi nafasi ya tatu , nyuma ya
mabingwa watetezi, Yanga wenye pointi 32 kwa mechi 13 na vinara, Azam
wenye pointi 35.
Azam ilitarajiwa kucheza na African Sports baadaye jana. Yanga
yenyewe itashuka uwanjani leo kucheza na Ndanda Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam mchezo unaotarajiwa kuwa wa vuta nikuvute.
Kwa kipigo hicho, Mtibwa Sugar imebaki nafasi ya nne ikiwa na pointi
27 baada ya kucheza mechi 14 kama Simba. Katika mchezo wa jana, bao hilo
la Simba lilifungwa dakika ya nne na Hamisi Kiiza kwa kichwa akimalizia
krosi ya Ibrahim Ajib.
Dakika ya 16 Kiiza akiwa katika nafasi nzuri ya kufunga, alishindwa
kulenga lango baada ya shuti lake kupaa juu ya lango. Timu hizo
ziliendelea kushambuliana kwa zamu, huku washambuliaji wa timu zote
wakishikwa na kigugumizi cha miguu kila walipokaribia eneo la hatari.
Mabadiliko iliyofanya Simba dakika ya 31 kumpumzisha Peter Mwalyanzi
na kumuingiza Said Ndemla yalichangamsha kwa kiasi kikubwa sehemu ya
kiungo ya timu hiyo. Dakika ya 47, kiungo wa Mtibwa Sugar aliye katika
kiwango cha juu kwa sasa, Shiza Kichua nusura aisawazishie bao timu
yake, lakini mpira aliopiga ulitoka nje kidogo ya lango.
Kipindi cha pili Mtibwa Sugar walitawala kiasi kikubwa sehemu ya
kiungo, lakini umaliziaji ulikuwa butu. Mtibwa watajutia zaidi nafasi ya
dakika ya 4 wakati shuti la beki wa kushoto Issa Rashid ‘Baba Ubaya’
lilipogonga mwamba na kuokolewa na mabeki.
Simba; Vincent Angban, Emery Nimubona, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’,
Hassan Isihaka, Juuko Murshid, Justice Majabvi, Mwinyi Kazimoto, Jonas
Mkude, Ibrahim Ajib/Danny Lyanga, Hamisi Kiiza/Awadh Juma na Peter
Mwalyanzi/Said Ndemla. Mtibwa Sugar; Said Mohamed, Ally Shomary, Issa
Rashid ‘Baba Ubaya’, Salim Mbonde, Henry Joseph, Shaaban Nditi, Shiza
Kichuya, Muzamil Yassin, Hussein Javu/Jaffar Kibaya, Ibrahim Rajab
‘Jeba’ na Mohammed Ibrahim/Vincent Barnabas.
Katika michezo mingine iliyofanyika jana, Coastal Union ilifungana
bao 1-1 na Coastal Union Uwanja wa Mkwakwani Tanga, wakati JKT Ruvu
imefungwa mabao 5-1 na Mgambo Shooting Uwanja wa Karume, Dar es Salaam.
Nayo Toto Africans ililala bao 1-0 kwa Prisons kwenye Uwaja wa CCM
Kirumba Mwanza. Katika mchezo mwingine Stand United iliifunga Kagera
Sugar 1-0 Uwanja wa Kambarage, Shinyanga huku Mbeya City ikiifunga
Mwadui FC bao 1-0.
Wakati huohuo, ligi hiyo inaendelea tena leo, wakati Yanga inayoshika
nafasi ya pili itakaposhuka Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuikabili
Ndanda FC ya Mtwara. Ndanda inashika nafasi ya 13 kati ya timu 16
zinazoshiriki ligi hiyo ikiwa na pointi tisa na bado ipo ukanda mbaya wa
timu za kushuka daraja.
Kutokana na mazingira hayo ni wazi Ndanda FC itataka kupambana ili
itoke mkiani mwa msimamo wa ligi, huku Yanga nayo ikitaka kutumia mechi
hiyo kuzidi kujiweka sawa kileleni.
Pia Yanga itatumia mchezo wa leo kuwafariji mashabiki wake baada ya
kutolewa Nusu Fainali ya Kombe la Mapinduzi kwa mikwaju ya penalti 4-3
na URA ya Uganda Jumapili wiki iliyopita.
Akizungumza na gazeti hili, kiungo wa kimataifa wa Yanga raia wa
Zimbabwe, Thabani Kamusoko, amewataka wachezaji wenzake kusahau ya Kombe
la Mapinduzi na kuelekeza nguvu zao katika kupigania ubingwa wa Ligi
Kuu Tanzania Bara.
Kamusoko, ambaye kwa sasa ni kipenzi cha mashabiki wa timu hiyo
kutokana na uwezo wake, alisema haitapendeza kama wataendelea kupoteza
nguvu kufikiria mambo yaliyopita, wakati bado wanakabiliwa na mtihani
mkubwa kupigania ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu.
“Ni matokeo ambayo yalikuja tofauti na matarajio yetu, lakini
hatuwezi kupoteza muda kufikiria mambo ya Kombe la Mapinduzi cha msingi
kwetu ni kuongeza nguvu kwenye mazoezi yetu, ili tuweze kupoza machungu
yetu kwa kubeba ubingwa wa Tanzania Bara,” alisema Kamusoko.
Chanzo Gazeti la HabariLeo.
Saturday, 16 January 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment