Wednesday, 13 January 2016

Tagged Under:

Shein: Mapinduzi Zanzibar yatalindwa

By: Unknown On: 00:53
  • Share The Gag
  • Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein akiwapungia wananchi baada ya kuwasili kwenye Uwanja wa Amaan kuhudhuria sherehe za Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar mjini Unguja jana.

    RAIS wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein amewataka wananchi wa Zanzibar, kulinda na kuenzi Mapinduzi ya Januari mwaka 1964 kwa nguvu zote.
    Amesisitiza kuwa mapinduzi hayo, ndiyo kielelezo cha utu wa Mwafrika kuheshimika na kuwa huru katika nchi yake. Dk Shein alisema hayo katika kilele cha sherehe za miaka 52 ya Mapinduzi ya Zanzibar, zilizofanyika katika Uwanja wa Amaan mjini hapa.
    Sherehe hizo zilihudhuriwa na viongozi wa kitaifa, akiwemo Rais wa Muungano, John Magufuli na wananchi wa mikoa mitano ya Unguja na Pemba.
    Alisema wananchi wa Zanzibar wanayo kila sababu ya kusherehekea na kuadhimisha Mapinduzi ya Zanzibar, kwani matunda yake yamewanufaisha wananchi wote bila ya kubagua.
    Alisema malengo ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964, ambayo yaliwafanya waasisi kufanya Mapinduzi, yanaendelea kutimizwa na kutekelezwa kwa vitendo katika sekta mbali mbali muhimu, ikiwemo elimu na sekta ya afya.
    Huduma za afya
    Rais Shein ambaye alitumia muda mrefu kuelezea mafanikio yaliyopatikana katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, alisema sekta ya afya imepata mafanikio makubwa, ikiwemo kufuta ada zilizokuwa zikitozwa kwa wajawazito wakati wa kujifungua katika hospitali za serikali.
    Alisema hatua hiyo imesaidia mno, ambapo mwaka 2014/2015 idadi ya wanaojifungua katika hospitali za serikali imefikia asilimia 67.8 kutoka asilimia 56.1 katika mwaka 2013.
    “Haya ni mafanikio makubwa ambayo yanakwenda moja kwa moja na malengo yetu ya kupambana na vifo vya akinamama vinavyotokana na uzazi na kuwafanya akinamama wote kujifungua na kupata huduma kutoka kwa wataalamu wanaotambuliwa,” alisema.
    Alisema SMZ hivi sasa imefuta gharama zote zilizokuwa zikitolewa za kuchangia matibabu katika hospitali kuu za serikali kwa vipimo vya uchunguzi wa maradhi mbali mbali.
    Hatua hiyo imeimarisha huduma za afya katika hospitali kuu za serikali, ikiwemo ya Abdalla Mzee iliyopo Pemba, ambayo ujenzi wake utakapomalizika mwaka huu, itakuwa na hadhi ya rufaa.
    “Ujenzi wa hospitali ya Abdalla Mzee unaofanywa na marafiki zetu wa China, ukimalizika utaifanya kuwa na hadhi ya rufaa kwa kutoa huduma za tiba zote ikiwemo upasuaji wa aina mbali mbali,” alisema.
    Sekta ya elimu
    Alisema sekta ya elimu imepata mafanikio makubwa mara baada ya mapinduzi ya mwaka 1964. Shule za maandalizi zimefikia 270, wakati shule za msingi kwa mwaka jana, zimefika 370.
    Shein alisema idadi ya shule za sekondari, imeongezeka kutoka 210 hadi kufikia 263 huku serikali ikiweka mkazo zaidi katika ujenzi wa vyuo vya amali. Vitajengwa Makuchuchi na Mtambwe katika mwaka ujao wa fedha kutokana na Mkopo wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB).
    Mambo mengine yaliyofanywa ni serikali kutilia mkazo ujenzi wa vyuo vya amali kwa ajili ya kuwezesha wahitimu wake kuwa na ujuzi, utakaowafanya kujiajiri moja kwa moja. Utunzaji mazingira Aidha Shein aliwataka wananchi kupambana na vitendo vya uharibifu wa mazingira vinavyokwenda sambamba na mabadiliko ya tabia ya nchi.
    Alisema serikali imechukua juhudi za makusudi ikiwemo kuundwa kwa mamlaka ya usimamizi wa mazingira kukabili athari zinazojitokeza ikiwemo za ukataji miti.
    Alisema miti aina ya mikoko milioni 50, inatarajiwa kuoteshwa kwa ajili ya kukabili athari za mazingira na kuzuia kasi ya maji ya bahari kuvamia maeneo ya nchi kavu.
    Pensheni kwa wazee
    Kuhusu mikakati ya kutunza wazee wasiojiweza, Dk Shein alisema moja ya malengo ya mapinduzi ya mwaka 1964 ni kuona wazee wanalindwa na kuenziwa.
    Alitoa mfano wa Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Abeid Amaan Karume aliyeamua kujenga makazi ya kudumu eneo la Sebleni na Pemba.
    Alisema katika mwaka wa fedha 2016, serikali ipo katika hatua za mwisho za kusajili wazee waliostaafu, ambao watakuwa wakilipwa fedha za pensheni ya jamii kwa wazee waliofikia umri wa miaka 70.
    Jumla ya wazee 22,243 wamesajiliwa kwa ajili ya malipo ya pensheni huku serikali ikiwa imetenga Sh milioni 20 kwa ajili ya kupunguza makali ya ugumu wa maisha kwa wazee wastaafu wote waliofikia umri wa miaka 70.
    Hali ya kisiasa
    Kuhusu hali ya kisiasa Zanzibar ambayo imetokana na kufutwa kwa uchaguzi mkuu wa Oktoba 25 mwaka jana, Dk Shein aliwataka wananchi kuwa watulivu.
    Aliwahakikishia kwamba mazungumzo ya kusaka suluhu yanayowahusisha viongozi waliopo serikalini na wastaafu, yanaendelea vizuri. Uchaguzi wa Oktoba 25 ulifutwa na Tume ya Uchaguzi wa Zanzibar (ZEC) na kutangazwa katika gazeti rasmi la serikali la Novemba 6 mwaka jana.
    “Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 na Sheria ya Uchaguzi Namba 11 ya mwaka 1984, ndiyo inayosimamia uchaguzi chini ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar ( ZEC) kwamba uchaguzi huo umefutwa...Tume ya uchaguzi itatangaza tarehe nyingine ya kurudiwa kwa uchaguzi huo,” alisema Shein.
    Aliwapongeza wananchi kwa kudumisha amani na utulivu katika kipindi chote; hatua aliyosema imeifanya Zanzibar kupiga hatua kubwa ya maendeleo ya kiuchumi na uwekezaji wa sekta mbali mbali na kupokea watalii kama kawaida. Oktoba 28 mwaka jana, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha, alitoa “Taarifa Kwa Umma ya Kufuta Uchaguzi wa Zanzibar”.
    Katika taarifa hiyo, Jecha Salim Jecha alisema “Mimi nikiwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, nimeridhika kwamba uchaguzi huu haukuwa wa haki na kuna ukiukwaji mkubwa wa Sheria na taratibu za uchaguzi. Hivyo, kwa uwezo nilionao natangaza rasmi kwamba uchaguzi huu na matokeo yake yote yamefutwa na kwamba kuna haja ya kurudia uchaguzi huu”.
    Jecha alitaja sababu zilizosababisha kufutwa kwa uchaguzi huo wa Zanzibar kuwa ni: Baadhi ya vituo vya uchaguzi katika Kisiwa cha Pemba kuwa na idadi kubwa ya kura, zilizopigwa kuliko idadi ya watu waliopo katika Daftari la Wapiga Kura.
    Sababu nyingine ni kadi za kupigia kura hazijachukuliwa, lakini watu wamepiga kura. Jecha alisema sababu nyingine ni kuvamiwa kwa vituo vya kupigia kura na kuibuka kwa fujo na kusababisha watu wengine kushindwa kupiga kura.
    Fujo katika vituo vya kupigia kura zilijitokeza katika majimbo yaliyopo kisiwa cha Pemba, ikiwemo Micheweni, Tumbe na Konde. Alitaja sababu nyingine ni vyama vya siasa kuingilia mchakato na kazi za Tume ya Uchaguzi na hatimaye baadhi ya vyama, kujitangazia ushindi katika uchaguzi huo, ikiwa ni kinyume cha sheria za Tume ya Uchaguzi.
    Alisema uamuzi wa kutangaza matokeo ya urais kinyume cha sheria za Tume ya Uchaguzi ni hatari na ungeweza kuliingiza taifa katika machafuko.
    Januari 12 kila mwaka ni maadhimisho ya mapinduzi ya mwaka 1964, ambayo yaling’oa utawala wa sultani kutoka Oman na wananchi wazalendo walio wengi kushika hatamu ya uongozi.
    Mapinduzi hayo yaliongozwa na Rais wa kwanza wa Zanzibar, Abeid Amaan Karume, ambaye mwaka 1972 Aprili aliuawa na wapinga maendeleo, ikiwa ni sehemu ya jaribio la kupindua utawala uliokuwa ukiongozwa na chama cha Afro Shiraz (ASP), ambacho mwaka 1977 kiliungana na TANU kuanzisha CCM.
    Rais Magufuli ashangiliwa
    Mamia ya wananchi wa mikoa mitano ya Unguja, walijitokeza kwa wingi katika Uwanja wa Amaan, kusherehekea miaka 52 ya Mapinduzi ya Zanzibar. Maandamano ya wananchi hao wa mikoa mitano ya Unguja, yalipita mbele ya mgeni rasmi Rais wa Zanzibar, Dk Shein na wageni mashuhuri.
    Ngoma ya asili za watu wa Unguja na gwaride la vikosi vya ulinzi, vikiongozwa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), vilipamba sherehe hizo. Wananchi walianza kuingia uwanjani kuanzia saa 1 asubuhi. Baadaye umati wa watu ulifurika huku wengine wakilazimika kubaki nje ya uwanja.
    Meli ya Mv Mapinduzi ililazimika kusafirisha wananchi kutoka Kisiwa cha Pemba kuhudhuria sherehe hizo.
    ‘Yadumu mapinduzi ya Januari 1964’ ni maneno yaliyoandikwa katika baadhi ya mabango, yaliyobebwa na waandamanaji waliopita mbele ya mgeni rasmi. Rais John Magufuli alishangiliwa kwa nguvu na wananchi alipoingia uwanjani hapo na kupigiwa wimbo wa taifa.
    “Hapa Kazi Tu” ni kauli zilizosikika kutoka kwa wananchi katika uwanja huo, ambapo ni mara ya kwanza kwa Magufuli kuhudhuria sherehe hizo za kitaifa za Mapinduzi, akiwa Rais wa Muungano.
    Chanzo Gazeti la HabariLeo.

    0 comments:

    Post a Comment