Rais John Magufuli akicheza ngoma ya kimasai pamoja na wananchi muda mfupi baada ya
kuwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) jana,
akiwa njiani kwenda Arusha kwa ziara ya kikazi.
RAIS John Magufuli ametoa mwito kwa Watanzania kumuombea ili aendelee
kuwashughulikia wote wanaofanya ubadhirifu wa fedha za umma kupitia
kampeni yake ya kutumbua majipu.
“Nataka niwahakikishieni kuwa nitaendelea kutumbua majipu yote mpaka
yaishe, na naomba mniombee ili kazi hii ya kutumbua majipu ifanyike kwa
mafanikio,” alisema Dk Magufuli.
Alitoa kauli hiyo wakati alipokuwa akizungumza na wananchi katika
mikoa ya Kilimanjaro na Arusha jana, alipotua kwa ziara ya kikazi ikiwa
ni ya kwanza kwao tangu achaguliwe kushika wadhifa huo Novemba 5, mwaka
jana.
Dk Magufuli aliwasili mkoani Arusha, ambako kesho atatunuku Kamisheni
kwa maofisa wanafunzi wa kundi la 57/15 katika Chuo cha Mafunzo ya
Kijeshi (TMA) Monduli mkoani hapa.
Rais Magufuli aliwasili mjini Arusha akitokea Uwanja wa Ndege wa
Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), alikotua kwa ndege akitokea jijini Dar
es Salaam na kupokewa na mamia ya wananchi. Akiwa uwanjani hapo, Rais
Magufuli aliwashukuru wananchi kwa mapokezi makubwa aliyoyapata na
aliwaeleza kuwa uchaguzi umekwisha, kilichobaki ni kazi tu.
“Nawashukuru sana ndugu wananchi kwa mapokezi haya makubwa, naomba
kuwahakikishia kuwa uchaguzi umekwisha na sasa kilichobaki ni kuchapa
kazi tu,” alisema Rais Magufuli.
Akiwa njiani kutoka KIA, Rais Magufuli alisimamishwa na wananchi wa
njiapanda ya KIA, Kikatiti, Usa River, Tengeru na Mount Meru mjini
Arusha ambako huko kote pamoja na kusisitiza kuwa uchaguzi umekwisha na
kilichobaki ni kuchapa kazi, aliwahakikishia kuwa hatawaangusha.
Aidha, Rais Magufuli alisema tayari serikali imeanza kutoa fedha kwa
ajili ya kugharimia elimu ya msingi na sekondari baada ya kufuta ada na
alionya kuwa watumishi wa umma hususani wakuu wa shule watakaothubutu
kufanya ubadhirifu wa fedha hizo watashughulikiwa.
Alisema yote aliyoyaahidi kwa wananchi wa mkoa wa Arusha na
Watanzania kwa ujumla, ikiwemo ujenzi wa barabara za Arusha, kulipa
fidia za wananchi na kufuta ada ya shule za msingi na sekondari
yanatekelezwa.
Rais Magufuli alisisitiza kuwa serikali yake haitawabagua Watanzania
kwa dini zao wala makabila yao na wala haitawabagua kwa misingi ya vyama
vyao na kanda zao. Aliwataka Watanzania wote kuiweka mbele Tanzania na
kushirikiana kuiendeleza.
Chanzo Gazeti la HabariLeo
Friday, 22 January 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment