Jengo la Mahakama Kuu. |
MKURUGENZI wa Kampuni ya Six Telecoms, Hafidh Shamte na wafanyakazi wengine watano, wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashitaka ya uhujumu uchumi kwa kuisababishia serikali hasara ya Sh bilioni nane.
Washitakiwa walifikishwa mahakamani na kusomewa mashitaka mawili na mawakili kutoka Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA), Jackline Nyantori na Johanes Kalungura wakisaidiwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Theophil Mutakyawa, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Respicius Mwijage.
Mbali na Shamte ambaye jina lake jingine ni Rashid, washitakiwa wengine ni Ofisa Mkuu wa kitengo cha Fedha, Raphael Hongo, Mha sibu Said Ally, Ofisa Masoko, Noel Chacha, Msimamizi wa mtandao, Tinisha Max na Mkuu wa takwimu za biashara, Vishno Konreddy.
Akisoma mashitaka, Jackline alidai, katika tarehe tofauti kati ya Mei 2010 na Januari mwaka huu, Dar es salaam, kwa lengo la kujipatia fedha, washitakiwa walitoza huduma za simu za kimataifa chini ya dola za kimarekani senti 25 kwa dakika.
Wakili Jackline, alidai jambo hilo lilisababisha washindwe kuilipa TCRA, mapato ya dola za Marekani milioni 3,836,861 zilizopatikana kutokana na huduma za simu za kimataifa zilizokuwa zinaingia.
Katika mashitaka mengine ilidaiwa, katika tarehe hizo, kutokana na kutoza chini ya dola za kimarekeni senti 25 kwa dakika na kushindwa kuilipa TCRA mapato yanayotokana na huduma hiyo, waliisababishia mamlaka hiyo hasara ya dola za kimarekani 3,836,861, sawa na Sh bilioni nane za kitanzania.
Wakili Jackline alidai, upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na kuomba tarehe nyingine ya kutajwa. Awali, kabla washitakiwa hawajasomewa mashitaka, Hakimu Mwijage aliwaambia washitakiwa hawaruhusiwi kujibu mashitaka kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo isipokuwa Mahakama Kuu, au endapo Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) atatoa kibali kwa mahakama hiyo kusikiliza kesi hiyo.
Aidha alisema mahakama haiwezi kutoa dhamana, hivyo wapeleke maombi ya dhamana Mahakama Kuu. Washitakiwa walirudishwa rumande na kesi hiyo iliahirishwa hadi Janurai 28 mwaka huu itakapotajwa tena.
Wakati huo huo, Mwanasheria Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Johanes Kalungura ametoa siku saba kwa Bodi ya waku rugenzi wa kampuni ya Six Telecoms Tanzania Limited, kuilipa mamlaka hiyo deni la Sh bilioni nane.
Kalungura alisema hayo jana, Dar es Salaam, akiwa nje ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu baada ya kuwafikisha mahakamani wafanyakazi watano wa kampuni hiyo kwa kuisababishia serikali hasara ya Sh bilioni nane.
Akizungumza na waandishi wa habari, Kalungura alisema “naomba wakurugenzi wote au bodi ya wakurugenzi walipe fedha za wananchi, shilingi bilioni nane ndani ya siku saba kuanzia leo (jana), wasipofanya hivyo sheria itachukua mkondo wake dhidi yao” .
Aidha aliwakumbusha wamiliki wa makampuni yote yanayotoa huduma za mawasiliano, ambao wanajua hawajalipa tozo za nchi, walipe haraka kwa sababu wasipolipa watashughulikiwa kwa mujibu wa sheria.
Chanzo HabariLeo
0 comments:
Post a Comment