NA SHABANI MATUTU, DAR ES SALAAM
SPIKA wa Bunge, Job Ndugai, anatarajia kutangaza kamati za Bunge leo.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Ndugai alisema atatangaza kamati hizo
chini ya utaratibu mpya na kwamba leo atatangaza Kamati ya Kanuni pekee.
Baada ya kuitangaza kamati hiyo, nyingine zilizobaki atazitangazia
mjini Dodoma wakati vikao vya Bunge vitakapokuwa vikiendelea mwishoni
mwa mwezi huu.
Utaratibu huo umebainishwa na Ndugai alipoulizwa na gazeti hili
ambalo lilitaka kujua iwapo Kamati za Bunge zitatangazwa kabla ya kuanza
kwa Bunge lijalo Januari 26, Mwaka huu.
“Kesho (Leo) nitatangaza kamati moja tu ya kanuni na nyingine
nitazitangazia mjini Dodoma kabla ya kuanza kwa Bunge lijalo,” alijibu
kwa ufupi.
Taarifa ambazo zimelifikia gazeti hili zinasema kwamba Spika Ndugai
amepanga kupunguza wingi wa Kamati za Bunge ili kuendana na uchache wa
wizara zilizopo.
Taarifa zaidi zinasema kuwa sababu kubwa ya kufanya hivyo ni
kuhakikisha kamati zinakuwa chache lakini zilizo na uwezo wa kufanyakazi
kwa kasi ambayo itaisaidia serikali ya awamu ya tano.
Baada ya leo kutangaza Kamati ya Kanuni, Spika Ndugai atabaki na
jukumu la kutangaza kamati nyingine 14 mjini Dodoma, iwapo hakutakuwa na
ongezeko la kamati.
Kamati za Bunge huundwa kwa mujibu wa Katiba Ibara ya 96, likiwa
limepewa madaraka ya kuunda kamati za Bunge za aina mbalimbali na muundo
wake umefafanuliwa na Kanuni za Kudumu za Bunge.
Katika muundo huo zipo kamati za kisekta na zile zisizokuwa za
kisekta, ambazo kwa pamoja hufanyakazi na kutekeleza majukumu yao kwa
niaba ya Bunge.
Kwa mujibu wa Kanuni ya 89 Bunge limeunda Kamati 15, ambapo baadhi ya
kamati hizo ni Kamati ya Haki, Maadili, Kinga na Madaraka ya Bunge na
Kamati ya Uchumi, Viwanda na Biashara.
Chanzo Mtanzania.
Monday, 11 January 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment