NA SHABANI MATUTU, DAR ES SALAAM
WANANCHI wa Kunduchi Mtongani, jijini Dar es salaam wameokota mwili wa mtoto mchanga aliyenyofolewa kichwa kwa kuliwa na mbwa.
Mmoja wa shuhuda wa tukio hilo, Thomas John aliliambia MTANZANIA
kwamba wananchi walikibaini kichanga hicho baada ya kuburuzwa na mbwa
kutoka kichakani kilikokuwa kimetupwa.
“Mtoto mchanga naona amezaliwa alfajiri ya leo (jana) na kutelekezwa
na mama yake ambaye hadi muda huu wa saa 11 jioni bado hatujamtambua.
“Hili linaonekana sasa kuwa tatizo sugu kwa wanawake wenye roho za
kinyama. Leo binadamu analiwa na mbwa kweli jamani Mungu wangu dunia
yetu hii tunakwenda wapi,” alisema kwa masikitiko John
Alisema baada ya kubainika kwa mwili wa kichanga hicho walitoa
taarifa kwa Mjumbe wa Nyumba Kumi ambaye aliwasiliana na polisi ili waje
kwa ajili ya hatua za uchunguzi, lakini hadi kufikia saa 12 jioni
hakuna askari aliyefika katika eneo hilo.
Mkazi mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Hussein Juma alisema
kwamba iwapo tukio hilo litaachwa bila kufanyika kwa uchunguzi wa
kumpata muhusika upo uwezekano mkubwa kwa wanawake kuendelea kutupa
watoto.
Alipoulizwa kuhusu tukio hilo, Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Kinondoni,
Camillius Wambura, alisema hana taarifa hizo, huku akiahidi kufutilia
tukio hilo kwa ajili ya uchungu wa kina.
“Kwa kifupi sijapata taarifa hizo ndiyo kwanza unanipatia ila Jeshi
la Polisi litafuatilia kwa karibu na likifanikiwa kumpata mtuhumiwa wa
tukio hilo hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake na tutatoa taarifa
kwa umma,” alisema Kamanda Wambura.
Chanzo Mtanzania.
Monday, 11 January 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment