KATIBU Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad,
leo anatarajia kufichua siri ya mazungumzo ya kusaka suluhu, baada ya
matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar kufutwa mwaka jana.
Habari za uhakika ambazo zimelifikia MTANZANIA jjini Dar es Salaam
jana zinasema kwamba, Maalim Seif atakutana na waandishi wa habari
kueleza kwa kina mwenendo wa mazungumzo hayo baina ya CUF na CCM
yalipofikia.
Maalim Seif, anachukua uamuzi huo wakati hali ya kisiasa visiwani
humo ikizidi kuwa ngumu kwa pande zote, licha ya Rais Dk. John Magufuli
kuahidi kuupatia ufumbuzi mgogoro huo.
Maalim Seif anajitokeza leo, wakati wiki iliyopita Rais Magufuli
alikutana na viongozi wastaafu, ambao kwa pamoja walizungumza mambo
mazito ya kitaifa pamoja na kutakiana heri ya mwaka mpya.
Wiki iliyopita Rais Dk. Magufuli alikutana na kufanya mazungumzo na
Rais mstaafu, Benjamin Mkapa ambaye alimhakikishia kumpa ushirikiano
atakapohitajika kufanya hivyo.
Katika kumhakikishia kuwa yuko tayari kufanyakazi atakayomtuma,
taarifa za ndani zinaeleza kuwa moja ya jambo kubwa ambalo Mkapa anaweza
kulisimamia ni suala la kusaka suluhu ya Zanzibar.
Akizungumza baada ya mazungumzo hayo, Mkapa alisema lengo la mkutano
huo ni kumpongeza Rais Dk. Magufuli kwa dhamana aliyopewa na Watanzania
na kumtakia heri ya mwaka mpya.
Mkapa alimhakikishia Rais Magufuli kuwa yupo tayari kutoa ushirikiano
wakati wowote na kufanya kazi yoyote endapo atahitajika kufanya hivyo.
Licha ya Mkapa, Rais Magufuli pia alikutana na Rais mstaafu wa awamu
ya nne, Jakaya Kikwete, ambaye alikabidhi baadhi ya nyaraka kwa Rais
Magufuli.
Kikwete alikabidhiwa nyaraka hizo zinazohusiana na mgogoro huo na
aliyekuwa mgombea urais wa Zanzibar kupitia Chama cha Wananchi (CUF),
Maalim Seif Sharif Hamad, Novemba 4, mwaka jana.
Inaelezwa kuwa Maalim Seif alikabidhi nyaraka mbalimbali, zikiwamo
fomu za matokeo ya Uchaguzi Mkuu kwa vituo vyote vya Zanzibar.
Mbali na kukutana na watangulizi wake hao pia alikutana na aliyekuwa
Mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Mstaafu
Joseph Warioba.
Katika mazungumzo hayo, licha ya Jaji Warioba, kumtakia heri ya mwaka
mpya, alimpongeza Rais Dk. Magufuli kwa jinsi alivyoanza kazi vizuri,
lakini pia wakazungumzia mchakato wa Katiba mpya na hali ya kisiasa
Zanzibar.
MAALIM KUUNGURUMA LEO
Naye Maalim Seif, leo natarajia kuzungumza na waandishi wa habari
kueleza hatima ya mazungumzo ya kisiasa ya kutafuta mwafaka Zanzibar
“Maalim Seif kesho (leo), atazungumza na wahariri na waandishi wa
habari juu ya mwenendo wa mazungumzo ya maridhiano Zanzibar,” ilisema
taarifa hiyo iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana.
Dk. Shein na Magufuli
Desemba 24, mwaka huu Rais Magufuli alikutana na Rais wa Zanzibar,
Dk. Ali Mohamed Shein Ikulu, Dar es Salaam kuhusu mwenendo wa mazungumzo
hayo na hali ya kisiasa visiwani humo.
Mazungumzo hayo yalifanyika, ambapo taarifa ya kukutana kwa viongozi
hao ilitolewa kwa vyombo vya habari jioni na Kaimu Mkurugenzi wa
Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu, Gerson Msigwa.
Taarifa hiyo ilieleza baada ya mazungumzo ya viongozi hao, Rais Shein
alieleza kuwa lengo la mazungumzo yao ilikuwa ni kumpa taarifa Rais
Magufuli kuhusu hali ya mazungumzo ya kutafuta mwafaka wa kisiasa
Zanzibar.
Taarifa ilieleza kuwa Dk. Shein alisema mazungumzo hayo yanaendelea
vizuri chini ya Kamati Maalumu ya kutafuta suluhu iliyopo chini ya
uenyekiti wake.
Mbali ya Dk. Shein, wajumbe wengine ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa
Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Balozi Seif Ali Idd na Rais mstaafu wa awamu ya pili Alhaji Ali Hassan
Mwinyi.
Wengine ni Rais Mstaafu Jakaya Kikwete, Rais Mstaafu wa awamu ya sita
wa Zanzibar Dk. Amani Abeid Karume na Rais Mstaafu wa awamu ya tano wa
Zanzibar, Salmin Amour.
Dk. Shein alisema amemtaarifu Rais Magufuli kuwa kamati yake ilianza
mazungumzo Novemba 9, mwaka huu na hadi sasa bado inaendelea na kazi
yake.
“Nimekuja kumpa taarifa Rais Magufuli kuhusu maendeleo ya mazungumzo
yetu ili aweze kujua kinachoendelea akiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania ambayo Zanzibar ni sehemu yake, na sisi ni jukumu letu kumpa
taarifa,” ilieleza taarifa hiyo.
Kabla ya kukutana na Rais Shein, tayari Desemba 21, mwaka jana Rais
Magufuli alikutana na Maalim Seif, Ikulu Dar es Salaam na kuzungumzia
mgogoro huo wa Zanzibar.
TAASISI NA UCHAGUZI
Wiki iliyopita, Jumuiya ya Maimamu Zanzibar (JUMAZA) na Taasisi za
Kiislamu zilitoa waraka kwa pamoja zikipinga kurudiwa Uchaguzi visiwani
humo, kwa hoja kuwa hazioni busara yoyote kwa sababu Uchaguzi wa
awali ulifanyika kwa ufanisi wa hali ya juu.
Waraka wa viongozi wa dini ya Kiislamu uliosainiwa na Katibu Mtendaji
wa JUMAZA, Muhidin Z. Muhidini, ambaye ulisema Uchaguzi wa Oktoba 25,
mwaka jana ulikuwa na waangalizi katika majimbo yote ya Unguja na Pemba
na kasoro zilizoripotiwa ni ndogo mno, ikilinganishwa na Uchaguzi
wowote uliopita tangu mfumo wa vyama vingi urejeshwe mwaka 1992.
KARUME
Kwa upande wake, mwanadiplomasia wa siku nyingi, Balozi Ally Abeid
Karume amejutia kitendo kilichofanywa CCM kukubaliana na viongozi wa
CUF kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK).
Akizungumza wakati wa kongamano lililoandaliwa na vijana wasomi
wanaounda Shirikisho la Wasomi wa Elimu ya Juu wa CCM jana, Ally ambaye
pia ni mtoto wa kwanza wa Rais wa Kwanza wa Serikali ya Mapinduzi
Zanzibar, Hayati Abeid Aman Karume alisema kitendo hicho ndicho
kinachowapa shida CCM hadi leo.
“Nafikiri tulikurupuka, waliposimamia viongozi wetu waliteleza kwa
sababu hawakupata maoni ya wanachama juu ya suala hili, chama
kinachoshinda kijenge Serikali na wale wengine wabaki kuwa wapinzani…
imani yao ilikuwa tuwe kitu kimoja, haki na amani ipatikane, imekuwa
sivyo.
“Tumejikuta wenzetu tumewapa uwezo, umaarufu, nyezo katika uchaguzi
wameleta shida. Waziri Kiongzi Mstaafu ‘Shamsi Vuai Nahodha’ niliwahi
kukwambia siku moja katika miaka mitano iliyopita, walianza kusema
hakuna SUK, bali ipo ya CUF na hadi wakurugenzi walisema wa kwao hadi
uchaguzi umesimamiwa na wao. Hakuna utaratibu huo duniani.
“Tuliteleza tukafika huko tulipofika, mkiona mmeharibikiwa lakufanya
si kunyoosheana vidole, bali kurekebisha pale ambapo tuliona
haikutusaidia,” alisema.
Aliwataka Wazazibari kujitokeza kwa wingi kwenye uchaguzi
unaotarajiwa kufanyika hivi karibuni ili CCM ipate ushindi wa kishindo.
“Tujitokeze kwa wingi ili tushinde kwa kishindo,baada ya hapo
turekebishe Katiba kwa sababu tatizo hili linatokana na Katiba lazima
ieleze kwamba Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi lazima atokane
na CCM, ingawa vyama vyote vya siasa vitaruhusiwa kushiriki uchaguzi na
kubakia wapinzani kama ambavyo Uingereza inafanya kiongozi anatoka
katika familia ya Malikia na hakuna malalamiko,” alisema.
NAHODHA
Kwa upande wake, Waziri Kiongozi Mstaafu, Shamsi Vuai Nahodha alisema
silaha kubwa itakayowakomboa Wazanzibari wakati wakitafakari mapinduzi
ni elimu.
“Binafsi ninapotafakari juu ya mapinduzi leo, yapo mambo yanayonitia
shaka juu ya uwezo na dhamira yetu ya kuyadumisha, unaweza kuwa na uwezo
usiwe na dhamira au ukawa na dhamira huku uwezo huna lazima haya yaende
sambasamba.
“Wapo baadhi yetu tukizungumza namna ya kuyadumisha wanadhani kazi
yetu kama vijana na viongozi ni kudumisha vielelezo vya mapinduzi kama
vile majengo ya maendeleo yaliyojengwa vijijini na michenzani.
“Nilikwenda China mwaka 2003, walikuwa na nyumba kama zetu za
wanyonge, nikaenda tena 2011 sikuziona, nilipoenda 2013, nikakuta
wamejenga majengo mengine ndio maana nasema sisi kazi yetu si kudumisha
vielelezo,” alisema.
Naye Mwenyekiti wa Shirikisho hilo, Zainab Abdalah alisema
wataendelea kutoa ushirikiano kwa Rais Dk. John Magufuli kwa kumwonesha
majipu makubwa na kuyatumbua yale madogo.
Alisema wataendelea kuyalinda Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuwaelimisha Wazanzibari wote juu ya umuhimu wake.
Chanzo Mtanzania.
Monday, 11 January 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment