*Asema hakuna mwananchi atakaye nyanyasika
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano, Mazingira),
January Makamba, amefanya ziara na kujionea namna wananchi waliobomolewa
nyumba zao wanavyoishi kwa kukosa makazi.
Kutokana na hali hiyo, amesema hakuna mwananchi anayeonewa au
anayeteseka na kunyanyasika katika kazi ya kuwaondoa wakazi wanaoishi
katika Bonde la Msimbazi ila kazi hiyo inafanyika kwa mujibu wa sheria.
Hayo aliyasema jijini Dar es Salaam jana, baada ya kuwatembelea
wananchi wa maeneo mbalimbali ambao nyumba zao zimebomolewa na nyingine
kuwekewa alama ya X kwa ajili ya kubomolewa.
Katika ziara hiyo, Makamba alijionea hali mbali ya uchafuzi wa
mazingira hasa katika maeneo ya Kigogo,Mburahati na na Kinondoni
Mkwajuni.
Akizungumza na wananchi wa maeneo hayo, Makamba alisema Serikali
haiwezi kuvumilia kuendelea kuwaona wananchi wanakufa kila mwaka
kutokana na mafuriko na wengine wanaishi katikati ya bonde na kwenye
kingo za mito, huku wakielekeza majitaka yao kwenye mito na mifereji.
Alisema kazi ya kuondoa wakazi itazingatia misingi ya ubinadamu.
“Hakuna mtu atakayekurupushwa na kubomolewa nyumba anayoishi bila
yeye na Serikali kuthibitisha kama hakumilikishwa kiwanja au nyumba, na
kwamba anapoishi hapastahili kwa makazi na shughuli za binadamu.
“Mtu yeyote ambaye amemilikishwa eneo na Serikali na amepewa kibali
cha ujenzi, hataondolewa hadi atakapopewa kiwanja mbadala, ila Serikali
yetu inataka sheria zifuatwe lakini pia ina sura ya kibinadamu,” alisema
January.
Akiwa katika eneo la Kinondoni Mkwajuni, Waziri Makamba alikagua
uzoaji wa kifusi kilichotokana na ubomoaji wa nyumba zilizokuwa katika
bonde hilo.
“Tunataka eneo hili liwe safi kabisa ili tuonyeshe mfano wa
maendelezo bora na rafiki kwa mazingira ya maeneo ya mabondeni,” alisema
.
Akiwa katika eneo hilo,alikutana na wananchi ambao waliomba ufafanuzi kuhusu kero mbalimbali wanazozipata.
Alisema Serikali imeomba taarifa kupitia mamlaka za Serikali za mitaa
kuhusu watu wote wenye kuhitaji msaada maalumu wa kibinadamu na
jitihada zitafanyika ili kuweza kuwasaidia watoto waliokuwa wanaishi
mabondeni kuhamishiwa katika shule nyingine.
Kutokana na hali hiyo, January alitoa siku saba kwa viongozi hao
kuhakikisha mito hiyo inakuwa safi kwa kuwashirikisha wananchi kufanya
usafi na kuomba halmashauri husika zitoe magari.
Alisema iwapo viongozi hao watashindwa kutekeleza agizo hilo, basi
kibarua chao kitakuwa shakani, ni pamoja na kuwawajibisha kwakuwa
wamechangia uchafuzi wa mazingira.
Alisema Benki ya Dunia na serikali ya Marekani zimetoa Sh bilioni 100
kwa ajili ya kusafisha mito na kuijengea ili ipitishe maji kwa
mtiririko ambao hautasababisha mafuriko.
“ Hali hii inatisha, haiwezekani kiongozi wa mtaa unaongoza wananchi
katika eneo chafu hivi, ninaondoka leo (jana), Jumapili ijayo nakuja,
kama nitakuta hivi, kazi utakuwa huna leo na kusamehe…itisha mkutano
panga wananchi wako,mfanye usafi,” aliagiza Januari.
Bomoabomoa jijini Dar es Salaam ilianza Desemba 17, mwaka jana ambapo
hadi sasa tayari nyumba kadhaa zimebomolewa na nyingi zimewe kuwekewa
alama ya X.
Chanzo Mtanzania.
Monday, 11 January 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment