Naibu Katibu Mkuu wa CCM- Zanzibar, Vuai Ali Vuai. |
JESHI la Polisi limeanza msako wa watu waliochoma nyumba tano za wananchi wakazi wa Kangagani, ofisi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Kituo cha Afya katika Mkoa wa Kaskazini Pemba.
Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu kutoka Pemba jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba, Hassan Nasiri Ali, alisema watu wanaotafutwa wamechoma nyumba tano za wananchi, Kituo cha Afya cha Kiuyu Minungwini na ofisi ya CCM Tibirinzi.
“Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi kuhusu matukio matatu ya hujuma za kuchoma moto nyumba za wananchi, kituo cha afya na ofisi ya Chama Cha Mapinduzi. Matukio hayo yote yanaonekana kuwa na muelekeo wa vitendo vya hujuma,” alisema.
Kamanda Nasiri alisema katika matukio hayo hadi sasa hakuna mtu anayeshikiliwa Polisi wala hakuna aliyejeruhiwa na Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi kuhusu matukio hayo.
Mkuu wa Mkoa Awali Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Omar Khamis Othman alipiga marufuku mikusanyiko ya watu katika nyakati za usiku ikiwa ni sehemu ya kujaribu kupambana na kupunguza vitendo vya hujuma alivyosema vimelenga kuvuruga uchaguzi wa marudio unaotazamiwa kufanyika Machi 20 mwaka huu.
“Tumepiga marufuku mikusanyiko ya vikundi vya watu katika nyakati za usiku ili kupambana na matukio ya hujuma yanayofanywa zaidi katika kipindi hiki kuelekea katika uchaguzi wa marudio, ambao baadhi ya watu wanataka kuvuruga kwa makusudi na kuzuia haki ya wapiga kura,” alisema.
Awali Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai akizungumza kwa simu kutoka Pemba, alisema matukio hayo yamelenga kuhujumu na kutisha wananchi ambao ni wafuasi wa chama hicho, ili wasijitokeze kupiga kura katika uchaguzi wa marudio.
Akifafanua zaidi alisema matukio hayo yote yanaonesha waziwazi yamelenga wafuasi wa CCM kwa sababu hakuna mwanachama wa CUF, ambaye nyumba yake imeharibiwa na moto.
“Haya matukio yote yanaonesha wazi wazi kwamba ni sehemu ya vitendo vya hujuma kwa ajili ya kuwashambulia wafuasi wa CCM na kuwatisha ili wasijitokeze katika uchaguzi wa marudio’ alisema.
Vuai aliwataka wafuasi wa CCM kuwa watulivu katika kipindi hichi kigumu na kuviachia vyombo vya dola kufanya kazi yake ya uchunguzi na kuwatia hatiani watuhumiwa wa matukio ya hujuma, ambayo hivi sasa yamekuwa yakijitokeza kwa wingi Pemba yakiwalenga zaidi wafuasi wa CCM.
Wananchi wa Zanzibar wapo katika matayarisho ya uchaguzi wa marudio unaotazamiwa kufanyika wiki ijayo Machi 20 mwaka huu, ambapo Tume ya Uchaguzi Zanzibar (Zec), tayari imeanza kutoa mafunzo kwa mawakala wa vyama vya siasa watakaosimamia uchaguzi wa marudio, ambao unafanyika baada ya kufutwa kwa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25.
Chanzo HabariLeo.
0 comments:
Post a Comment