NA GUSTAPHU HAULE, PWANI NA TUNU NASSOR, DAR ES SALAAM
SIRI ya kifo cha aliyekuwa mwanasiasa nguli na Mwenyekiti wa Chama
cha Democratic (DP), Mchungaji Christopher Mtikila, imeanza kufichuka.
Uchunguzi wa kitabibu umebaini kuwa, Mchungaji Mtikila alifariki
dunia baada ya kuvunjika mbavu nane, huku damu nyingi ikivujia katika
mfumo wa hewa, kitendo kilichosababisha ashindwe kupumua.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Kamanda wa
Polisi Mkoa wa Pwani, Jaffari Ibrahim alisema taarifa za kuumia kwa
mwanasiasa huyo zimetokana na uchunguzi uliofanywa na jopo la madaktari
katika Hospitali ya Rufaa ya Tumbi.
Kamnda Ibrahimu, alisema timu maalumu iliyoongozwa na mkuu wa
utawala wa askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani Makao Makuu,
Johansen Kahatano, Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Pwani
na wataalamu wa sayansi ya makosa ya jinai kutoka makao makuu ya polisi
akiwemo daktari wa maabara ya kisayansi inayohusu uchunguzi wa makosa ya
jinai ACP Kashindye, walibaini mambo manne yaliyosababisha kutokea
ajali hiyo.
Alisema kabla ya ajali hiyo kutokea Oktoba 2, mwaka huu, jioni
Mchungaji Mtikila na wenzake waliondoka Dr es Salaam kwenda mkoani
Njombe ambapo walifika Oktoba 3 alfajiri kwa ajili ya kampeni ya chama
chao.
Alisema Mchungaji Mtikila na wenzake wakiwa Njombe, wanadaiwa
walipata ajali kwa kugonga magari mawili yaliyopata na kusababisha
uharibifu wa gari lao.
Baada ya tatizo hilo, walishauriwa kulifanyia matengenezo gari lao kabla ya kuendelea kulitumia.
Hata hivyo, baada ya kumaliza shughuli zao za kichama, Mchungaji
Mtikila na wenzake Oktoba 3, saa 3 usiku waliondoka Njombe kurudi D ar
es Salaam.
Alisema walipofika Kijiji cha Msolwa saa 11:45 alfajiri walipata ajali ambayo inadaiwa chanzo chake ni mwendokasi.
Alisema baada ya timu ya Jeshi la Polisi kukagua tukio na kuwahoji
majeruhi na mashuhuda, inaonyesha wazi chanzo chake ni mwendokasi,
huku dereva wa gari hilo akikiri kosa lake, licha ya kuwapo alama ya
tahadhari ya kupunguza mwendo eneo hilo.
Alisema sababu ya pili, ni uchovu wa dereva kutokana na safari ndefu kwa kuendesha gari usiku na mchana.
“Dereva hakupata muda wa kupumzika, kabla ya kuanza safari yao alikuwa akishughulikia matengenezo ya gari,”alisema Kamanda.
Alisema katika tukio hilo, Mchungaji Mtikila alikuwa hakufunga mikanda .
Kutokana na uchunguzi huo, aliwataka madereva kuzingatia sheria za
usalama barabarani na wale watakaokaidi hatua kali zitaendelea
kuchukuliwa.
Waliojeruhiwa katika ajali hiyo ni Patrick Mgaya (57) ambaye alipata
michubuko kidogo usoni na kuumia kichwani na Geoge Ponera aliyepata
michubuko eneo la mabegani.
KUAGWA
Katika hatua nyingine, mwili Mchungaji Mtikila unatarajiwa kuagwa
kesho nyumbani kwake Mikocheni na kusafirishwa kwenda Ludewa kwa
mazishi.
Akizungumza na waandishi wa habari nyumbani kwa marehemu Mikocheni,
Dar es Salaam jana, Msemaji wa Familia, Stanley Mtikila alisema
wanategemea kuaga mwili huo, kisha kusafirisha hadi kijijini kwao Milo
alikozaliwa kwa mazishi.
“Tutaanza safari ya kwenda Ludewa keshokutwa muda mfupi baada ya
kuaga hapa Dar es Salaam, tunatarajia kuzika siku hiyo, itategemea na
muda tutakaofika,” alisema Stanley.
Alisema kwa kuwa yeye(marehemu), ndiye alikuwa kiongozi wa kanisa, hafahamu ni kiongozi gani wa dini atakayeongoza mazishi hayo.
“Hakuna kiongozi wa Serikali wala wa dini aliyethibitisha kuongoza
mazishi hayo mpaka sasa, bado tunaendelea na mawasiliano nao tutawapa
taarifa kama kutakuwa na mabadiliko yoyote,” alisema Stanley.
Aliyesoma naye
Naye Anyambilile Mwakatobe alimwelezea marehemu Mchungaji Mtikila
kama mtu aliyekuwa na kipawa cha pekee katika kujieleza na kujenga hoja
bila kuogopa mtu yeyote.
Alisema Taifa limepoteza mtu muhimu aliyekuwa msaada wa kimwili na kiroho.
“Tumeachana na Mchungaji Mtikila Alhamisi iliyopita, baada ya kufanya
ibada katika kanisa lake saa 2 usiku na yeye kuondoka Ijumaa jioni
kwenda Njombe kumnadi mgombea ubunge jimboni humo,” alisema Mwakatobe.
Alisema walikutana na marehemu mwaka 1966 katika Shule ya Sekondari ya Malangali iliyopo Iringa na kuwa marafiki.
“Tulikutana na Mchungaji tukiwa na umri wa miaka 16, tukiwa na
Profesa Mark Mwandosya, nakumbuka aliwahi kutengeneza kundi la kuzuia
wizi shuleni hapo,” alisema Mwakatobe.
Mchungaji Mtikila alifariki dunia juzi katika eneo la Msolwa wilaya
ya Bagamoyo mkoani Pwani,baada ya gari waliokua wakisafiria lenye namba
za usajili T 189 AGM aina ya Toyota Corola kuacha njia na kupinduka.
Created by Gazeti la Mtanzania
Tuesday, 6 October 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment