NA MWANDISHI WETU DAR ES SALAAM
MKAKATI wa chama cha ACT Wazalendo kumtumia aliyekuwa Katibu Mkuu wa
Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa kutumia
jukwaa lake ‘kumchafua’ mgombea urais wa Chadema, Edward Lowassa
anayeungwa mkono na vyama vinavyounda Ukawa, umegonga mwamba.
Kukwama kwa mkakati huo kunatokana na kuwapo msigano wa mawazo
miongoni mwa viongozi wa ACT ambao waliona kumtumia Dk. Slaa kuiponda
Chadema na hata Ukawa wataifanya jamii kuamini kwamba wao (ACT)
wanaisaidia CCM katika kampeni zake.
Chanzo cha kuaminika ndani ya ACT kimelidokeza MTANZANIA kuwa mpango
wa kumkaribisha Dk. Slaa kusimama katika jukwaa lake na kuwasema vibaya
viongozi wa Ukawa hususan Lowassa, kungekishushia hadhi chama hicho na
kuonekana kinafanya kazi ya CCM.
“Ni kweli mpango huo ulikuwapo lakini baadhi ya viongozi wa
ACT wamepima uzito wa kumtumia Dk. Slaa katika kampeni
zetu ‘kuwashughulikia’ Ukawa au Chadema kungetuondoa katika mstari wa
upinzani na kuitwa ‘CCM B’ kwa sababu tayari jamii inamuona Dk. Slaa
kama ni msaliti wa mabadiliko kwa sasa,” kilisema chanzo hicho.
Hali hiyo inaungwa mkono na taarifa iliyotolewa na ACT Wazalendo Dar
es Salaam jana kuhusu kuacha kumtumia Dk Slaa katika kampeni zake
kama ilivyotarajiwa, kuwa ni baada ya kufanya tathmini ya kina
na kugundua kuwa hali ya usalama kwa kiongozi huyo si nzuri.
Taarifa hiyo ya ACT imetolewa siku moja baada ya gazeti la
MTANZANIA Jumapili kuripoti kuwapo mpango wa Dk. Slaa kusimama katika
jukwaa la chama hicho kuzungumza kile anachodai kukijua kuhusu
tuhuma mbalimbali za viongozi mbalimbali wa Chadema wakati wa
kuwapokea baadhi ya waliokuwa wanachama wa Chama Cha Mapinduzi
(CCM) waliojiunga na upinzani.
Taarifa kutoka ACT zilisema Dk. Slaa angeungana na Kiongozi Mkuu wa
chama hicho, Kabwe Zitto katika mkutano uliopangwa awali
kufanyika mkoani Iringa katika Uwanja wa Mwembetogwa ambako Katibu Mkuu
huyo wa zamani wa Chadema aliyetofautina na wenzake kabla ya kutangaza
kujitenga nao, angeeleza mambo yaliyofichika kuhusu tuhuma za ufisadi
wanazodaiwa kuhusika nazo baadhi ya viongozi wa vyama vinavyounda Umoja
wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Ukawa unaundwa na Chadema, Chama cha Wananchi (CUF), NCCR-Mageuzi na National League for Democracy (NLD).
Dk. Slaa alitarajiwa kuwatataja kwenye mkutano huo kuwa ni Mwenyekiti
wa Chadema, Freeman Mbowe, Tundu Lissu ambaye ni mwanasheria wa chama
hicho, John Mnyika ambaye ni Naibu Katibu Mkuu Bara na Mbunge wa
Iringa Mjini anayemaliza muda wake, Mchungaji Peter Msigwa. Ingawa ACT
haikuweka wazi kuhusu mpango huo wa kumtosa Dk. Slaa, lakini taarifa
yake ilitoa hoja kwamba usalama wa kiongozi huyo utakuwa mdogo kutokana
na
vitisho mbalimbali anavyovipata na kwamba chama hicho hakina uwezo wa kumhakikishia ulinzi.
“Chama chetu kimekuwa na mawasiliano na Dk. Slaa, mwanasiasa nguli wa
upinzani nchini kuhusu uwezekano wa yeye kushiriki katika kampeni za
chama chetu kwa lengo la kuendeleza vita dhidi ya ufisadi nchini.
“Hivyo kutokana na hali hiyo ya vitisho dhidi ya usalama wake,
chama chetu kimejiridhisha kuwa hakina uwezo wa kumhakikishia
Dk.Slaa usalama wake atakapokuwa jukwaani.
“Kutokana na sababu hizo, ACT kimefuta mikutano yote ya nguli huyo wa
siasa nchini ambayo alikuwa aifanye kupitia jukwaa la chama chetu,”
ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Taarifa hiyo ya ACT ilisema inamshukuru Dk. Slaa kwa imani aliyonayo
juu ya chama hicho na uamuzi wake wa kuikabidhi rasmi mikoba yake ya
vita dhidi ya ufisadi nchini.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Dk. Slaa aliamini kwamba chama
hicho ndicho chama pekee chenye uhalali na uwezo wa kupambana na
ufisadi baada ya chama chake cha zamani Chadema kuitelekeza vita hiyo.
“Dk. Slaa alikuwa ashiriki kwa ukamilifu katika kampeni za uchaguzi
zinazoendelea kupitia jukwaa la ACT Wazalendo kwakuanza kwenye mkutano
wa hadhara mjini Iringa Jumatano Oktoba 7 mwaka huu.
“Baadaye angeendelea na mikutano mingine katika majimbo mbalimbali
na kuhitimisha kampeni hizo katika Viwanja vya Mwembeyanga Dar es
Salaam, ambao ndiyo uwanja ambako vita dhidi ya ufisadi ilitangazwa
rasmi Septemba 15 mwaka 2007,” ilisema taarifa hiyo.
Created by Gazeti la Mtanzania.
Tuesday, 6 October 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment