Afisa Habari wa TFF, Baraka Kizuguto. |
SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limetaja viingilio vya kuiona timu ya Taifa, Taifa Stars, katika mchezo wa kesho dhidi ya Malawi wa kufuzu Kombe la Dunia huku kile cha chini kikiwa ni Sh 5,000.
Ofisa Habari wa TFF, Baraka Kizuguto alisema kuwa, kiingilio cha juu kitakuwa Sh 10,000, na watakaolipa kiasi hicho ni wale watakaokaa VIP B na C. Kizuguto alisema maandalizi ya mchezo huo yamekamilika kwa kuwa tayari wachezaji wote walioitwa kambini wamewasili.
“Mchezo utachezwa kuanzia saa 10:30 jioni kwa ajili ya kuwapa nafasi watu wanaotoka maofisini kushiriki kuishangilia timu ya taifa, tunaomba watu wajitokeze kwa wingi na kuiunga mkono timu yetu ya Taifa,” alisema.
Kizuguto alisema tayari timu ya taifa ya Malawi iliwasili juzi na kufikia katika Hoteli ya Demaji Mwananyamala, ambapo leo watafanya mazoezi ya mwisho kwenye Uwanja wa Taifa kabla ya mchezo wa kesho.
Alisema wachezaji 22 wa wanaocheza ndani na wale wa nje walishawasili, huku Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu walitarajiwa kuwasili jana mchana, kuungana na wenzao tayari kwa mchezo huo.
Katika mchezo wa Stars dhidi ya Nigeria uliofanyika hivi karibuni kwenye Uwanja wa Taifa, kiingilio cha mwisho kilikuwa Sh 7,000, bei ambayo baadhi ya watu walikilalamikia kuwa ni kikubwa.
Akizungumza na gazeti hili kuhusu maandalizi ya mchezo huo Kocha wa Taifa Stars, Charles Mkwassa alisema kikosi chake kinaendelea vizuri na mazoezi na wamejipanga kuhakikisha wanashinda.
“Wachezaji wote wako vizuri, tunaendelea na programu ya mazoezi na malengo yetu ni kushinda katika mchezo wa nyumbani ili kujiweka katika nafasi nzuri,” alisema. Alisema anajua kuwa Malawi ni timu yenye wachezaji wengi wapya na iko vizuri, na wanataka ushindi, lakini hata wao wamejipanga na wanaamini watafanya vizuri.
Baada ya mchezo huo, Taifa Stars itaanza maandalizi ya safari ya kwenda Malawi kwa ajili ya mchezo wa marudiano utakaochezwa Oktoba 11, mwaka huu. Wakati huo huo, waamuzi wa mchezo huo kutoka nchini Somalia, kamisaa na mtathimini waamuzi wa walitarajia kuwasili jana nchini na kufikia katika hoteli ya Protea iliyopo Oysterbay.
Mwamuzi wa kati ni Hagi Yabarow Wiish, akisaidiwa na Hamza Hagi Abdi, Salah Omar Abubakar, mwamuzi wa akiba Bashir Olad Arab (wote kutoka Somalia), mtathimini wa waamuzi Sam Essam Islam (Misri) na kamisaa wa mchezo ni Muzambi Gladmore (Zimbabwe).
Created by Gazeti HabariLeo.
0 comments:
Post a Comment