NA ABDUCADO EMMANUEL, DAR ES SALAAM
MTANZANIA Mbwana Samatta, anayekipiga katika timu ya TP Mazembe ya
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, amebakisha mabao mawili tu kuweza
kutwaa kiatu cha ufungaji bora wa michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika
mwaka huu.
Mpaka sasa timu yake ikiwa imeingia fainali ya michuano hiyo, Samatta
anashika nafasi ya pili kwenye chati ya ufungaji bora akiwa na mabao
sita, sawa na Mouhcine Iajour wa timu ya Moghreb Tetouan ya Morocco
iliyotolewa, anazidiwa bao moja tu na kinara Bakri Al-Madina anayekipiga
El Merreikh ya Sudan aliyetupia saba.
TP Mazembe inatarajia kucheza na USM Alger ya Algeria katika fainali
ya michuano hiyo, mchezo wa kwanza utafanyika kati ya Oktoba 30 na
Novemba mosi, mwaka huu huku wa marudiano ukifanyika kati ya Novemba 6
na 8 mwaka huu.
Mshambuliaji huyo, 23, ana nafasi ya kumzidi Al Madina kama
atafanikiwa kufunga mabao mawili katika mechi mbili zijazo za fainali
watakazocheza dhidi ya USM Algier.
Wachezaji wanaoweza kuyafikia mabao ya Samatta ni mshambuliaji
mwenzake wa TP Mazembe, Roger Assale, aliyefunga matano, Youcef Belaili
(USM Algier) aliyetupia manne sambamba na Kaddour Beldjilali na Mohamed
Meftah (USM Alger) waliotupia matatu kila mmoja.
Mwaka jana mshambuliaji mwingine wa Tanzania, Mrisho Ngassa,
aliyekuwa akikipiga Yanga alikuwa ni miongoni mwa wafungaji bora wa
michuano hiyo kwa mabao yake sita, akilingana na wenzake watatu, El Hedi
Belameiri (ES Setif, Algeria), Haythem Jouini (Esperance, Tunisia) na
Ndombe Mubele (AS Vita, Kongo).
Samatta anayecheza TP Mazembe sambamba na Mtanzania mwingine, Thomas
Ulimwengu, wana nafasi ya kuandika rekodi ya kuwa Watanzania wa kwanza
kutwaa ubingwa huo mkubwa wa Afrika kwa ngazi ya klabu kama wataifunga
USM Algier.
Chanzo Gazeti la HabariLeo
Tuesday, 6 October 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
badilisha template tunashindwa kuelewa vizuri habari imeisha au bado
ReplyDelete