Tuesday, 6 October 2015

Tagged Under:

Zaidi ya watoto 1,000 nchini wawekwa kizuizini

By: Unknown On: 04:11
  • Share The Gag

  • Waziri wa Afya, Dk Seifa Rashid.

    IDARA ya Ustawi wa Jamii iliyo chini ya Wizara ya Afya imesema kwamba taarifa ya ufuatiliaji wa mashauri ya watoto nchini ya mwaka 2014 ambayo iliandaliwa na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP) ilibainisha kuwepo kwa wastani wa watoto 1,000 waliowekwa megerezani.
    Kaimu Kamishna wa Idara ya Ustawi wa Jamii nchini, Rabikira Mushi, alisema hayo jana mjini hapa, wakati akifungua mafunzo ya siku tano yanayohusu utaratibu na uendeshaji wa kesi za watoto mahakamani kwa maafisa ustawi wa jamii na mahakimu kutoka mikoa mitano nchini.
    Alizitaja sababu za watoto hao kuhukumiwa kufungwa au kubaki mahabusu ni kukutwa wakiwa wamefanya makosa yanayokinzana na sheria pasipo wao kujua. Alitaja makosa hayo kuwa ni kujamiiana, kulawiti na mauaji.
    Alisema baadhi ya watoto hao wamekosa dhamana huku mashauri yao yakichukua muda mrefu unaotokana na uelewa mdogo wa sheria ya mtoto kwa Mahakimu, watendaji wa polisi pamoja na Maofisa Ustawi wa Jamii kutoshughulikia mashauri yao katika ngazi mbalimbali.
    Pia alisema taarifa hiyo ya uchuguzi ya DPP, ilibainisha kwamba Mahakama za Mwanzo zimeendelea kusikiliza kesi za watoto licha ya kutokuwa na mamkala kisheria ya kusikiliza mashauri hayo ambayo yanapaswa yasikilizwe na Hakimu Mkazi na si vinginevyo.
    Kutokana na changamoto hizo alisema lengo kuu la mafunzo hayo ni kuwawezesha kwa kuwajengea uwezo ili washiriki wote waweze kuwa na uelewa wa pamoja na wa kutosha juu ya mtoto aliyekinzana na sheria .
    Kaimu Kamishna wa idara hiyo alisema, mafunzo hayo yatawawezesha pia washiriki hususani Maofisa Ustawi wa Jamii katika ngazi za Halmashauri ili waanze kufuatilia mashauri ya watoto katika maeneo mbalimbali ili kutetea haki na maslahi yao wakiwa katika vituo vya polisi, magereza na pale shauri lao linapokuwa mahakamani.
    “Kwa kutekeleza mkataba wa kimataifa na wa kikanda, sheria ya mtoto namba 21 ya mwaka 2009, pamoja na kanuni zake, vinasisitiza kuwa nchi inawajibika kulinda hali na maslahi ya mtoto aliyekinzana na sheria,” alisema.
    Alisema mafunzo hayo ni ya muhimu kutokana na uzito wake ili kulinda hali, ustawi na maslahi ya watoto walio katika vizuizi vya polisi, magereza, mahabusu za watoto, mahakamani, shule ya maadilisho na katika jamii.
    Alisema utetezi wa haki na maslahi ya watoto ni jukumu la ofisa ustawi wa jamii kama sheria ya mtoto inavyomtaja na kwamba ili hakimu aweze kutoa hukumu kwa mtoto mwenye kesi mahakamani anategemea ushauri kutoka kwa ofisa ustawi wa jamii.
    Naye Kaimu Kamishna Msaidizi wa Idara ya Ustawi wa Jamii, Steven Gumbo, alisema lengo la mafunzo hayo ni kuwawezesha kwa kuwajengea uwezo maofisa ustawi wa jamii na mahakamu kuhusu namna ya kushughulikia mashauri ya watoto wanaokinzana na sheria.

    Chanzo Gazeti la HabariLeo.

    0 comments:

    Post a Comment