UPENDO MOSHA NA NORA DAMIAN
BAADHI ya Majimbo ya Kanisa Katoliki nchini, yametoa ruhusa maalum
kwa mapadri yakiwataka kuendesha ibada zao siku ya Jumamosi ya Oktoba 24
badala ya Jumapili mwaka huu ili kutoa nafasi kwa waamini wao kushiriki
Uchaguzi Mkuu wa rais, wabunge na madiwani kwa uhuru.
Hatua hiyo inatokana na siku ya Jumapili ambayo waamini wengi wa
kanisa hilo huabudu kuangukia Oktoba 25 ambayo ni siku ya Uchaguzi Mkuu.
Habari za uhakika ambazo MTANZANIA imezipata mjini Dar es Salaam jana
na kuthibitishwa na Makamu wa Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki
Tanzania (TEC), Askofu Severin Niwemugizi, zinasema kila askofu wa jimbo
ana mamlaka ya kutoa maelekezo ya aina hiyo kwa waamini wake.
Askofu Niwemugizi alisema kila askofu katika jimbo lake
anawajibika kufanya hivyo, kwani ni haki ya msingi ya waamini wake
kupiga kura.
“Kilitrujia siku ya bwana inaanza Jumamosi jioni, kwa msingi huo wanaweza pia kuadhimisha dominika bila tatizo lolote.
“Si utaratibu wa kawaida kwa sababu kama baraza hatujakaa, lakini kila
askofu anawajibika ndani ya jimbo lake, hivyo anaweza kutoa fursa
hiyo. “Hata mimi katika jimbo langu la Rulenge Ngara, nimetoa kibali
hicho kwa makanisa yote… kwa wanaotaka wala siwalazimishi wote,”
alisema Katika hatua nyingine, askofu huyo alizungumzia mwenendo wa
kampeni za uchaguzi, alisema amesikitishwa na dharau na
matusi yanayotolewa na wanasiasa katika
majukwa ya kampeni.
“Kumekuwa na lugha chafu, hakuna anayeona kama amefanya vibaya kwa
mwenzake,…. kwa mfano unamwita mwenzako oil chafu, maana yake unamdharau
muumba aliyemuumba hata kama ana upungufu.
Alisema tabia hiyo ya kutoleana lugha chafu ipo siku viongozi wa dini nao wategeukiwa.
MOSHI
Habari kutoka Jimbo Katoliki la Moshi mkoani Kilimanjaro na Mbulu
mkoani Manyara, zinasema kanisa hilo limetoa ruhusa maalumu kwa waamini
wa majimbo hayo kusali ibada ya Jumapili Oktoba 24, ili kutoa fursa kwa
waamini hao kwenda kupiga kura.
Uamuzi huo unatokana na waraka wa Askofu wa Jimbo Katoliki la Moshi,
Mhashamu Isaac Amani uliosambazwa katika makanisa yote ya majimbo hayo.
Waraka huo wenye kumbukumbu namba PROT Na. BSH/2657/2015- VIII/B
kwenda kwa mapdre, watawa na waamini walei, uliosainiwa na Askofu Aman
unawahimiza waamini wake kushiriki Uchaguzi Mkuu.
“Wakati kampeni za Uchaguzi Mkuu zikiendelea, ni muhimu wananchi
wafuatilie hotuba za wagombea ili hatimaye waweze kuchagua viongozi
wenye sera na sifa za kuleta maendeleo ya wananchi.
“Tunaendelea kumwomba Mungu atujalie amani wakati wa kampeni, siku ya
uchaguzi na baada ya uchaguzi wagombea na wananchi wayapokee matokeo
kwa utulivu na raha ya kudumisha umoja na amani ya kitaifa.
“Kwa kuwa siku ya uchaguzi ni Dominika, nawaletea tangazo
la kuboresha mazingira ya kupiga kura. Kwa waraka huu natoa
kibali maalumu kwa mapadre majimboni Mbulu, Moshi kufanya ibada
ya Dominika ya 30 ya mwaka huu siku ya Jumamosi Oktoba 24.
“Lengo la kibali hiki ni kuwapa wapiga kura fursa ya kupata
ibada Jumamosi jioni na Jumapili asubuhi ili wakapige kura mapema.
Hata Mapadre wanatakiwa kushiriki zoezi hili la kitaifa. Kwa hiyo
ratiba za misa zipangiliwe maparokiani na vigangoni kwa kuzingatia
kibali kilichotolewa.
“Natumia fursa hii kuwahimiza wale wote waliojiandikisha watumie haki
na wajibu wa kupiga kura ili tupate viongozi wazalendo tunaowapenda.
Kura yako ni muhimu katika harakati za kuwasaka viongozi,
madiwani,wabunge na rais.
“Usiachie wengine wakuchagulie viongozi wakati wewe unao wajibu wa
kupiga kura. Ukishapiga kura yako rudi nyumbani
ukangojee matokeo,”ilisema sehemu ya waraka huo.
Akizungumza na gazeti hili jana, Mhashamu Askofu Amani ambaye pia ni
msimamizi wa kitume wa Jimbo Katoliki la Mbulu alisema kutoa fursa hiyo
ni kuwataka waamini wake kutumia haki ya kidemokrasia ya kupata
viongozi.
Alisema ratiba za misa zote za ibada zitapangwa kwa parokia zote na
vigango vyote kwa mujibu wa kibali kilichotolewa na kanisa hilo.
Uamuzi huo wa kanisa unakwenda sambamba na ushauri uliowahi kutolewa
siku za nyuma na Jukwaa na Katiba Tanzania (JUKATA) pamoja na wadau
wengine. Wadau hao waliwahi kupendekeza kuhusu haja ya siku ya Uchaguzi
Mkuu ibadilishwe ili kutoa fursa kwa waamini ya dini ya Kikristu
kutumia vizuri haki yao ya kupiga kura, ili siku ya jumapili waitumie
kwa ajili ya ibada tu.
Utaratibu huo wa siku maalum ya kupiga kura ulitumiwa na nchi
ya Kenya katika uchaguzi mkuu uliopita, uliomuweka madarakani Rais
Uhuru Kenyatta.
Chanzo Gazeti la Mwananchi.
Tuesday, 6 October 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment