WIKI tatu zilizobaki, Watanzania wenye sifa za kupiga kura
waliojiandikisha watapiga kura yao ya msingi kuchagua viongozi
wawatakao, ambao ni rais, mbunge na diwani, ili washirikiane nao kuleta
maendeleo yao na taifa.
Wakati tukijiandaa kuelekeo kupiga kura, elimu ya uraia ni muhimu kwa
wananchi ili kuwahamasisha ushiriki wao katika demokrasia na kwamba
haipaswi kuwa na utashi wa kisiasa au upendeleo kwa chama chochote cha
siasa.
Elimu hiyo ya upigaji kura inapaswa kuzingatia miongozo iliyowekwa ya
kutofungamana na upande wowote kisiasa ili wapiga kura waelewe na
kuhakikisha wanatumia vyema nafasi yao kupiga kura yao kwa usahihi bila
woga wala mashaka.
Tunafahamu kwamba pamoja na wenye sifa kujiandikisha ili kupiga kura
yao kwenye uchaguzi mkuu ujao, lakini sio wote wanaofahamu kusoma na
kuandika, hivyo kwao kusoma machapisho yanayoelimisha elimu ya mpiga
kura ni vigumu kuelewa.
Kwa maana hiyo basi, tutambue kuna changamoto hiyo ambayo kama
hatutaishughulikia vyema, ni wazi kwamba kundi hilo la wasiojua kusoma
na kuandika, vilevile walemavu wasioona na wasiosikia, itakuwa vigumu
kwao kupata elimu hiyo.
Hivyo basi ni wajibu wetu kama jamii kushirikiana kusaidiana na pia
kuelekezana bila kupotoshana mambo muhimu ya kuzingatia ili kujiweka
kwenye upande sahihi wakati wa kupiga kura.
Kwa upande wa vyombo vya habari, wajibu wao ni kuendelea kuelimisha
jamii na kutoa vipindi vinavyoelekeza au kuelimisha umma jinsi ya kupiga
kura jambo ambalo litasaidia kupunguza uharibifu wa kura unaoweza
kutokea.
Katika uchaguzi wa mwaka huu, pamoja na kwamba wananchi wengi wana
mwamko na wamejitokeza kwa wingi kujiandikisha, lakini bado pia wapo
wachache ambao watawahadaa wapiga kura kwa kuwapandikiza mawazo mabaya
ili wasiende kupiga kura.
Mfano katika uchaguzi mkuu mwaka 2010 watu wachache walijitokeza
kupiga kura pamoja ingawa jitihada za uelimishaji zilifanywa kuhusu
kupiga kura lakini wachache walitumia fursa hiyo kusema hata wakipiga
hawapati faida, wala hakuleti mabadiliko.
Hayo ni maoni ya wachache wasiopenda maendeleo wala demokrasia,
lakini kwa uchaguzi wa mwaka huu mwamko wa wananchi kujiandikisha
ulikuwa mkubwa na ni vyema mwamko huo huo utumike pia kuelimishana mambo
muhimu ya kuzingatia wakati wa upigaji kura ili kuhakikisha kura
haiharibiki.
Sheria ya Taifa ya uchaguzi, inaeleza wazi kwamba mtu au mpiga kura
anayestahili kupiga kura ni yule aliyejiandikisha kwenye daftari la
kudumu la wapiga kura ,raia wa Tanzania, umri wa miaka 18 na kuendelea
na mkazi wa eneo husika la kupigia kura.
Mambo hayo ni muhimu wakati wa kupiga kura na kwamba elimu kuhusu
hayo inapaswa kutolewa kwa wananchi ili wafahamu na kuondokana na dhana
kwamba kwa vile wameshajiandikisha, wanaweza kupiga kura kwenye eneo
lolote, ili mradi tu awe na kitambulisho cha mpiga kura.
Hivyo basi ni wajibu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), ambayo ndiyo
yenye wajibu wa kuelimisha wapiga kura, kufanya hivyo ili elimu ya
uraia na upigaji kura iwafikie wote wenye sifa na waweze kutekeleza bila
kuvunja sheria.
Mfano wapo wananchi wasiofahamu kuwa kuvaa mavazi yenye rangi za
chama fulani au kuvaa nguo za chama fulani ni kosa wakati wa kwenda
kupiga kura. Wengine wanavaa tu kwa vile ni nguo jambo ambalo litamfanya
akose nafasi ya kupiga kura.
Sasa basi ni vyema mambo hayo muhimu yakaelezwa sasa ili ifikapo
Oktoba 25, kila mmoja wetu awe na uelewa na asifanye makosa yanayoweza
kumsababishia akose nafasi yake ya msingi ya kupiga kura.
Zikiwa zimebaki siku chache tu kupiga kura, ni vyema tuzitumie vyema
kuelimishana hata sisi kwa sisi juu ya mambo muhimu ya kuzingatia wakati
wa kupiga kura badala ya kuendelea kutupiana vijembe vya siasa baina ya
wagombea tuwapendao.
Kuendelea kubishana kuhusu wagombea mbalimbali na vyama vyao
hakusaidii, kinachotakiwa ni elimu kwa wananchi ili siku ya kupiga kura
watumie vyema nafasi hiyo kumpigia kura mgombea wamtakaye kwa kuwa
watakuwa na uhakika wa kura wapigazo zimefuata taratibu na
hazitaharibika.
Chanzo Gazeti la HabariLeo.
Sunday, 4 October 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment