IGO Ernest Mangu. |
POLISI Kanda Maalumu ya Dar es Salaam inawashikilia watu saba, wakiwemo sita wa familia moja kwa tuhuma za kujihusisha na vitendo vya ugaidi. Kukamatwa kwa watuhumiwa hao ni muendelezo wa operesheni inayoendeshwa na Polisi Kanda hiyo pamoja na mikoa jirani ya kuwatafuta watuhumiwa wote waliojihusisha na matukio ya kupanga kuvamia vituo vya polisi, kuua askari na raia na kupora silaha.
Akizungumza na waandishi wa habari jana ofisi kwake, Kamanda wa kanda hiyo, Kamishna Suleiman Kova alisema watuhumiwa hao sita ni wa familia ya mtuhumiwa aliyetajwa kama kiongozi wa kundi linalojihusisha na vitendo hivyo Ally Ulatule.
“Hawa watu sita ni miongoni mwa familia ya Ulatule na inaonekana wanahusika moja kwa moja na vitendo hivi, lakini jeshi la polisi tunaendelea na operesheni ya kuwatafuta wote waliohusika,” alisema Kova.
Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Said Mohamed Ulatule maarufu kama uso wa Simba (67), Hamis Ulatule (51), Ally Ulatule (65), Nassoro Ulatule (83) wote wakazi wa Mamdimkongo, Mkuranga mkoani Pwani, Said Chambeta maarufu kama Mzee wa Fasta (40) muuza mitumba mkazi wa Yombo Makangarawe na Ramadhani Ngande (29) dereva bodaboda mkazi wa Kongowe.
Watuhumiwa hao wanafanya idadi ya watu waliokamatwa kwa tuhuma za kujihusisha na ugaidi kufikia 7. Katika hatua nyingine, Kova alisema, wamefanikiwa kuwakamata watuhumiwa waliojihusisha na mauaji ya Ofisa wa Polisi Elibariki Palangyo yaliyotokea Agosti 4, mwaka huu nyumbani kwake Yombo Makangarawe jijini Dar es Salaam.
Hata hivyo alisema, kiongozi wa kundi hilo aliyemtaja kwa jina la Said Mazinge maarufu kama Omary Salehe au Bonge Mzito (39) alipigwa risasi na kujeruhiwa baada ya kujaribu kuwatoroka askari kwa kujirusha kutoka kwenye gari.
Aliwataja watuhumiwa wengine kuwa ni Rashid Watson maarufu kama Dodo (21), Ramadhani Salum maarufu kama Nguzo (38), Bakari Rashid (38) na Hamis Hamis maarufu kama Freemason (24).
Alisema mtuhumiwa Watson alikamatwa maeneo ya Vingunguti akiwa na silaha aina ya Shotgun iliyokatwa mtutu na kutengenezwa kienyeji ikiwa na risasi nne na betri mbili zilizounganishwa kwa ajili ya kulipua baruti.
Aidha alisema, wamekamata bunduki aina ya SMG moja, shotgun mbili, bastola moja pamoja na risasi 14. Aidha, alisema Polisi wamefanikiwa kuokoa mali yenye thamani ya Sh milioni 159.
Chanzo Gazeti la HabariLeo.
0 comments:
Post a Comment