ZIMEBAKI siku 18 tu kuanzia leo hadi kufikia siku inayosubiriwa kwa
hamu na Watanzania mwaka huu, yaani Oktoba 25, ili kutumia haki yao ya
kikatiba ya kuwachagua viongozi wa kuwavusha katika kipindi cha miaka
mitano ijayo. Katika uchaguzi huo mkuu Watanzania watawachagua madiwani,
wabunge, wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na rais.
Kwa kuzingatia umuhimu wa shughuli hiyo na upatikanaji wa taarifa
sahihi kwa wanachi, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) tayari imeanza
kusambaza karatasi za kura za mfano kwa halmashauri zote nchini ili
wagombea wahakiki majina yao.
Karatasi hizo pia zitatumika katika harakati za kutolea elimu kwa
wapiga kura wafahamu wanapotakiwa kuweka alama ya vema kumchagua mgombea
wanayemtaka ili kuepuka kuharibu kura zao.
Taarifa rasmi zimeeleza wazi kwamba hadi leo hii, inatarajiwa
halmashauri zote nchini ziwe zimekwishapata karatasi hizo. Karatasi hizo
pia zimetolewa ili kupata marekebisho katika maeneo yanayohitajika
kabla ya siku yenyewe ya tukio la kupiga kura.
Kila halmashauri itapatiwa nakala 200 zitakazogawiwa kwa wagombea ili
wazitumie kutolea elimu kwa wapiga kura wao na kufanya usahihi wa
majina ya wagombea iwapo yatakuwa yamekosewa.
Hakuna ubishi kwamba hatua zote hizo zinalenga kutufikisha katika
hatua za kutuwezesha kufanya uchaguzi huru na haki kwa wagombea na pia
kwa wapiga kura kupata kile wanachokihitaji kutokana na atakayeibuka
mshindi dhidi ya wapinzani wake katika kinyang’anyiro cha kupata nafasi
hizo muhimu za uongozi wa nchi yetu.
Tunapenda kuwakumbusha wadau wote katika hili wakiwemo watendaji wa
halmashauri, wasimamizi wa uchaguzi na wasaidizi wao, wapiga kura na
wagombea kwamba kila mmoja wetu achukue nafasi yake kuhakikisha mambo
yote muhimu kama yalivyopangwa yanafanyiwa kazi ipasavyo na kinyume
chake atakayejaribu kufanya tofauti ashughulikiwe kwa mujibu wa sheria
na taratibu kwa sababu hakutakuwa na sababu nyingine nje ya kutotutakia
mema.
Tunaamini kwamba hayo yakizingatiwa hakutakuwa na malalamiko yasiyo
ya lazima ya kutufikisha katika tafrani ya kuvuruga amani, utulivu,
upendo na mshikamano wetu uliojengeka tangu tupate uhuru wetu Desemba 9,
1961 hadi sasa tunapotaraji kufanya uchaguzi wa kuwapata viongozi wa
kutuongeza kwenye serikali ya Awamu ya Tano.
Sote ni mashahidi kwamba karibu nchi za wenzetu mbalimbali duniani
inapofikia suala la kubadilisha uongozi wa juu wa nchi kwa maaana ya
kufanya uchaguzi mkuu, vurugu hutawala kipindi husika kiasi cha
kusababisha kuvurugika kwa amani, kusababisha vita na raia kuikimbia
nchi yao wenyewe ili kuokoa nafsi zao.
Hatuna haja ya mtu yeyote kuja kutueleza hili kwa sababu sisi kama
Tanzania tumekuwa tukipokea wakimbizi kutoka nchi mbalimbali kutokana na
hali kama hiyo ya kutozingatia haki katika usimamizi wa masuala ya
uchaguzi mkuu.
Ndiyo maana tunasema, atakayetaka kutupotosha kwa makusudi kwa
maslahi yake au vikundi ili tutumbukie katika janga la vurugu,
tusimwonee haya kamwe. Mungu Ibariki Tanzania.
Chanzo Gazeti la HabariLeo.
Tuesday, 6 October 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment