Tuesday, 6 October 2015

Tagged Under:

Simba yaanza kuzipigia ramli Prisons, Mbeya City

By: Unknown On: 12:54
  • Share The Gag
  • Asha Kigundula
    KIKOSI cha timu ya Simba, kesho kitaingia kambini kujiandaa na mechi zake za Ligi Kuu Bara, ambapo zitaendelea Oktoba 17, mwaka huu kwa kusafiri hadi mkoani Mbeya.
    Akizungumza Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa Klabu ya Simba, Haji Manara alisema kikosi hicho kilichoanza mazoezi jana kwenye viwanja vya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), kitaingia kambini kujiandaa na mechi zilizopo mbele yao.
    Manara alisema anachojua kambi itakuwa Dar es Salaam, lakini hajajua itakuwa wapi.
    Alisema kikosi hicho kinachoondoka Dar es Salaam Jumatatu ijayo kwenda mkoani Mbeya kwa ajili ya mchezo wake dhidi ya Mbeya City na Prisons, ambazo zitafanyika kwenye Uwanja wa Sokoine mkoani humo, watahakikisha wanajiandaa kwenda kuzoa pointi zote sita.
    Aidha Manara alisema jana jioni mara baada ya mazoezi kulikuwa na zoezi la utoaji zawadi ya mwezi kwa mchezaji wa timu hiyo aliyefanya vizuri Septemba.
    Manara alisema mchezaji atachaguliwa kwa kura zinazopigwa na Wanasimba wenyewe, atapata kitita cha sh. 500,000 kama zawadi.
    Simba iliwapa siku mbili za mapumziko wachezaji wao baada ya baadhi ya wachezaji wao kuwa kwenye timu ya Taifa (Taifa Stars), ambayo kesho itacheza mechi ya dhidi ya Malawi kuwania kufuzu kucheza Kombe la Dunia 2018 Urusi.
    Timu hiyo kwenye msimamo wa ligi hiyo inashika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 12 ikitanguliwa na Azam FC na Yanga zenye pointi 15 ila zinatofautiana kwa mabao.

    0 comments:

    Post a Comment