RAIS Jakaya Kikwete amelihutubia Bunge la Kenya na kuwaaga wananchi
wa Kenya huku akisisitiza ushirikiano kati ya Tanzania na Kenya kwamba
utadumu milele. Aidha, amesema anaamini Wakenya watakuwa wamepata
fundisho kutokana na machafuko yaliyotokana na uchaguzi wa mwaka 2007 na
hawatarudia tena.
Katika hotuba yake aliyotumia lugha ya Kiingereza kwa dakika 15 na
kisha akaombwa kuzungumza kwa Kiswahili na wabunge na maseneta, Rais
Kikwete alisema uhusiano wa Kenya na Tanzania ni wa kidugu zaidi na
kwamba hata kama anaondoka madarakani, anaamini utaendelea kwa sababu
zipo sababu za msingi za kufanya hivyo.
Alisisitiza kuwa, Kenya ni mshirika mkubwa wa Tanzania katika
maendeleo na kwamba kwa vyovyote, vile sera hiyo haitabadilika kutokana
na umuhimu wake. Akifafanua, alisema Kenya na Tanzania zimekuwa
washirika wakubwa katika masuala ya kiuchumi, kijamii, kisiasa na
kidiplomasia, hali ambayo inaifanya iendelee kuwa na ushirikiano wa
kudumu.
Akitoa mfano, alisema kumekuwa na ushirikiano katika kuunganisha
barabara za nchi hizo, kwenye huduma za umeme, na sasa hivi mradi mpya
wa gesi ya Mtwara ambayo Kenya itanunua kutoka Tanzania.
“Katika mazungumzo na Rais Uhuru Kenyatta tulikubaliana kuanza mradi
wa kupeleka umeme Kenya na tutaanza na kilovoti 400 kwa kujenga mtambo
wa kupeleka umeme huko,“ alisema Rais Kikwete.
Alisema kilovoti hizo 400 ni sehemu ya mahitaji ya kilovoti 1000
ambayo Kenya itapatiwa na Tanzania katika mradi huo. Pia alisema,
kuhusiana na gesi Kenya itanunua gesi kutoka Tanzania ili kurahisisha
maendeleo ya nchi hiyo kwa sababu itapatikana kwa bei rahisi na itakuwa
ya kuaminika.
Kuhusu siasa aliwakumbusha kwamba ni vyema Kenya mpya ikaendelea kuwa
ya amani na utulivu na kwamba machafuko ya 2007 yawe ni fundisho kwao.
Aliwaahidi wabunge na maseneta wa Kenya kwamba atabaki kuwa rafiki wa
kweli wa Kenya na kwamba baada ya kumaliza muda wake wa uongozi atakuwa
anawatembelea mara kwa mara.
Apewa barabara ya Ikulu Aidha, wakati leo akiadhimisha miaka 65 ya
kuzaliwa kwake, mapema jana Rais Jakaya Kikwete alipewa zawadi ya kudumu
ya bethidei nchini hapa, baada ya Mamlaka ya Jiji la Nairobi kuipa jina
lake moja ya barabara za jiji hilo.
Rais Kikwete ambaye jana alihitimisha ziara yake ya siku tatu ya
kiserikali nchini Kenya, atakumbukwa daima hapa baada ya Barabara ya
Mlimani sasa kuanzia jana itajulikana kwa jina la Barabara ya Jakaya
Kikwete. Barabara hiyo inaanzia katika makazi ya Rais wa Kenya, Uhuru
Kenyatta, karibu kabisa na Ikulu ya nchi hii.
Rais Kikwete alizindua barabara iliyopewa jina lake jana saa tano
asubuhi katika eneo jirani na geti la kuingia katika makazi ya Rais
Uhuru. Katika shughuli hiyo, vijana wa eneo hilo la Jimbo la Dagoretti
North ambalo Mbunge wake ni Simba Arat na anayeonekana kupendwa na
wananchi wake, walikuwa wamebeba mabango yenye ujumbe wa kufurahia Rais
Kikwete kupewa barabara hiyo, huku wakiimba na kucheza wimbo maarufu wa
My Number One wa msanii Nassib Abdul `Diamond Platnumz’ wa Tanzania.
Mabango hayo mawili yalikuwa yameandikwa, “Vijana wa Mlimani sasa ni
vijana wa Kikwete,” na jingine “Kikwete karibu Kikwete Road.”
Akizungumza katika shughuli hiyo, Gavana wa Kaunti ya Nairobi, Evans
Kidero alisema mara nyingi watu kwa Kenya vitu hupewa majina ya wapendwa
wao.
Alisema moja, watu huwapa majina watoto wao kutokana na majina ya
marafiki zao na kwa Kenya, jina la Rais Kikwete wamepewa watoto wengi.
Gavana aliongeza kuwa na pia majina ya marafiki wapendwa hupewa shamba
au barabara, ndio maana wameamua kuipa barabara hiyo jina la Rais
Kikwete.
“Kutokana na urafiki wako mkubwa na uhusiano mwema na Rais Uhuru
Kenyatta, barabara hii ya Mlimani Road, sasa itajulikana kwa jina la
Barabara ya Jakaya Kikwete,” alisema Kidero na kuongeza: Akizungumza
katika hafla hiyo, Rais Kikwete alisema hana maneno ya kutosha kuonesha
furaha yake kwa uamuzi huo wa Jiji la Nairobi kumpa barabara yenye jina
lake.
“Rais Uhuru jana (juzi) aliniuliza kuhusu suala hilo kama nalikubali,
nami nilimjibu kama mmeamua hivyo, sina pingamizi. Mmenikabidhi funguo
za Jiji la Nairobi na sasa mmeipa barabara jina langu, hii ni habari
kubwa. Rais Kikwete pia jana alitembelea kiwanda cha magari cha General
Motors East African Limited, na baadaye kulihutubia Bunge la Kenya na
jioni alirejea nchini.
Created by Gazeti la HabariLeo.
Tuesday, 6 October 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment