Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadik. |
MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam Said Mecky Sadiki amewataka waratibu wa uchaguzi, wasimamizi wa uchaguzi na viongozi wa vyama vya siasa katika mkoa huo kuhakikisha kuwa wanafanya kazi zao kwa ushirikiano ili kuwawezesha wananchi kupiga kura kwa amani na utulivu na kuepusha manung’uniko yasiyokuwa na maana.
Akifungua mafunzo ya siku mbili ya waratibu wa uchaguzi, wasimamizi wa uchaguzi, wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi na maofia uchaguzi jana jijini Dar es Salaam, Sadiki alisema mkoa wa Dar es Salaam ni miongoni mwa maeneo yenye wapiga kura wengi hivyo mkoa kwa kushirikiana na Tume ya Uchaguzi umejipanga kuhakikisha kuwa wananchi wote waliojiandikisha wanapiga kura kwa amani na utulivu siku ya uchaguzi Oktoba 25 mwaka huu.
Alisema wakurugenzi wa halmashauri wa mkoa huo ambao ndiyo wasimamizi wa uchaguzi katika wilaya wanalo jukumu la kuwaita na kuwaelimisha viongozi wa vyama vya siasa juu ya taratibu na kanuni za kufuata wakati wa uchaguzi mkuu ili wajenge mazingira rafiki ya kufanya kazi kwa ushirikiano.
Aliwasisitiza wasimamizi hao kutojihusisha kwa namna yoyote ile na kampeni za siasa wakati wa kutekeleza majukumu yao kwani kufanya hivyo watakuwa wanahujumu ufanisi wa uchaguzi mkuu katika mkoa wa Dar es Salaam.
Kuhusu waangalizi wa Kimataifa waliowasili nchini ambao baadhi yao watafanya kazi jijini Dar es Salaam alisema watafanya kazi zao kwa mujibu wa taratibu na kanuni walizopewa na Tume na kuongeza kuwa kazi yao itakuwa ni kuangalia kama tunazingatia na kufuata sheria tulizojiwekea na si kuingilia shughuli za wasimamizi wa zoezi la upigaji wa kura.
Aidha, amevitaka vyama vya siasa kuhakikisha kuwa vinawapeleka mawakala wao mapema katika vituo vya kupigia kura kabla ya kuanza kwa zoezi la upigaji wa kura ili kuondoa manung’uniko yanayoweza kujitokeza.
Kwa upande wake Clesensia Mayala ambaye ni Kaimu Mkuu wa Sehemu, Kanda ya Kusini Tume ya Taifa ya Uchaguzi alisema lengo la mafunzo hayo ni kuwakumbusha wasimamizi na mofisa uchaguzi kuzingatia na kufuata taratibu zilizotolewa na Tume ili waweze kufanya kazi zao kwa ufanisi.
Chanzo Gazeti la HabariLeo.
0 comments:
Post a Comment